Tuesday, January 19, 2016

KAMA UNA TABIA KAMA HIZI, MAFANIKIO UTAYASIKIA KWA WENZAKO TU!




Ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea vyema na shughuli zako za kila siku kama kawaida.

Mimi namshukuru Mungu kwa kila jambo ambalo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu na hakika nitaendelea kumhimidi ili aweze kuniwekea mkono kwenye kila nilifanyalo.

Mpenzi msomaji wangu, kama wewe ni mfuatiliaji wa safu hii, utakumbuka wiki iliyopita nilianza kuzungumizia mada hii na nikaishia kuzungumzia tabia ya kukata tamaa.
 
Nikasema kwamba, watu wanaotaka kufanikiwa huchukulia kushindwa kama hatua ya kuelekea kwenye mafanikio, lakini watu wasioweza kufanikiwa wanapojaribu mara moja au mbili kuvuka kikwazo fulani cha kimaisha na kushindwa, hukata tamaa na kutotaka kujaribu tena kusonga mbele.

Wenye tabia ya kushindwa kimaisha hawako tayari kudumu na jambo moja linaloonekana kushindikana kwao kwa muda mrefu. Akiona mwanamke ambaye ni mkorofi kidogo, haraka hukimbilia kumwacha na kutafuta mwingine, mara nyingi si watu wavumilivu.

Akijaribu biashara ya vitumbua kwa wiki moja na akaona havinunuliwi, anaanza kupika maandazi, wiki moja baadaye yuko kwenye mihogo, basi ilimradi kuhangaika kusikokuwa na tija katika maisha.

Ukitaka kuwa mmoja kati ya watu wasioweza kufanikiwa kimaisha, jaribu kuishi maisha ya kukata tamaa mapema unapofanya mambo.

Kujaribu kuwarudisha nyuma wengine
Mara nyingi watu walioshindwa kimaisha huwa na tabia za kuwashawishi watu wengine wawe kama wao katika mawazo na matendo.

Tabia za watu wa aina hii huwa si za kimaendeleo kwa vile wao hudhani kuwa njia zao ni sahihi na hivyo hujaribu kwa nguvu zao kuwarudisha wengine nyuma ili wawe kama wao. Ni watu wenye wivu wa ‘kijinga’, wakiona mwingine anaendelea katika hiki na kile humpiga vita ili afilisike.

Ni wafitini na wachonganishi
Wenye tabia za kutofanikiwa hudhani kuwa kukwama kwao hutokana na vikwazo vinavyoletwa na wengine.

Kupoteza muda mwingi bure
Watu ambao hawawezi kufanikiwa ni wale ambao hupoteza muda mwingi kufanya mambo yasiyokuwa na tija, kwa kuangalia TV, kusengenya watu, kunywa pombe, kufanya starehe na kutumia muda hovyo kwenye kazi ambazo hazina msaada kwao.

Wapo watu mahodari wa kutembelea kwenye nyumba za wengine na kuongea huko kutwa nzima bila kujali kama muda waliopoteza wangeweza kufanya kazi na kujipatia kipato.

Hizo ni baadhi tu ya tabia ambazo unatakiwa kuziepuka kama tu unataka kufanikiwa. Kumbuka katika kufanikisha kila jambo kuna kanuni, hivyo kama unataka kuwa miongoni mwa waliofanikiwa, fuata kanuni za mafanikio.


0 Responses to “ KAMA UNA TABIA KAMA HIZI, MAFANIKIO UTAYASIKIA KWA WENZAKO TU!”

Post a Comment

More to Read