Friday, January 22, 2016

MGOGORO SUGU KUHUSU MPAKA WA WILAYA MBILI MKOANI MBEYA KUPATIWA SULUHU.





NA SAMWEL NDONI, MBEYA
SERIKALI mkoani Mbeya kwa kushirikiana na wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi inatarajia kuunda timu ya wataalamu watakaotambua na kubainisha mipaka ya wilaya za  Mbozi na Chunya ili kumaliza mgogoro wa mipaka kwenye wilaya hizo.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amesema hayo hivi karibuni kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Magamba uliopo wilayani Mbozi mkoani Mbeya ambao upo mpakani mwa wilaya hizo Mbili.

Amesema hali hiyo imezua mgogoro kati ya wananchi wa wilaya hizo Mbili ambao kila upande unadai kuwa mgodi upo upande wake.

Hata hivyo kandoro alisema tayari wamekubaliana na waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuunda timu ya wataalamu wakaobainisha mipaka halisi ya wilaya hizo mbili ili kumaliza mgogoro huo.

“Tumeshakubaliana na waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi tuunde timu ya wataalamu ambao watawasili muda wowote kwa ajili ya kubainisha na kutambua uhalisia wa mipaka hiyo ili tumalize mgogoro,”amesema

Aidha Kandoro alieleza kuwa mgogoro huo uliibuka baada ya eneo hilo kugundulika kuwa na madini ya makaa ya mawe hali ambayo iliifanya kila halmashauri kutaka kupata asilimia 0.3 ya mapato kutoka kwa mwekezaji wa mgodi huo.

Vilevile Kandoro alisema endapo itabainika kuwa makaa yapo ndani ya mpaka wa wilaya hizo Mbili itabidi gawio la asilimia 0.3 litagawanywa kwa halmashauri zote mbili kulingana na ukubwa wa eneo lenye madini kwa kila halmashauri.

Awali mkuu wa wilaya ya Mbozi, Ahamed Namohe alimweleza mkuu wa mkoa kuwa mgogoro huo ulishika kasi baada ya wananchi wa wilaya ya Chunya kuhamisha alama za mipaka na kuzisogeza upande wa Mbozi.
MWISHO

0 Responses to “MGOGORO SUGU KUHUSU MPAKA WA WILAYA MBILI MKOANI MBEYA KUPATIWA SULUHU.”

Post a Comment

More to Read