Thursday, January 7, 2016

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC),MKOA WA MBEYA LADAI TAASISI ZAIDI YA SHILLING MILLION 45




                                                                                                                                           
NA SAMWELI NDONI, MBEYA                  
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), Mkoa wa Mbeya linazidai taasisi za umma zaidi ya shilingi milioni 45 ikiwa ni malimbikizo ya malipo ya pango ya mwaka uliopita hali ambayo inadaiwa kukwamisha shughuli za shirika hilo.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Shirika hilo Mkoa wa Mbeya ambaye pia anashughulikia Mkoa wa Njombe, Juma Kiaramba, mbele ya Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, William Lukuvi alipotembelea shirika hilo ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani hapa.

Kiaramba alizitaja taasisis zinazodaiwa na Shirika lake kuwa ni pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambalo linadaiwa kiasi cha shilingi milioni 30.5 na kwamba ndiyo taasisis inayodaiwa fedha nyingi kuliko zote.

Alizitaja taasisi zingine kuwa zinazodaiwa malimbikizo ya madeni hayo kuwa ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo inadaiwa shilingi milioni 9.9, Mkuu wa Polisi shilingi milion 1.5 pamoja na Hospitali ya kanda ya Rufaa Mbeya ambayo inadaiwa shilingi miloni 3.

“Mheshimiwa Waziri kuna baadhi ya kazi za shirika zinakwama kutoka na baadhi ya wateja wetu hasa taasisi za umma zinalimbikiza madeni, ambapo mpaka sasa kuna malimbikizo ya madeni ambayo mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka uliopita deni tunalodai taasisi hizo limefikia shilingi milioni 43.5, na miongoni mwa taasisi hizo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania, ofisi ya mwanasheria mkuu, Hospitali ya Rufaa na Ofisi ya Mkuu wa Polisi,” alisema Kiaramba.

Aidha Kiaramba alisema kuwa malimbikizo ya madeni hayo yanatokana na utaratibu uliowekwa na Serikali wa kulipa madeni kwa kupitia Hazina ndogo, wakati madeni ya Jeshi la wananchi wa Tanzania yanalipwa kupitia uongozi wa shirika ngazi ya juu unaendelea.

Vilevile Kiaramba alisema kuwa NHC mkoa wa Mbeya lina jumla ya majengo 42 yenye sehemu za kupangisha 200 ambapo kwa mwaka uliopita shirika lilikusanya zaidi ya shilingi bilioni moja huku mwaka huu likitarajia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.3

Alimwambia waziri Lukuvi kuwa shirika linaendelea na miradi ya kujenga nyumba za bei nafuu ili watanzania wengi zaidi waweze kununua, ambapo alisema tayari wana miradi mitatu ambayo ipo katika hatua za utekelezaji.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na nyumba 14 ambazo zinajengwa katika Halmashauri Mpya ya Busokelo wilayani Rungwe ambazo zote zimenunuliwa na Halmashauri hiyo, mradi wa nyumba 50 Wilaya ya Makete na nyumba 14 katika Halmashauri ya Momba.

Kwa upande wake waziri Lukuvi aliushauri uongozi wa Shirika hili la Nyumba la taifa (NHC)kuongeza bidii ya kufuatilia madeni kutoka kwa taasisi za umma zinazodaiwa pamoja ili kukamilisha miradi mingine iliyopo
Alishauri pia Shirika kuendelea na ujenzi wa nyumba za bei nafuu mpaka vijijini ilikupanua wigo wa watanzania wengi zaidi kuweza kumiliki nyumba.

“Hakikisheni mnaongeza bidii katika kudai madeni yenu ili muweze kukamilisha miradi ambayo mnatekeleza, lakini pia msijenge nyumba maeneo ya mjini tu bali jengeni hadi vijijini na kwa sababu nyumba zenu ni za bei nafuu watu wengi zaidi watashawishika kununua,” alisema Lukuvi.
Vilevile alishauri NHC kuendelea na ubunifu wa vifaa vya ujenzi vya bei nafuu ili nyumba zake ziendelee kupungua bei na shirika lipate faida zaidi.
Mwisho.

0 Responses to “SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC),MKOA WA MBEYA LADAI TAASISI ZAIDI YA SHILLING MILLION 45 ”

Post a Comment

More to Read