Thursday, January 7, 2016

TFDA KUTAIFISHA MAGARI YATAKAYOBEBA VIPODOZI NA VYAKULA AMBAVYO SI BORA KWA MATUMIZI YA BINADAMU.




NA SAMWEL NDONI, MBEYA
MAMLAKA ya chakula na dawa nchini,kanda ya nyanda za juu kusini (TFDA) imetishia kuyakamata na kuyataifisha magari yatakayobainika kutumika kusafirisha bidhaa zilizopigwa marufuku na serikali kwa ajili ya matumizi ya binadamu ikiwa ni mkakati wa kutomeza bidhaa hizo.

Akizungumza na Blog ya Fahari News ofisini kwake meneja wa TFDA, kanda ya nyanda za juu kusini Rodney Alananga alisema kuwa hatua hiyo itaongeza mfumo wa udhibiti wa bidhaa zilizopigwa marufuku na serikali zinazotengenezwa ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na ofisi za wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini itakuwa ikifanya kaguzi za kushtukiza kwenye magari mbalimbali na kwamba yatakayobainika yamebeba bidhaa hizo kinyume cha sheria yatataifishwa.

“Tumekuwa na changamoto kwenye suala la uingizaji wa bidhaa hizi kwani baadhi ya wafanyabiashara wanazipitishwa kwa kutumia njia za panya, mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine zikiwemo ofisi za wakuu wa mikoa tumekubalina kuwa tutafanya kaguzi za kushtukiza kwenye, mipaka na kwenye magari na itakapobainika gari limebeba bidhaa hizo kunauwezekano gari hilo likaifishwa” amesema.

Amesema TFDA,itaendelea kushirikiana na wadau wengine ikiwemo ofisi ya waziri mkuu tawala za mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi), na halmashauri kudhibiti bidhaa hizo na kuwataka wafanyabiashara kufanya baishara ziilizoruhusiwa kisheria.

Alanaga amesema kuwa TFDA,imepiga marufuku matumizi ya vyakula na madawa ambayo yamegunduliwa kuwa na madhara kwa binadamu vikiwemo vipodozi 550, baada ya kuthibitika kuwa na viambata vyenye sumu.

“kuna vipodozi 550, ambavyo vimepigwa marufuku na serikali baada ya kufanyiwa uchunguzi vilibainika kwamba vina viambata vyenye sumu, baadhi yake ni Carolight ambayo inapendwa kutumiwa na watu wengi, vingine ni Ectra Claire,Diproson, Mount Claire,Claire man,Betasol,Movate,removate, miki craile na vingine” amesema.

Amesema kuna madhara ya muda mfupi na ya muda mrefu yanayoweza kutokea baada ya kutumia vipodozi hivyo ambapo ya muda mfupi ni kutokwa na upele,kulainisha ngozi ambayo inapunguza kiwango cha kutoa kinga ya mwili.
Madhara ya muda mrefu ni kansa ya damu,kansa ya ngozi, matatizo wakati wa kujifungua kwa wakina mama wajawazito au kujifungua watoto wenye uzio wa ubongo,kuchelewa kupona majeraha baada ya kuumia.
MWISHO

0 Responses to “TFDA KUTAIFISHA MAGARI YATAKAYOBEBA VIPODOZI NA VYAKULA AMBAVYO SI BORA KWA MATUMIZI YA BINADAMU.”

Post a Comment

More to Read