Tuesday, January 5, 2016
WAZIRI WA MALIASILI PROF.MAGHEMBE AMSIMAMISHA KAZI MAOFISA MISITU NCHI NZIMA
Do you like this story?
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) Bw. Juma Mgoo (kulia) akiwasilisha taarifa
ya ofisi yake kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Prof.
Jumanne Maghembe (wa tatu kulia
|
Waziri wa Maliasili na
Utalii Prof. Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na
Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) Bw. Mohammed Kilongo na Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima
kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.
Akizungumza leo na
Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam, Prof. Maghembe
amesema agizo hilo limekuja kutokana na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa
ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika
Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Ameagiza pia maofisa
hao wote wanaokusanya maduhuri ya Serikali katika Wilaya watumie muda wa siku
kumi kuanzia leo kuhakikisha maduhuri yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki
ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo
watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Wale district
forestry officers wote wapeleke vitabu vyao wanavyokusanyia maduhuri ya
Serikali kwenye ofisi za Kanda, Naibu Katibu Mkuu tusaidie kuwasiliana na Ofisi
ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali ifanye ukaguzi wa vitabu hivyo ndani ya siku kumi
tuhakikishe fedha zinazotakiwa zinaingia kwenye mfuko wa Serikali, Mtu
anakusanya fedha ya Serikali toka mwaka 2004 mpaka leo hajapeleka benki
ananeemesha hali yake ya nyumbani, hili hapana”. Alisisitiza Prof. Maghembe.
Kwa mujibu wa Waziri
Maghembe Bw. Mohammed Kilongo ambaye Idara yake ndiyo inatoa vitabu kwa ajili ya
kukusanya maduhuri ya Serikali katika Mikoa yote na Wilaya zote nchini
analazimika kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi ambapo ukikamilika sheria
itachukua mkondo wake bila uonevu wowote.
Katika hatua nyingine
Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amewaagiza pia Wakala wa Huduma za Misitu
nchini (TFS) kutumia muda wa siku saba kurudi katika jengo la Wizara ya
Maliasili na Utalii maarufu kama Mpingo House ambalo walihama mwishoni mwa
mwezi Septemba mwaka jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF Mafao House
lililopo Ilala.
“Wakati tunajenga
nyumba hii hapa, tumejenga jengo hili ni kama jengo la misitu ndio maana
linaitwa Mpingo House kwa maana ni jengo la Misitu, ninyi wenyewe mmejenga
jengo kubwa hili mmemaliza mmehama, Naagiza jumatatu Desemba 11 muwe mmesharudi
katika jengo hili, ghorofa ya tatu nikija kukagua niwakute, haiwezekani mueleze
matatizo yote mliyonayo muhame nyumba ya Serikali mkapange jengo hapo jirani”
Alisema Prof. Maghembe.
Katika hatua nyingine
ya kuboresha uhifadhi wa Misitu nchini Waziri Maghembe ameiagiza Idara ya
Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili kuhakikisha inajiimarisha katika lengo
lake kuu la uhifadhi kwa kushirikiana na wadau wanaohusika kuhakikisha Mamlaka
iliyolengwa ya Uhifadhi Misitu inakamilika.
“Tunataka tutoke
kwenye Wakala wa Huduma za Misitu (Tanzania Forestry Services Agency) twende
kwenye Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu (Tanzania Forestry Services Authority) ili
tuweze kufanya vizuri zaidi kwenye eneo la uhifadhi na uendelezaji wa misitu
nchini, Katibu Mkuu tunaomba pia usaidie kufanikisha hili” Alisema Prof
Maghembe.
Aliongeza kuwa wakati
wa kuundwa Mamlaka hiyo ni vizuri pia Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya
Maliasili ikatenganishwa na kila moja kuwa Idara kamili kutokana na umuhimu wa
kila sekta katika kujenga uchumi wa nchi kwa kutoa fursa ya kuboresha maeneo
hayo na kuongeza pato la taifa.
Ameitaka pia Idara ya
Misitu na nyuki kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhakikisha kuwa
inaongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya yote ya ubadhilifu
pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo.
Akizungumzia mchango
wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwenye pato la taifa Mtendaji Mkuu, Bw.
Juma Mgoo amesema katika mwaka huu wa fedha TFS imeweka makisio ya kukusanya
Tsh. Bilioni 88 ambapo mpaka hivi sasa wameshakusanya zaidi ya asilimia 20 na
makisio hayo.
Waziri Maghembe
akizungumzia kuhusu uvamizi kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba
amewataka wananchi wote waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa kwa ajili ya
kuchunga mifugo waondoke ndani ya siku saba zijazo, na wale walivamia mapori ya
akiba kwa shughuli za kilimo na ufugaji waondoke ndani ya miezi mitatu ijayo.
"Serikali
itawaondoa kwa nguvu wasipotekeleza agizo hili la kuondoka katika maeneo ya
hifadhi za taifa na kwenye mapori ya akiba yaliyohifadhiwa” Alisisitiza Prof.
Maghembe.
Akizungumzia kuhusu
biashara ya Mkaa, Prof. Maghembe amewaagiza wataalamu wa Idara ya Misitu
kusimamia biashara ya mkaa kwa kuzingatia taratibu na sheria ikiwa ni pamoja na
kuzuia usafirishaji wa Mkaa nje ya nchi.
Ameongeza kuwa nishati
ya Mkaa ni muhimu lakini Tanzania ina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe ambapo
ameitaka Idara ya Misitu kwa kushirikiana na wadau wengine kuona ni namna gani
ya kuweza kutumia mbadala huo kwa kuzalisha makaa hayo ya mawe kwa matumizi ya
kawaida ili kuokoa misitu nchini.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema kuwa maagizo yote
yaliyotolewa na Waziri yatafanyiwa kazi kwakuwa lengo lake ni kuona dhamira ya
msingi ya Serikali ya awamu ya tano inafikiwa ya kubana matumizi, kuongeza
mapato ya Serikali na kuhifadhi maliasili za taifa ikiwemo misitu.
(Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maliasili na Utalii - www.wizarayamaliasilinautalii.blogspot.com)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WAZIRI WA MALIASILI PROF.MAGHEMBE AMSIMAMISHA KAZI MAOFISA MISITU NCHI NZIMA”
Post a Comment