Thursday, February 4, 2016
MAHAKAMA YA RUFAA KUAMUA UGOMVI WA NYUMBA YA AFANDE SULEIMAN KOVA NA GODFREY NZOWA
Do you like this story?
Mahakama ya
Rufaa wiki ijayo inaanza kusikiliza kesi za rufani 50 za jinai na madai katika
Kanda ya Arusha ikiwamo rufaa ya makamishna wawili wa Jeshi wa Polisi
wanaogombea nyumba ya serikali iliyopo Uzunguni Arusha.
Maofisa hao,
Godfrey Nzowa ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika
Jeshi hilo amemshitaki mahakamani aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova akipinga kuuziwa nyumba hiyo. Kamishna Kova hata
hivyo amestaafu rasmi mapema mwaka huu.
Kwa mujibu wa
orodha ya kesi zitakazosikilizwa na majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa kwa
mwezi mmoja mjini hapa, Nzowa anamlalamikia Kova na wenzake kupinga kuuziwa
nyumba hiyo aliyokuwa akiishi alipokuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(RCO) wa Mkoa wa Arusha.
Nyumba hiyo
aliuziwa Kamishna Kova akiwa ameshahama mkoani Arusha na wakati inauzwa Nzowa
alikuwa akiishi katika nyumba hiyo, familia yake akiwa RCO kabla ya kuhamishiwa
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea na wadhifa huo, Kova akiwa bosi wake.
Orodha hiyo
yenye jumla ya mashauri 50 inaonesha mahakama hiyo itasikiliza rufani ya Wakili
maarufu jijini Arusha, Median Mwale ambaye amekata rufaa dhidi ya Jamhuri
katika kesi yake ya kudaiwa kutakatisha fedha chafu na kujipatia mabilioni ya
fedha kwa njia ya udanganyifu akiwa na wenzake watatu.
Rufani hiyo
namba 395 ya mwaka 2013 ya Wakili Mwale dhidi ya Jamhuri imepangwa kusikilizwa
na majaji watatu, Mbarouk Salim Mbarouk, Bernard Luanda na Semistocles Kaijage
watakaosikiliza pia mashauri mengine kabla ya kutoa uamuzi Machi 5, mwaka huu.
Orodha
iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, E.Y. Mkwizu inaonesha kesi
nyingine yenye mvuto ni ile ya wafanyabiashara Philemon Mang’ehe na Gesso
Bajuta iliyodumu kwa miaka 20 sasa.
Katika kesi
hiyo, Mang’ehe wa Kampuni ya Bukine anamdai fidia ya mamilioni ya fedha Bajuta
baada ya kudai kuharibiwa biashara yake ya kusambaza vifaa vya ofisi katika
Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) mwaka 1996.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAHAKAMA YA RUFAA KUAMUA UGOMVI WA NYUMBA YA AFANDE SULEIMAN KOVA NA GODFREY NZOWA”
Post a Comment