Wednesday, February 10, 2016
SIMBA KWENDA KILELENI VPL KWA MARA YA KWANZA BAADA YA MIAKA 3?
Do you like this story?
Na Baraka Mbolembole
Kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka
mitatu timu ya Simba SC itakuwa na nafasi ya kuongoza msimamo wa ligi kuu
Tanzania bara, hilo litawezekana endapo mabingwa hao wa zamani watapata ushindi
katika mchezo wa wikendi hii dhidi ya Stand United katika uwanja wa Kambarage,
Shinyanga.
Mara ya mwisho kwa ‘Wekundu wa Msimbazi’ kuongoza
msimamo wa ligi kuu ni mwanzoni mwa msimu wa 2013/14 wakiwa chini ya kocha
Abdallah ‘King’ Kibadeni na Jamhuri Kiwhelo’ ‘Julio’ ambao waliiongoza timu
hiyo kushinda michezo mitano mfululizo ya mwanzo mwa msimu.
MSIMU WA 2014/15
Simba haikuwahi kufika hata nafasi ya pili
katika msimu mzima, lilikuwa jambo jipya kabisa kwa mabingwa hao mara 19 wa
zamani kushindwa kabisa kuongoza msimu walau kwa masaa kadhaa tu. Baada ya taji
lao la mwisho msimu wa 2011/12 itakumbukwa kuwa msimu uliofuata walimaliza katika
nafasi ya 3, wakamaliza nafasi ya nne msimu wa 2013/14, na msimu uliopita
walimaliza nafasi ya tatu.
USHINDI WA MECHI 5 MFULULIZO
Baada ya mwendo wa kusuasua mwanzo mwa msimu
huu chini ya Muingereza, Dylan Kerry timu hiyo imeonekana kuamka chini ya kaimu
kocha mkuu Jackon Mayanja ‘gwiji wa zamani kiuchezaji’ kutoka nchini
Uganda. Chini ya Mganda huyo Simba imefanikiwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka
2010 kushinda michezo 6 mfululizo.
Mayanja alianza na ushindi wa 1-0 dhidi ya
Mtibwa Sugar, kisha akaisimamia timu hiyo kushinda 2-0 mbele ya JKT Ruvu. Kama
hiyo haitoshi wakasafiri kwenda Morogoro na kupata ushindi wa 3-0 dhidi ya
Burkina Faso FC katika michuano ya kombe la FA. Wakashinda 4-0 dhidi ya African
Sports kisha 5-1 dhidi ya JKT Mgambo katika michezo ya ligi kuu.
Jumapili iliyopita walipata ushindi wa 1-0
dhidi ya Kagera Sugar katika uwanja wa Kambarage.
Matokeo hayo mazuri mfululizo yamerejesha ari
katika timu na huku wakiwa nyuma kwa alama moja tu dhidi ya vinara Yanga SC,
nafasi pekee ya wao kushika usukani ni kuwafunga Stand katika mchezo wa
Jumamosi hii kwa kuwa timu za Yanga na Azam FC hazitakuwa na mechi za ligi kuu
wikendi hii kutokana na kukabiliwa na michezo ya vilabu Afrika.
MECHI 3 ZILIZOPITA DHIDI YA STAND UNITED
Stand ni timu mpya kabisa katika mpira wa
miguu Tanzania bara. Huu ni msimu wao wa pili kucheza ligi hiyo ya juu zaidi
nchini baada ya kunusurika kushuka siku ya mwisho ya msimu uliopita baada ya
kuishinda Ruvu Shooting ya Pwani iliyoteremka daraja (Shooting tayari wamerejea
VPL msimu ujao).
Mechi yao ya kwanza katika ligi kuu dhidi ya
Simba ilimalizika kwa sare ya 1-1 katika uwanja Taifa, Dar es Salaam,
wakashinda 1-0 katika uwanja wao wa nyumbani (Kambarage.) Mechi yao ya
kwanza msimu huu ilimalizika kwa Simba kushinda 1-0 katika uwanja wa Taifa.
Mechi yao ya nne haitakuwa rahisi kwa kuwa
kila timu ipo vizuri na timamu kimwili na kiakili. Stand wanashika nafasi ya 5
wakiwa na pointi 29 wakati Simba wataingia uwanjani wakiwa na pointi 42 katika
nafasi ya pili ya msimamo.
Itakuwa mechi kali lakini kitendo cha Simba
kushindwa kupata ushindi kitakuwa kimewanyima nafasi ya kuongoza ligli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SIMBA KWENDA KILELENI VPL KWA MARA YA KWANZA BAADA YA MIAKA 3?”
Post a Comment