Wednesday, February 10, 2016
VYAMA 9 HAVITASHIRIKI UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR.
Do you like this story?
Vyama tisa vya
siasa kati ya 14 vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu Zanzibar mwaka jana vimeungana na
CUF kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, hadi
utakapopatikana mwafaka wa kumaliza mgogoro wa kisiasa.
Mratibu wa
umoja wa vyama hivyo, Kassim Bakari Ali alisema jana kuwa vyama hivyo vilikutana
Unguja na kupitisha maazimio mawili ya kutoshiriki uchaguzi huo.
Vyama hivyo ni
UMD, Jahazi Asilia, Chaumma, UPDP, DP, CCK na ACT Wazalendo. Ushiriki wa vyama
vya ADC na CCK bado una utata kutokana na wagombea wake kutangaza kushiriki
licha ya vyama vyao kuwa na msimamo tofauti, hali iliyosababisha wagombea hao
kusimamishwa.
Vyama ambavyo
vimetangaza kushiriki marudio hayo hadi sasa ni CCM, Tadea, TLP, Sau na AFP.
Kwa kipindi cha
miezi miwili iliyopita, Zanzibar imeendelea kuwa kwenye mgogoro wa kisiasa kati
ya vyama vikubwa vinavyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya CUF
kususia marudio ya uchaguzi baada ya ule wa awali kufutwa na Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Akitaja
maazimio ya vyama hivyo, Kassim alisema wamekubaliana kutoshiriki marudio ya
uchaguzi huo hadi mgogoro wa CCM na CUF utakapomalizika na wameunda kamati ya
wajumbe 18 ya wenyeviti na makatibu wa kila chama ili kuanzisha meza ya
kutafuta suluhu ya mvutano uliopo kati ya CCM na CUF.
“Tutaanza
kukaa na viongozi wa vyama hivyo kila upande kujua ni nini hasa hatima ya
mvutano huo na tunajikwamuaje,”
alisema.
Ali ambaye pia
ni mwenyekiti wa Jahazi Asilia alisema mgogoro wa Zanzibar utamalizwa na
Wazanzibari wenyewe, hivyo ni vyema viongozi hao wa kisiasa wakajenga uvumilivu
katika kutafuta mwafaka.
Alisema tatizo
la vyama hivyo siyo kushiriki marudio ya uchaguzi huo tu bali ni kuangalia
chanzo na hatima ya mgogoro huo kwa masilahi ya Wazanzibari.
Mwenyekiti wa CCK,
Constatine Akitanda aliwaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi wa kusimamishwa
uanachama kwa mgombea wake wa urais, Ali Khatibu Ali, unakwenda sanjari na
kutoshiriki uchaguzi hadi maridhiano ya CUF na CCM yapatikane.
Mgombea urais
wa Zanzibar kupitia AFP, Said Soud Said alisema jana kwamba, chama hicho
kimekubali kurudia uchaguzi huo.
“Lengo
la chama chetu ni kushika dola, sasa tusiposhiriki itakuwaje? Kwanza hatuamini
kama CUF haijatendewa haki kwa sababu ni kweli kulikuwa na udhaifu, mfano
vurugu za kituo cha kupigia kura cha Matrekta Wawi,” alisema.
Mwenyekiti wa
TLP, Augustine Mrema alisema kama vyama hivyo viliiamini ZEC katika uchaguzi
uliopita, vinatakiwa kuiamini kwenye marudio hayo kwa kuwa hakuna mbadala.
“Naomba
wakubali kurudia uchaguzi kwani ‘maji yalishamwagika na kuzoleka haiwezekani...
Nani aliyekwenda mahakamani kupinga? Wanachoogopa kurudia ni kitu gani kama
walishinda?” alihoji Mrema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ VYAMA 9 HAVITASHIRIKI UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR.”
Post a Comment