Thursday, February 11, 2016

WATU 40 MBARONI KWA MAUAJI YA WANANDOA MBEYA.




NA SAMWEL NDONI, KYELA
ZAIDI ya wakazi 40 wa Kata ya Ipinda katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakidaiwa kujichukulia Sheria mkononi kwa kuwaua wazee wawili ambao walikuwa ni mme na mke kwa madai ya kuwa ni washirikina.

Katika siku za hivi karibuni wananchi hao waliwaua wazee hao ambao ni Geneli Kapwela (65) na Rahabu Bungulu (70) kwa kuwakatakata na vitu vyenye ncha kali na kIsha kuwachoma moto kwa madai kuwa wanasambaza kipindupindu kwa njia za kishirikina.

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Dk. Thea Ntara, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hiyo amesema kuwa idadi ya watu waliokamatwa ilikuwa imefikia 47 na kwamba msako bado unaendelea huku akisisitiza kuwa kuna baadhi wamekimbilia milimani.

Amesema kuwa baada ya mauaji ya wazee hao yeye pamoja na kamati nzima ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya walienda katika Kata hiyo na kuitisha mkutano ambapo walifanikiwa kuwakamata viongozi wa kijiji yaani Mwenyekiti na Mtendaji ambao ndio wanaodaiwa kuitisha mkutano ulioazimia kuwaua.

Amesema kuwa baada ya kuwakamata viongozi hao na kuanza safari ya kwenda nao Kyela mjini kwa ajili ya hatua zaidi njiani walikutana na kundi la watu ambao walikuwa wanakimbia ndipo walipowashakia kuwa ni miongoni mwa wahusika wa mauaji hayo na kuwakamata.


Alifafanua kuwa baada ya kuwafikisha watu hao Kyela mjini walianza kufanya uchunguzi ambapo walibaini kuwa kati ya watu 47 waliokuwa wamekamatwa watu Saba ndio waliobainika kuwa walihusika katika mauaji ya vikongwe  hao.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi wa Kyela kuacha kuhusisha ugonjwa wa Kipindupindu na ushirikina, kwa madai kuwa ugonjwa huo unasababishwa na uchafu hivyo akawataka kuendeleza zoezi la usafi wa mazingira.

Amesema kuwa ugonjwa huo unasababishwa na vijidudu vijulikanavyo kwa jina la ‘Fibro Cholerae’ ambavyo vinazalishwa kwenye uchafu wa aina mbalimbali.

Amesema kuwa ili kuhakikisha unyama huo haurudiwi amemwagiza Mkurugenzi wa Wilaya hiyo kuwatawanya maafisa Maendeleo ya Jamii kwenda katika vijiji ili kuwaelimisha wananchi kuwa Kipindupindu hakisababishwi na Uchawi.
Mwisho.

0 Responses to “WATU 40 MBARONI KWA MAUAJI YA WANANDOA MBEYA.”

Post a Comment

More to Read