Saturday, March 12, 2016
MAMENEJA 9 DAWASCO WATUMBULIWA MAJIPU AKIWEMO MKURUGENZI MSTAAFU WA SHIRIKA HILO
Do you like this story?
Mameneja wa DAWASCO wakiwa katika mkutano huo. Baadhi yao walisimamisha kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazo wakabili. |
Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Mhandisi Gerson Lwenge amewasimamisha kazi mameneja tisa wa Shirika la
Majisafi na Majitaka la Dar es Salaam (Dawasco), akiwamo mkurugenzi aliyestaafu
kwa tuhuma za kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh2.8 bilioni.
Awali utumbuaji majipu, ambao unalenga kuondoa ufisadi na uzembe katika utumishi wa umma, ulikuwa ukihusisha watendaji walio kazini, lakini jana Waziri Lwenge alisema aliyehusika kwenye tuhuma hizo za ufisadi wa kitaasisi atachukuliwa hatua hata kama ameshaachia nafasi yake.
Akizungumza katika mkutano wake na
watendaji wakuu wa shirika hilo, Waziri Lwenge alisema kusimamishwa kwa
watumishi hao ni kutokana na kutuhumiwa kushiriki katika njama za kuiunganisha
maji kampuni ya Strabag bila kufuata utaratibu.
Aliwataja watumishi waliosimamishwa
kuwa ni Peter Chacha, Regnald Kessy, Theresia Mlengu, Josper Kilango, Fred
Mapunda, Mvano Mandawa, Emanuel Gulupa, Raymond Kapyela na Jumanne Mapunda.
Waziri Lwenge pia ameagiza aliyekuwa
mkurugenzi wa shirika hilo ambaye alistaafu, Jakson Midala naye achunguzwe
ushiriki wake katika njama hizo kwa kuwa zilifanyika wakati wa uongozi wake.
Sambamba na maagizo hayo, waziri huyo
wa maji ametoa siku 14 kwa Strabag kulipa kiasi hicho cha pesa kilichokwepwa
vinginevyo hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya kampuni hiyo.
Strabag ni kampunii ya ujenzi
inayoshughulikia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mabasi yaendayo Haraka
(BRT).
Waziri alisema kampuni hiyo kwa
kushirikiana na wafanyakazi wasio waaminifu wa shirika hilo la maji
walifanikisha kuunganisha maji bila kupata vibali na kufuata utaratibu.
Alisema baada ya kuunganishiwa maji,
Strabag walianza kuyatumia katika ujenzi wa barabara hizo bila kuyalipia na
kulikosesha shirika mapato yake.
Alisema uunganisho huo ulifanyika
mwaka 2014 kutoka kwenye mabomba yenye vipenyo vikubwa (DN 100 na DN 400).
Alisema ukubwa wa mabomba yaliyotumika
kuunganisha maji ni ushahidi kuwa watumishi wasio waaminifu wa Dawasco
walishiriki katika mpango huo.
Alisema kutokana na matumizi hayo ya
maji yasiyolipiwa, Serikali imekosa mapato ya shilingi 2.887,577,134.
Waziri pia aliagiza bodi ya Dawasco
kusimamia menejimenti ya shirika hilo na kusaidia kumaliza tatizo la upoteaji
wa maji linalosababishwa na kupasuka kwa mabomba pamoja na wizi.
Pia aliagiza bodi isaidie kutatua
kero za wananchi, hususan kusambaza maji kwa wananchi wasiopata huduma hiyo,
usomaji mbaya wa mita za maji unaosababisha wananchi kulipia ankara kubwa
zisizolingana na matumizi halisi.
“Naiagiza bodi vilevile iweke
mipango endelevu itakayohakikisha asilimia ya wananchi wanaopata huduma ya
majisafi inafika 95 ifikapo mwaka 2020,”
alisema.
Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi
Cyprian Luhemeja alisema changamoto kubwa inayolikabili shirika hilo ni upotevu
wa maji ambao mbali na wezi, pia unasababishwa na uchakavu wa mitambo ambayo
mingi ni ya miaka 1970.
Naye mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Dawasco, Meja Jenerali Samwel Kitundu alimuomba waziri
kulisaidia shirika hilo kuweza kukusanya madeni yake inayozidai taasisi za
Serikali ambazo bila kuzitaja alisema zinadaiwa madeni makubwa.
Pia, Kitundu aliitaka serikali iweke
sheria kali dhidi ya wezi wa maji ili waweze kuwabana wanaokamatwa kuhusika na
vitendo hivyo vinavyochangia kulikosesha shirika hilo mapato yake.
Akizungumzua tuhuma hizo, ofisa
uhusiano wa Strabag, Yahaya Mkumba alisema si kweli kuwa hawakufuata taratibu
zote zinazotakiwa ili waunganishiwe maji, ingawa alisema maji hayo yalikuwa
hayatoshelezi mradi na kuwalazimu kununua ili kukidhi mahitaji yao.
Alikiri kuwapo kutokuelewana kwa
kampuni yake na shirika hilo katika gharama za maji wanazopelekewa lakini
akasema suala hilo walilimaliza kisheria.
“Wamekuwa wakituletea bili
zisizoeleweka, hata hivyo tuliamua kulishughulikia suala hili kisheria,” alisema Mkumba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MAMENEJA 9 DAWASCO WATUMBULIWA MAJIPU AKIWEMO MKURUGENZI MSTAAFU WA SHIRIKA HILO”
Post a Comment