Monday, March 7, 2016
OFISI 5 ZA CUF ZACHOMWA MOTO ZANZIBAR.
Do you like this story?
HALI ya kisiasa
visiwani Zanzibar, inazidi kuwa tete huku siasa za visasi, chuki na uhasama
zikionekana kurejea kwa kasi.
Hali hiyo
imejitokeza baada ya ofisi za matawi matano ya Chama cha Wananchi (CUF)
zilizopo Pemba na moja Unguja kuchomwa moto na watu wasiojulikana.
Matukio ya
kuchomwa moto kwa ofisi hizo yamekuja siku mbili baada ya watu wasiojulikana
kuchoma moto maskani ya CCM ya Sauti ya Kisonge iliyopo mjini Unguja.
Hata hivyo
Jeshi la Polisi visiwani humo limetangaza kufanya uchunguzi wa kina ili
kuwabaini watu waliohusika na matukio hayo.
Uchomaji huo
ulifanyika usiku wa kuamkia jana saa 8 usiku, ambapo watu hao walichoma moto na
kuteketeza nyaraka za chama hicho.
Matawi
yaliyochomwa moto ni Kilimahewa mjini Unguja Wilaya ya Magharibi, Mkanyageni,
Kiwapwa, Kiuyu Minungwini, Wingwi na Kinowe yote ya Kisiwani Pemba.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, amethibitisha kutokeo kwa
matukio hayo.
Amesema
kutokana na hali hiyo tayari ameagiza askari wake kuanza uchunguzi wa tukio
hilo haraka ili waliohusika watiwe nguvuni na kufikishwa katika vyombo vya
sheria.
“Ni
kweli kuna hilo tukio ingawa kwa sasa nipo safari kuelekea Unguja na tayari
nimeagiza kuanza kwa uchunguzi wa matukio haya ili wahusika waweze kukamatwa na
kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“…siwezi
kusema kama matukio haya yana uhusiano wa masuala ya kisiasa ingawa huu ni
uhalifu kama uhalifu mwingine,”
alisema Kamanda Nassir.
Akizungumzia
tukio hilo, Mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamad (CUF), alilaani tukio hilo huku
akiwatuhumu wafuasi wa CCM kuhusika nalo.
Alisema hatua
ya CUF kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20,
mwaka huu imekuwa ikiwaumiza CCM.
“Haya
mambo yapo wazi tumeumizwa vya kutosha lakini katika hilo mimi binafsi wala
sifichi hapa kuna mkono wa CCM na sisi hatutarudi nyuma tunaendelea na
msimamo wa chama,” alisema Hamad.
Kauli ya Maalim
Seif
Machi 4, mwaka
huu, Akizungumza na wafuasi wake waliomtembelea nyumbani kwake, Katibu Mkuu wa
CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema yuko tayari kukamatwa kutokana na
msimamo wake wa kutotambua uchaguzi wa marudio.
“Msidhani
kuwa mtatupiga shavu la kulia tukawageuzia la kushoto. Kila mara tunaibiwa,
tunapigwa, tunafanywa kila kitu. Tukisema kuwa watu wajilinde, inakuwa nongwa.
“…basi
tunawaambia kuwa kuitwa polisi, kuwekwa ndani, kufunguliwa mashtaka ya bandia,
hata kuteswa, hayo ni mambo yamekuwa yakitutokea tangu 1992 tumeshayazoea,” alisema Maalim Seif.
Alisema
udhalilishwaji kama huo haujawahi kukirudisha nyuma chama chake, zaidi ya
kukiongezea umashuhuri na ufuasi mkubwa visiwani Zanzibar, huku akilituhumu
Jeshi la Polisi kwa kuwa ‘tawi la CCM’ ambalo litakuwa dhamana wa machafuko
yoyote yatakayotokea.
Katika hatua
nyengine, Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi wa Oktoba
25, mwaka jana alirudia msimamo wa chama chake wa kutoshiriki kile
alichodai uchaguzi wa marudio ulioitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
(ZEC), Jecha Salim Jecha, Machi 20, mwaka huu.
Alisema yeye
alishashiriki uchaguzi na kushinda na hahusiki kabisa na uchaguzi mwengine. “Ninamwambia
Jecha kuwa uchaguzi huo ni wenu peke yenu,” alisema Maalim Seif.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ OFISI 5 ZA CUF ZACHOMWA MOTO ZANZIBAR.”
Post a Comment