Tuesday, March 8, 2016
PROF. MBARAWA AITAKA SUMATRA KUJIPANGA UPYA.DAR
Do you like this story?
Watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa(hayupo pichani), wakati alipokutana nao. |
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka
Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), kudhibiti wasafirishaji
wasio waaminifu, wanaobadilisha ruti za safari na kuongeza nauli nyakati za
asubuhi na jioni nchini.
Akizungumza na wafanyakazi wa SUMATRA amewataka kutengeneza mkakati
utakaoboresha huduma za usafiri na kupunguza ajali za barabarani nchini
kote.
“Sumatra mna mchango mkubwa wa kusimamia sekta ya usafirishaji nchini,
hatutaki kuona nauli zinabadilika nyakati za asubuhi na jioni na kusababisha
usumbufu kwa abiria,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amewataka SUMATRA kutosita kuchukua sheria kwa yeyote anayekiuka taratibu
za usafiri, kujenga mazingira sawia ya ushindani, kusimamia gharama na viwango
vya huduma na kutoa leseni kwa wasafirishaji kwa haraka.
Waziri Prof. Mbarawa ameipongeza Mamlaka kwa jitihada wanazozifanya za
kuweka mifumo ya utendaji wa kieletroniki itakayo ratibu mabasi yawapo safarini
ili kupunguza mwendo kasi na kupunguza ajali.
Aidha Waziri Mbarawa ameitaka SUMATRA kukusanya mapato yanayostahili
kikamilifu na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Kwa upande mwingine Waziri Mbarawa ameitaka Mamlaka hiyo kusimamia mfumo
uliopo wa kieletroniki kwa ajili ya kupata leseni kwa muda usiozidi miezi
miwili.
Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA Bw. Giliard Ngewe amemhakikishia Waziri
Mbarawa kuwa Mamlaka inaendelea kutoa elimu kwa madereva kwa kushirikiana na
Jeshi la Polisi ili kupunguza ajali za barabarani na kuboresha huduma za
usafiri nchini.
“Tumejipanga kuhakikisha maeneo yenye upungufu wa mabasi ya abiria
yanapatiwa ruti mpya ili kupunguza changamoto katika maeneo ambayo yana
changamoto ya usafiri”, amefafanua Waziri Mbarawa
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa ameitaka SUMATRA kuangalia namna ya
kutenganisha udhibiti wa usafiri wa majini na Nchi kavu ili kuongeza tija na
kukuza sekta hizo hapa nchini.
“Kukiwa na udhibiti wa usafiri wa majini (Maritime Authority) kutasaidia
kukuza sekta hiyo na Sumatra kuendelea kudhibiti usafiri wa nchi kavu (reli na
barabara)”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa alikuwa katika ziara ya kikazi ya kutoa miongozo na
muelekeo wa serikali ya Awamu ya Tano ambapo amesisitiza uadilifu, uwazi, na
utendaji kazi wenye malengo yanayopimika,
Katika mikakati ya kudhibiti usafiri wa nchi kavu SUMATRA imepanga
kuunganisha mikoa yote 25 ya Tanzania Bara kwenye mfumo wa kompyuta ili kutoa
leseni kwa haraka na kuongeza mapato ambapo takribani shilingi bilioni 45
zinatarajiwa kukusanywa katika mwaka huu wa fedha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “PROF. MBARAWA AITAKA SUMATRA KUJIPANGA UPYA.DAR”
Post a Comment