Friday, March 4, 2016
WAKUU WA MIKOA WAPEWA JUKUMU LA KUTOA VIBALI VYA KUCHANGIA ELIMU
Do you like this story?
Serikali imeongeza wigo wa utoaji wa
kibali cha uchangiaji wa elimu msingi bila malipo hadi kwa Wakuu wa Mikoa baada
ya kujiridhisha kuwa taratibu zilizowekwa zimefuatwa kikamilifu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari iliyotolewa jijini Dar es salaam Msemaji wa Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Rebecca Kwandu amesema kuwa awali vibali
hivyo vilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) pekee ikiwa na lengo la kudhibiti michango holela.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa azma ya
Serikali ya kutoa elimumsingi bila malipo haizuii wadau mbalimbali wa elimu
kuchangia maendeleo ya elimu kwa hiari ambapo wadau wakiamua kuchangia kwa nia
ya kushughulikia kero fulani iliyopo katika shule yao au shule zao baada ya
kupata kibali wanaruhusiwa kufanya hivyo.
Katika kutekeleza dhana ya utoaji wa
elimumsingi bila malipo, hadi kufika mwishoni mwa mwezi Januari,
2016 Serikali inatoa elimu hiyo kwa jumla ya wanafunzi 9,771,902.
Kati ya wanafunzi hao, 8,301,759 ni wa
elimu ya msingi na 1,470,143 ni wa sekondari ambao wanapatiwa elimumsingi bila
malipo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Serikali inasisistiza kuwa viongozi
wanahusika katika kusimamia utekelezaji wake ambapo kwa upande wa wazazi au
walezi, kamati na Bodi ya shule pamoja na jamii wao nao wanajukumu la kuelewa
majukumu yao ipasavyo.
Aidha, juhudi za makusudi zinapaswa
kufanywa na viongozi na watendaji wa elimu ili kuwezesha jamii kufahamu wajibu
wao katika utekelezaji wa elimumsingi bila malipo na hatimaye kufikiwa kwa
malengo yaliyokusudiwa.
Katika kutekeleza wajibu wake, Serikali
ya Awamu ya Tano (SAT) kuanzia mwezi Januari, mwaka huu imeanza kutoa
elimumsingi bila malipo imetoa waraka wa Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 ambao
unaofafanua na kubainisha majukumu ya serikali na wadau mbalimbali katika
utekelezaji wa elimu msingi bila malipo.
Imeandaliwa na Eleuteri Mangi- MAELEZO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WAKUU WA MIKOA WAPEWA JUKUMU LA KUTOA VIBALI VYA KUCHANGIA ELIMU”
Post a Comment