Tuesday, March 8, 2016
WAZIRI WA ARDHI, WILLIAM LUKUVI AKATAA RUSHWA YA BILIONI 5.
Do you like this story?
Waziri wa
Ardhi, William Lukuvi amesema rushwa imekithiri kwenye sekta ya ardhi kiasi
kwamba wafanyabiashara wawili walimuahidi rushwa ya Sh5 bilioni afanikishe
mpango wao wa kuiuzia Serikali ardhi kwenye eneo linalotakiwa kujengwa mji wa
kisasa wa Kigamboni.
Mji huo kabambe
wa Kigamboni unajumuisha kata za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada,
Somangila na eneo lote lina ukubwa wa takribani ekari 6,000.
Awali mradi huo
ulitarajiwa kugharimu Sh13 trilioni ambazo zingetolewa na Serikali, lakini
ikaamua kushirikisha sekta binafsi ili zishiriki kuujenga na Serikali
ishughulikie uwezeshaji wa awali.
Lukuvi, ambaye
alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa takriban miaka mitano kabla ya
kuhamishiwa Wizara ya Ardhi mapema mwaka jana na kubakizwa wizara hiyo na Rais
John Magufuli, alitoa siri hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mbunge huyo wa
miaka mingi wa Isimani mkoani Iringa alisema amegundua kuna mtandao mkubwa wa
rushwa unaoanzia ngazi ya halmashauri mpaka wizarani ambao unahusisha maofisa
wa Serikali na viongozi wa wizara.
Waziri Lukuvi
alisema mtandao huo ni hatari na unaweza kusababisha mtu ashindwe kufanya kazi
ya wananchi iwapo ataendekeza rushwa.
“Hapa
(Wizara ya Ardhi) fedha ipo,”
alisema Lukuvi ambaye amekuwa mbunge wa Isimani tangu mwaka 1995.
“Kama
ukiwa na tamaa huwezi fanya kazi uliyotumwa. Kuna wakati walikuja
wafanyabiashara wawili wakubwa na kutaka wanipe Sh5 bilioni ili nikubali
kupitisha mradi wao wa mabilioni ya shilingi na walitangaza kwa marafiki zangu
kuwa wangenipa fedha, lakini hapa hawawezi” alisema
Lukuvi.
“Wakati
naingia tu wizara hii, nilikuta harakati za kukamilisha mradi wa Kigamboni
ukiwa katika hatua za mwisho na kila kitu kilikuwa kimekamilika. Lakini
nilipopitia vizuri, nilikataa kuwalipa wafanyabiashara hao. Cha ajabu
hazikupita siku mbili wafanyabiashara hao walipata taarifa wakaja mbio kutaka
kuniona.”
Kwa mujibu wa
Waziri Lukuvi, wafanyabiashara hao walitaka walipwe kiasi cha Sh141 milioni kwa
kila ekari wakati wao walinunua ardhi kutoka kwa wananchi kwa Sh5 milioni kwa
ekari, jambo ambalo alisema lilishapitishwa awali.
“Niligundua
pale kuna udanganyifu na wizi mkubwa. Haiwezekani mwekezaji anunue kutoka kwa
wananchi ekari moja kwa Sh5 milioni, kisha Serikali tumlipe Sh141 milioni kwa
ekari kwa kuvuka pantoni tu. Ni wizi mkubwa. Kama kweli Serikali ina fedha hizo
kwa nini tusimlipe mwananchi moja kwa moja?”
alihoji.
Waziri Lukuvi
alisema endapo njama hizo zingefanikiwa, Serikali ingetumia zaidi ya Sh84
bilioni kuwalipa wawekezaji hao hewa kwa kuwa mmoja anamiliki takribani ekari
200 na mwingine 400.
“Niliwaambia
Serikali haiwezi kuwalipa fedha hizo na badala yake waende kuiendeleza ardhi
wenyewe kulingana na mradi unavyotaka. Walitaka kutajirika kwa ujanja ujanja,” alisema Lukuvi.
“Eti
walidai wamekopa benki kwa ajili ya mradi huo. Haiingii akilini mtu utumie Sh5
milioni, halafu uje uvune mabilioni ya fedha kwa kuvuka pantoni tu.”
Hata hivyo,
Lukuvi alikataa kutaja majina ya wafanyabiashara hao.
Akiongea na
gazeti moja la kila wiki mwaka 2013, Profesa Anna Tibaijuka, waziri
aliyemtangulia Lukuvi kwenye wizara hiyo, alisema tayari kampuni mbili za
Miworld kutoka Dubai na China Hope (China) zilishasaini mkataba wa maridhiano
na Serikali wa kujenga nyumba takriban 20,900 kwenye eneo hilo.
Miworld
ilisaini mkataba wa kujenga nyumba 5,000 wakati China Hope ilitaka kujenga
nyumba 15,900 kwenye eneo hilo la mradi wa mji mpya.
Profesa
Tibaijuka aliliambia gazeti hilo wakati huo kuwa wananchi wangefidiwa kwa bei za soko kwa mujibu wa sheria, akisema
ekari moja ingefidiwa Sh141 milioni kwa ajili ya kumuwezesha kulipia
gharama ya nyumba mpya mbadala.
Akizungumzia
migogoro ya ardhi, Waziri Lukuvi alisema amegundua mingi inasababishwa na
maofisa na viongozi wa wizara hiyo wasio waaminifu, lakini pia wawekezaji wenye
tamaa ya kumiliki kiasi kikubwa cha ardhi hata kama hawana shughuli nayo.
“Nimegundua
kuna watu hapa wanataka kumiliki ardhi kila sehemu. (Mtu huyo) Atafanya kila
njia ashirikiane na watumishi wasio waaminifu ili wampatie eneo hata kama
limeshauzwa,” aliongeza.
Lukuvi alisema
wengi wao ni wafanyabiashara wenye asili ya Kiarabu na Asia ambao kwa muda
aliokaa wizarani hapo amegundua wamehodhi mashamba katika miradi yote ya
viwanja au mashamba iwe ya halmashauri au wizara.
“Wanasiasa
na viongozi wa Serikali wanaohodhi maeneo wapo, lakini siyo wengi ukilinganisha
na hawa wafanyabiashara wengi wenye tamaa ambao wakishapata ardhi wanatumia
kukopa mabilioni ya fedha ndani na nje ya nchi kisha wanawekeza katika miradi
yao mingine ikiwamo kujenga majumba katika nchi za Dubai na Ulaya na
kuyatelekeza maeneo hayo kuwa mapori hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa
wananchi wasio na maeneo."
Akizungumzia
matarajio yake, Waziri Lukuvi alisema endapo Rais John Magufuli ataendelea
kumuweka katika wizara hiyo anatamani amalize migogoro yote baina ya wananchi
katika kipindi cha miaka mitano
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WAZIRI WA ARDHI, WILLIAM LUKUVI AKATAA RUSHWA YA BILIONI 5.”
Post a Comment