Thursday, April 21, 2016
MKUU WA MKOA WA MBEYA AMOSI MAKALLA AONJA MOTO WA UKAWA...MADIWANI 34 WAKIONGOZWA NA MEYA WAO WASUSIA KIKAO CHAKE CHA KUJITAMBULISHA.
Do you like this story?
Meya wa Jiji la Mbeya Mh Mch David Mwashilindi akiwa na madiwani wakitoka nje.(Picha na David Nyembe wa Fahari News) |
Madiwani Wakitoka ndani ya ukumbi (Picha na David Nyembe wa Fahari News) |
Baadhi ya madiwani wa Chadema wakiondoka.(Picha na David Nyembe wa Fahari News) |
Meya wa Jiji la Mbeya Mh Mch David Mwashilindi akiondoka mara Baada ya kususia Kiakao cha Mkuu wa Mkoa.(Picha na David Nyembe wa Fahari News) |
Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amekumbana na joto la Mbeya baada ya meya wa jiji
hilo, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani wake 34 kususia kikao chake cha
kujitambulisha kwa wananchi, baada ya kudaiwa kwenda kukagua Soko la Mwanjelwa
bila kumpa taarifa yoyote meya wa jiji hilo.
Meya
alifikia uamuzi huo ndani ya ukumbi wa Mkapa muda mfupi kabla ya Makalla kuanza
kuzungumza na watumishi wa jiji, wananchi, wazee maarufu, viongozi wa dini na
machifu ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Nyirembe Sabi alimkaribisha Meya
Mwashilindi kuzungumza chochote kwa niaba ya madiwani wake.
Hata
hivyo, Meya Mwashilindi alipochukua kipaza sauti alisema: “Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, nakumbuka kwa mara ya kwanza kukutana na wewe tulizungumza kwamba
tufanye kazi, siasa zimekwisha. Lakini masikitiko yangu ni kwamba leo hii
umekwenda Soko la Mwanjelwa bila ya mimi mwenye jiji kupewa taarifa yoyote wala
madiwani wangu. Sasa hiki kikao hakinihusu hivyo muendelee na kikao chenu.”
Baada ya
kusema maneno hayo alikabidhi kipaza sauti kwa mkuu wa wilaya, kisha akachukua
nyaraka zake akainuka pamoja na madiwani wote kupitia Chadema na kutoka
ukumbini huku wakisikika wakisema, ‘hizi ni siasa ambazo tulizikataa, lakini
wanatulazimisha kuendesha siasa. Hatuwezi kupuuzwa kwa kiasi hiki.”
Mkuu wa
Wilaya, Mnasa alisema anaamini taratibu na ratiba yote ilipangwa vizuri hivyo
hawaoni sababu ya madai ya madiwani hao kwamba hawakushirikishwa kwenye ziara
hiyo, wao kama wawakilishi wa Rais hawaangalii siasa, bali wanaangalia
uchapakazi na siyo masuala ya siasa.
Akizungumzia
kitendo cha meya na madiwani wake kususia kikao hicho, Makalla alisema ‘Nashangazwa
na uamuzi wa madiwani hawa kwa kitendo hiki, kwani siku ile nilipotembelea
Shule ya Sekondari Iyunga, nilisema kwamba Aprili 20 ambayo ndiyo leo (jana)
nitakuwa na ziara ya jiji na kabla ya kikao nitataka kutembelea Soko la
Mwanjelwa,” alisema Makalla.
Alisema
suala la meya na madiwani wake kutoshirikishwa kwenye ziara ya kwenda Soko la
Mwanjelwa halimhusu, kwani mwenye wajibu wa kupeana taarifa ni kwenye ngazi ya
halmashauri ya jiji, lakini siyo yeye (Makalla).
“Jamani
mimi sijaja kufanya siasa nimekuja kufanya kazi ya wananchi na
nilishatahadharisha jambo hili, sasa kwa kitendo hiki ndiyo siasa na
wananilazimisha kufanya siasa, lakini wao ndiyo watahukumiwa na wananchi. Na
ninasema kama Mola ataendelea kunilinda kubaki katika mkoa mwaka 2020
nitakwenda kuwaambia hiki kinachofanyika sasa na wawakilishi wao,” alisema Makalla.
Awali
Makalla akiwa katika Soko la Mwanjelwa alinusa harufu ya ufisadi kwenye soko
hilo na kuagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoa huo, kufanya uchunguzi ndani
ya wiki nne wa uhalali wa fedha kiasi cha Sh22.9 bilioni iliyotumika katika
ujenzi huo ukiwa ni mkopo kutoka Benki ya CRDB.
Makalla
alitoa agizo hilo jana mchana baada ya kutembelea soko hilo na kuzungumza na
wafanyabiashara wa jijini hapa, ambao walimueleza wanashindwa kumudu gharama ya
upangaji ya vyumba vya biashara ambayo inaanzia kiasi cha Sh500,000 kwa chumba
kimoja kwa mwezi, ndiyo maana hawataki kuingia ndani ya soko hilo.
Mwenyekiti
wa soko hilo, Peter Chacha alimueleza Makalla kwamba wasipokuwa makini soko
hilo litabaki gofu, kwani wafanyabiashara hawataki kuingia kwa kuogopa gharama
kubwa ya vyumba hivyo, alimuomba afanye awezalo kukaa chini na uongozi wa benki
ambao unadai fedha zao kwa jiji na kuona namna ya kupunguziwa gharama hiyo.
“Ni
kweli wenzetu jiji, wametingwa na deni la mkopo kutoka Benki ya CRDB, ndiyo
maana wamekuja kutubana sisi wafanyabiashara kwa kutupangia chumba kuanzia
Sh500, 000 hadi Sh 800,000, kitu ambacho hatuwezi kumudu hata kidogo,”alisema Chacha
Baada ya
kusikiliza kilio cha wafanyabiashara hao, Makalla alisema kiasi cha Sh22.9
bilioni iliyotumika kwenye ujenzi wa soko hilo haiendani na thamani yake, hivyo
vyombo vya dola vikiongozwa na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, wanafanya uchunguzi wa kina na kuwanasaka wale
wote waliohusika kwenye mchakato mzima wa ujenzi wa soko hilo.
“Nataka
kupata taarifa ya mchanganuo mzima wa namna ya fedha ilivyokopwa, ilivyotumika
na mkataba wake ulivyokuwa ndani ya wiki nne, taarifa hii niipokee na wale
watakaobainisha kufuja fedha watapelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
"Kwenye
hili, kuna watu waliotufikisha hapa, Sh22.9 bilioni iliyotumika kwenye ujenzi
huu haiendani na ujenzi wa soko hili, kuanzia muda uliotumika na gharama ya
kodi ya upangishaji wa vyumba siyo rafiki ni kubwa mno, hivyo jiji na CRDB mkae
muone namna ya kupunguza gharama hiyo, kwani hali ilivyo sasa lile soko
litabaki gofu."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MKUU WA MKOA WA MBEYA AMOSI MAKALLA AONJA MOTO WA UKAWA...MADIWANI 34 WAKIONGOZWA NA MEYA WAO WASUSIA KIKAO CHAKE CHA KUJITAMBULISHA.”
Post a Comment