Thursday, May 5, 2016
KIKWETE "AGOMA" KUKAMKABIDHI RAIS MAGUFULI CHAMA ........MWINYI,MKAPA,MALECELA KUKUTANAKWA DHARURA KUMJADILI
Do you like this story?
Hali si
shwari ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na mchakato unaoendelea wa
kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli uenyekiti wa chama hicho, kukumbwa na
sintofahamu.
Taarifa
kutoka ndani kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC), kilichofanyika
juzi Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, zimethibitisha kutokea mgawanyiko wa
vigogo ndani ya chama hicho.
Hali hiyo
imekuja baada ya kutokea kwa mvutano juu ya tarehe rasmi ya kufanyika kwa
mkutano mkuu maalumu uliopangwa Juni mwaka huu, ambao pamoja na mambo mengine
Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete atakabidhi kijiti
kwa Rais Magufuli.
Chanzo cha
kuaminika ndani ya kikao hicho kilidokeza kuwa, kabla kilifanyika kikao
kidogo kilichokuwa na wajumbe wanne ambao pamoja na mambo mengine walijadili
ajenda muhimu ikiwamo ya kupanga tarehe kwa ajili ya mkutano huo.
Kwa mujibu
wa chanzo hicho, kikao hicho kidogo kilishirikisha viongozi wanne akiwemo
Mwenyekiti wa chama hicho Jakaya Kikwete, Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Habari
hizo zinaeleza kuwa, katika kikao hicho kidogo viongozi hao walikubaliana
wakatangaze tarehe rasmi, na Rais Magufuli alikubali kukabidhiwa uenyekiti
wa chama kama ulivyo utaratibu wa CCM lakini baada ya kikao cha
Kamati Kuu kuanza, Kikwete alikataa kuruhusu
hoja hiyo ijadiliwe, hatua iliyozua mfarakano.
“Baada
ya kumalizika kwa kikao kile viongozi hao wanne waliingia ndani ya kikao cha CC
ambacho kilikuwa na ajenda kadhaa ikiwemo ya mkutano mkuu maalumu ambapo
mwenyekiti alirusha na kutaka hoja ya tarehe isijadiliwe,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu
wa chanzo hicho, ilipofika ajenda ya tatu ambayo iliwasilishwa na Katibu Mkuu,
Kinana kuhusu kutangazwa kwa tarehe ya mkutano mkuu maalumu, Kikwete aligoma isijadiliwe na badala yake
aliahirisha kikao na kutoka nje.
Chanzo
hicho kilisema, uamuzi wa Mwenyekiti Kikwete wa kuahirisha kikao ulijikita
katika suala la gharama za mkutano ambazo zinakadiriwa kuwa ni zaidi ya Sh bilioni
mbili, hivyo aliwataka wajumbe waahirishe kikao ili kutoa fursa ya kutafuta
fedha.
Taarifa
hizo zilieleza kuwa, kutokana na hali hiyo yaliibuka makundi mawili, moja
linalomuunga mkono Kikwete na jingine linalopingana na hoja hiyo, likidai kuwa
fedha si tatizo kwa chama hicho kwa kwani kina miradi, ruzuku na marafiki
wengi.
“Wanaompinga
mwenyekiti walishangazwa na hoja hiyo wakisema kuwa, suala la fedha ni la
watendaji wa chama na si la mwenyekiti, kitendo ambacho wamekitafsiri kwamba
mwenyekiti hana dhamira ya dhati ya kukabidhi chama kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo
hicho kiliendelea kutoa taarifa kuwa, baada ya Kikwete kugoma kujadili tarehe
alisimama mjumbe Jenista Mhagama, ambaye alipinga uamuzi huo, huku akisema
suala hilo ni lazima lijadiliwe kwa kina na tarehe ya mkutano mkuu itangazwe.
“Kauli
ya mwenyekiti inaonekana iliwaudhi baadhi ya wajumbe, lakini Jenista
alizungumza vizuri sana na kumhoji mwenyekiti inakuaje hataki kusema lini
utafanyika mkutano mkuu maalumu ili akabidhi chama.
“Maana
suala la makabidhiano ni la utamaduni wa ndani ya CCM, Jenista alisema aliyekaa
muda mrefu alikuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pekee lakini na yeye
alikabidhi kwa mzee Mwinyi (Ali Hassan) na pia ilipofika wakati kama huu mzee
Mwinyi naye alikabidhi kwa mzee Mkapa.
“Si
hilo tu hata mzee Mkapa naye alikabidhi chama kwake (Jakaya Kikwete), sasa
inakuwaje yeye leo hataki kufuata utaratibu huo ambao ni wa kawaida ndani ya
chama?,” kilihoji chanzo hicho.
Chanzo
kingine cha habari kilisema kuwa baada ya
mwenyekiti huyo wa CCM taifa kuahirisha kikao hicho juzi, aliondoka na kurejea
jijini Dar es Salaam kwa gari tofauti na ratiba iliyokuwa imepangwa.
“Ratiba
ya chama ilikuwa baada ya kikao cha jana (juzi) mwenyekiti angelala Dodoma na
badala yake alipoahirisha kikao kwa utata alipanda kwenye gari na kuondoa hali
ya kuwa alitakiwa kurejea Dar leo (jana).
“Baada
ya kikao hicho alitoka mzee Kinana akiwa amekasirika sana, tena huku akiwa
amekunja sura, unajua siku zote mzee Kinana anaamini kwamba kile kilichokuwa
kinapiganiwa na chama hivi sasa ndicho kinachotekelezwa na Rais Magufuli tena
kwa vitendo tofauti na huko nyuma,”
kilisema chanzo chetu.
Baraza
la Wazee kukutana
Taarifa nyingine
zinaarifu kwamba, kutokana na hali hiyo Baraza la Wazee la CCM
linaloundwa na viongozi wastaafu, linatarajiwa kukutana kati ya leo na kesho
kwa lengo la kujadili hali hiyo ili kuondoa mtanziko huo uliojitokeza.
“Ninachotaka
kukuambia katika kipindi cha siku mbili baraza la ushauri la wazee litakutana
na kujadili hali hii na baada ya hapo watakwenda kwa mwenyekiti kumshauri juu
ya uamuzi wake na autafakari kwa kina.
“Tunajua
tunakwenda vizuri katika hili na hakuna kitakachoharibika na wazee wetu
watamshauri vema mwenyekiti ili kupata mwafaka wa kudumu na mkutano mkuu
utafanyika mwezi uliopangwa,”
chanzo hicho kilisema.
Baraza la
Ushauri la Wazee wa CCM, linaongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali
Hassan Mwinyi (Mwenyekiti), Pius Msekwa (Katibu) na wajumbe ni Rais mstaafu
Benjamin Mkapa pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu (Bara), John
Malecela.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KIKWETE "AGOMA" KUKAMKABIDHI RAIS MAGUFULI CHAMA ........MWINYI,MKAPA,MALECELA KUKUTANAKWA DHARURA KUMJADILI”
Post a Comment