Sunday, August 21, 2016
CHADEMA WATANGAZA SAFU YA MAANDAMANO YA UKUTA....LOWASSA APANGIWA MBEYA, KATIBU MKUU MWANZA
Do you like this story?
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe jana alitangaza mkakati wa chama hicho kufanikisha
mikutano na maandamano ya walichokiita Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania
(Ukuta), huku jeshi la polisi nao wakijiandaa kukabiliana nao.
Mbowe
aliitaja mikakati hiyo ikiwamo kamati za kuhamasisha Ukuta ambapo aliyekuwa
mgombea urais kupitia Ukawa Edward Lowassa amepangiwa Mbeya, Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Vincent Mashinji atakuwa Mwanza, Makamu Mwenyekiti Profesa Abdallah
Safari atakuwa Tabora huku Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Halima Mdee na Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema Mabere Marando wakipangiwa Dar es Salaam.
Alisema
yeye (Mbowe) ataongoza Kanda ya Kaskazini wakati Profesa Mwesiga Baregu amepewa
jukumu la kufafanua Ukuta kwa taasisi za kimataifa, viongozi wa dini na
wastaafu.
Mwanasheria
Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu na mawakili 12 wao watajifungia Dar es Salaam
kufungua kesi 21 kutetea mikutano.
Lakini,
Jeshi la Polisi limesema litatoa taarifa rasmi baadaye huku CCM wakisisitiza msimamo
wao wa kupinga maandamano hayo.
Msemaji
wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema jeshi hilo litatoa taarifa
siku chache zijazo. “Tutawaita na tutazungumza, naomba tujaribu tu kuvuta
subira,”alijibu kwa ufupi msemaji huyo wa polisi.
Hata
hivyo kikosi cha Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika mikoa
mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam na Kilimanjaro walionekana wakifanya mazoezi
wakiwa na silaha na magari ya maji ya kuwasha kwa siku tofauti.
CCM
watoa ushauri
Msemaji
wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema licha ya chama kuzungumza mara kadhaa,
wanatarajia kutoa tamko kwa lengo la kuwaeleza Watanzania tahadhari juu ya
mchezo unaojaribiwa na Chadema.
Sendeka
alisema viongozi wa dini na makundi mbalimbali yameshauri juu ya mipango yao,
lakini hawataki kusikia.
“Jambo
hilo limezungumzwa mara nyingi sana, viongozi wa dini wameshasema, watu wenye
mapenzi na nchi yao wakishauri waache huo mchezo wao ambao sidhani kama
watafanikiwa, kwa hivyo tunatarajia kutoa tamko letu siku yoyote kuanzia kesho
(leo),”alisema.
Mbowe
na safu yake
Akizungumza
wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini jana katika
Hoteli ya Coridol Springs jijini hapa, Mbowe alisema chama hicho kimejipanga
kufanya mikutano na maandamano ya amani nchi nzima Septemba Mosi ili kutetea
utawala wa sheria na Katiba.
Mbowe
alisema Rais Magufuli aliapa kuilinda Katiba, Wabunge waliapa kuilinda Katiba,
madiwani waliapa kuilinda Katiba ili nchi iongozwe katika misingi ya sheria na
utawala bora.
Alisema
haiwezekani nchi kuongozwa kwa matamko ambayo yanakiuka katiba na Chadema kama
chama kikuu cha upinzani kina wajibu wa kuishauri na kuikosoa serikali na
hawawezi kukaa kimya.
Alisema
matamko ya Rais kuwa hakuna ruhusa ya kufanya mikutano ya kisiasa kwa vyama
vingine na kuacha chama chake kufanya mikutano na pia kuzuia mikutano hadi
mwaka 2020 haikubaliki.
“Sisi
tunataka nchi iongozwe kwa kufuata sheria na siyo matakwa ya viongozi ambayo
yanakinzana na sheria na Katiba ya nchi,” alisema Mbowe.
Alisema
wanafanya mikutano na maandamano kama sehemu ya kueleza malalamiko yao, hasa
kutokana na kauli za viongozi ambazo zinakiuka sheria.
Mbowe
alisema vyama vyote vikiamua kukaa kimya na kuacha mambo yaliyotokea Zanzibar,
yaliyotokea Dodoma na yanayotokea sasa kutokana na kauli za viongozi, ni wazi
nchi haitakuwa salama.
“Tukiamua
sote kujifanya wanafiki kusema hewala nchi haitakuwa salama itazaa taifa la
watu wenye hofu na ndiyo sababu tumeamua kamati kuu kuanzia sasa kufanya kazi
kila siku kuisaidia sekretarieti,” alisema.
Mbowe
alisema kutokana na unyeti wa Ukuta, Kamati Kuu ya Chadema imeunda kamati ndogo
tano, ambazo zitasaidia kufikiwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuhusisha taasisi
na vyombo vingine.
Alisema
pia kuna kamati ya maandalizi ya Ukuta ambayo tayari imeanza kazi ya kufafanua
maamuzi ya kamati kuu, ambayo sasa imesambaa katika kanda zote kutoa elimu kwa
viongozi wa Chadema.
“Katika
kanda zote nchi nzima viongozi watakwenda kuzungumza na wanachama wa kada zote
na kuwaelimisha kwanini Kamati Kuu imefikia maamuzi ya kuanzisha Ukuta kabla ya
kushiriki mikutano na maandamano Septemba Mosi,” alisema
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “ CHADEMA WATANGAZA SAFU YA MAANDAMANO YA UKUTA....LOWASSA APANGIWA MBEYA, KATIBU MKUU MWANZA”
Post a Comment