Monday, August 22, 2016

MAAMBUKIZI MAPYA YA VIRUSI VYA UKIMWI (VVU) YAPUNGUA




Serikali imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama na watoto pamoja na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi (VVU)katika kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 2005 hadi 2015.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akitoa ripoti ya utekelezaji wa sera ya afya ya mwaka 2005/2015 jijini Dar es Salaam.

Kuhusu vifo vya akina mama na watoto, Ummy amesema kuwa vifo vya watoto wanaozaliwa vimepungua kutoka vifo 112 katika kila vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2005 hadi kufikia 54 katika kila vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2010 .

“Mwaka 2005 idadi ya vifo vilivyotokea ni 578 katika vizazi hai laki moja, lakini kwa mwaka 2012 vimepungua hadi kufikia 432 katika vizazi hai 100,000.” amesema.

Amesema ingawa serikali imefanikiwa kuvipunguza vifo hivyo, atahakikisha anapambana na vifo vya akina mama na watoto.

Kuhusu maambukizi mapya ya VVU, amesema yamepungua kutoka asilimia 7 kwa mwaka 2004 hadi asilimia 5 kwa mwaka 2012/2015.

“Maambukizi mapya ya VVU yamepungua ambapo sasa kati ya watu 100, watu 5 wanamaambukizi mapya ya VVU, ” amesema.

Amesema serikali imefanikiwa kutoa huduma za afya kwa walionaupungufu wa kinga mwilini (Ukimwi) ikiwa ni pamoja na kutoa dawa za kupunguza Makali (ARV)

“Awali wagonjwa 16,199 nchi nzima ndiyo walikuwa wanapata vidonge vya kupunguza makali lakini sasa zaidi ya wagonjwa laki saba nchi nzima huipata huduma hiyo, ” amesema.

Ameongeza “Katika vituo vya kutoa huduma za wagonjwa wa ukimwi wagonjwa wamepungua jambo linaloashiria kuwa wagonjwa wapya wamepungua.” amesema.

Amesema hivi sasa serikali imeandaa sera inayofahamika kama ‘Pima na Tibu’, kwa lengo la kila mtanzania kupima VVU na watakaobainika na maambukizi wataanzishwa dozi ya kupunguza makali papohapo.

Aidha, Ummy amesema kuwa katika kipindi cha miaka kumi ya utekelezaji wa sera hiyo serikali imefanikiwa kuongeza vituo vya afya kutoka 5,172 na sasa kunavituo zaidi ya 7,000.
“Changamoto iliyojitokeza ni kwamba licha ya kuongeza vituo vya afya bado kunachangamoto ya miundombinu. Upungufu wa watumishi wa afya hususan katika mikoa ya kanda ya ziwa,” amesema.
Na Regina Mkonde

0 Responses to “ MAAMBUKIZI MAPYA YA VIRUSI VYA UKIMWI (VVU) YAPUNGUA”

Post a Comment

More to Read