Monday, December 5, 2016

MIKOA SITA YARIPOTIWA KUWA NA KIPINDUPINDU,TAYARI WATU SITA WAMEPOTEZA MAISHA




Baada ya maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu kusimama kwa zaidi ya miezi mitatu, ugonjwa huo umelipuka tena katika mikoa sita Tanzania Bara na kusababisha vifo sita, huku idadi ya wagonjwa iliyoripotiwa kuanzia mwezi Oktoba ikiongezeka kutoka 250 hadi 458 Novemba mwaka huu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akitoa ripoti ya ugonjwa huo kwa wanahabari, amesema Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa idadi ya wagonjwa kwa kuwa na wagonjwa 282, ukifuatiwa na Dodoma 96, Mara 31, Kigoma 30, Arusha 11 na Dar es Salaam ikiwa na wagonjwa 8.

“Kipindupindu bado tunacho nchini licha ya kusimama kwa miezi mitatu hadi minne. Mwezi Oktoba mikoa 4 iliripotiwa kuwa na ugonjwa huo, Novemba imeongezeka na kufikia mikoa 6. Oktoba wilaya zilizokuwa na wagonjwa zilikuwa 6, Novemba zikawa 14. Kwa upande wa wilaya Kilosa inaongoza kwa kuwa na wagonjwa 236 ikifuatiwa na Mpwapwa yenye wagonjwa 88,” amesema.

Ummy ametaja sababu ya ugonjwa huo kulipuka tena kuwa ni ukosefu wa vyoo bora na maji safi na salama, utiririshaji maji mata, pamoja na baadhi ya Halmashauri kuficha taarifa za wagonjwa wapya.

Kufuatia sababu hizo, Ummy ameagiza ifikapo Juni 5, 2017 kila kaya nchini iwe na choo bora na kwamba kaya isiyotekeleza agizo hilo itachukuliwa hatua.

“Asilimia 34 ya kaya nchini ndizo zenye vyoo bora, natoa miezi 6 kila kaya iwe na choo bora. Halmashauri kuanzia sasa zianze kufanya ukaguzi ili kubaini kaya zisizokuwa na choo bora,” amesema.

Pia, ameagiza kila halmashauri nchini kutoficha taarifa za ugonjwa wa kipindupindu kwa kuhofia watendaji wake kusimamishwa kazi.

“Halmashauri nyingi zinaficha taarifa za wagonjwa wa kipindupindu kwa kuhofia kutumbuliwa, matokeo yake wagonjwa wa kipindupindu wanachanganywa na wagonjwa wengine, huu ni uuaji, tunatoa tahadhari kwa wahusika watoe taarifa mapema ili ugonjwa huu udhibitiwe,” amesema.

Ameziagiza halmashauri ambazo kata zake hazina kamati ya afya kuanzisha kamati hizo ili ziweze kusimamia usafi na kufuatilia mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu.

Aidha, Ummy amesema serikali itawachukulia hatua maafisa afya wa kata watakaoshindwa kudhibiti utitirishaji maji taka katika mitaa.

0 Responses to “ MIKOA SITA YARIPOTIWA KUWA NA KIPINDUPINDU,TAYARI WATU SITA WAMEPOTEZA MAISHA”

Post a Comment

More to Read