Friday, February 17, 2017

SERIKALI ZANZIBAR WAMPA JECHA RUNGU


 
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepitisha Muswada wa Sheria ambao ukiridhiwa na Rais wa Zanzibar, itampa nguvu zaidi Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuhakikisha hakuna mtu anajitokeza tena kuharibu uchaguzi. Kwa muswada huu wa sheria mpya, Mwenyekiti wa ZEC atakuwa na nguvu ya kutangaza uamuzi wowote bila kuiitisha kikao cha wajumbe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema kuwa muswada huo haukuandaliwa kwa kubahatisha na kwamba kikubwa kilichofanyika ni kuangalia kasoro zilizopo ndani ya tume na kuamua kuzifanyia kazi. Alisema katika Uchaguzi Mkuu uliopita kuna mambo mengi yalijitokeza ya upotoshaji wa jamii, hivyo anaamini muswada huo ukipitishwa na kuwa sheria utasaidia kuiboresha tume katika utendaji kazi.
Kuhusu suala la waangalizi wa uchaguzi, Aboud amesema kuwa waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi watafungiwa kuangalia uchaguzi kwa muda wa miaka 10 iwapo watapatikana na hatia ya kutoa taarifa za uongo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alipokuwa akifunga mjadala wa Muswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar namba 9 ya mwaka 1992 katika Baraza la Wawakilishi.
Alisema serikali imekubali mapendekezo ya wajumbe wa Baraza hilo ya kuweka adhabu kali kwa waangalizi wanaotoa taarifa zisizo sahihi kwa kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 3.5 au kutumikia adhabu ya kuanzia mwaka mmoja hadi mitano jela.
“Taasisi yoyote haitaruhusiwa kuwa na waangalizi kwa muda wa miaka 10 kama itapatikana na hatia ya kutoa taarifa za uongo wakati wa uchaguzi pamoja na adhabu ya kulipa fedha au kifungo,” alisema Aboud.

0 Responses to “SERIKALI ZANZIBAR WAMPA JECHA RUNGU”

Post a Comment

More to Read