Saturday, March 15, 2014

AL AHLY WATUA DAR WAWAFUATA CANAVARO, DIDA.



‘Canavaro’
Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga.


siku chache baada ya kuonyesha uwezo mzuri kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, imefahamika kuwa ule mpango wa timu hiyo ya Misri kuwasajili Nadir Haruob ‘Canavaro’ na Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga, umeendelea kwa kasi.

Habari za uhakika ni kuwa Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, wametuma mashushushu wake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia nyendo za wachezaji hao kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho ya kuwasajili.

Al Ahly ilivutiwa na wachezaji hao kutokana na uwezo mzuri katika mechi zote mbili, ile ya Dar na ile ya Alexandria, Misri, ambapo Yanga iliondolewa kwa penalti 4-3 baada ya matokeo ya jumla ya bao 1-1. Habari ambazo tumezipata kutoka ndani ya Yanga zimesema kuwa Waarabu hao wametua jijini Dar es Salaam, juzi Alhamisi na leo Jumamosi wataenda Morogoro kwa lengo la kuwafuatilia nyota hao katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri.

“Tulijua ni utani kumbe jamaa wapo siriasi, mashushushu wao wametua nchini jana (juzi) na kesho (leo) wataenda Morogoro kuwashuhudia wachezaji hao watakapokuwa wanacheza dhidi ya Mtibwa.
“Hata hivyo, mara baada ya kufika nchini waliwasiliana na mmoja wa viongozi wetu na kumwambia kuwa watakuwa hapa kwa zaidi ya wiki mbili wakiwafuatilia wachezaji hao,” amesema mtoa habari huyo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, alipoulizwa juu ya suala hilo hakuwa tayari kulizungumzia, amesema: “Siwezi kulizungumzia suala hilo, nipo bize sana, nitakuwa nikifanya kazi ya msemaji ambaye hatanilipa.”

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alipoulizwa juu ya suala hilo alisema: “Sina taarifa yoyote juu ya watu hao.”

Tangu ujio wa kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm, katikati ya msimu huu, Dida amekuwa chaguo la kwanza wakati Cannavaro naye amerejea katika kiwango cha juu baada ya kupata wakati mgumu kutoka kwa mashabiki wa timu yake waliokuwa wakimshutumu kushuka kiwango.

0 Responses to “AL AHLY WATUA DAR WAWAFUATA CANAVARO, DIDA.”

Post a Comment

More to Read