Thursday, March 27, 2014

KUHUSU SAKATA LA WATANZANIA KUFANYISHWA UKAHABA CHINA, WAZIRI MEMBE ATOA KAULI.




WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imebaini kuwepo mtandao wa wanaosafirisha wasichana wenye umri mdogo kutoka nchini na kuwapeleka China kisha kuwafanyisha vitendo vya ukahaba pasipo ridhaa yao.
 
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusu wizara yake.
 
Alisema mtandao huo ukishasafirisha wasichana hao na kuwafikisha China, huwanyang'anya hati zao za kusafiria na kujikuta wakishindwa kurejea nyumbani, hali inayowalazimisha kujikuta wakitumbukia kwenye biashara hiyo.
 
Membe alisema, taarifa ambazo wizara yake inazo ni kwamba, tayari mmoja wa wasichana hao amefariki kwa kuuawa. Alisema mwezi uliopita walialikwa kwenda nchini China, ambapo walibaini kuwepo kwa vitendo hivyo vya kusafirisha wasichana kutoka Tanzania na kuwapeleka nchini humo ili kuwafanyisha ukahaba.
 
"Inaelekea kuna Watanzania wanaokwenda nchini China kwa kutumia nyaraka bandia, huku wengine wakitumia paspoti ya nchi zingine wakati wao ni Watanzania ili kusafiri nje ya nchi kwa lengo la kufanya biashara ambazo ni haramu," alisema Membe.
 
Alisema kutokana na kukithiri kwa hali hiyo, Rais Jakaya Kikwete, atakuwa na ziara ya kutembelea nchi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine ataenda kujionea hali halisi ya kuwepo kwa vitendo hivyo.
 
Kwa mujibu wa Waziri Membe, zaidi ya Watanzania milioni 3 wanaishi nje ya nchi, lakini baadhi yao wapo wanaofanya ukabaha, biashara za dawa za kulevya na ugaidi. "Kufanya vitendo hivyo ni kuivunjia heshima nchi yetu," alisema na kuwataka Watanzania wasirubuniwe kwenda nje ya nchi kwa kudhani kuwa maisha ya huko ni rahisi.
 
Aliwataka wenye mitandao ya kuendesha madanguro ya ukahaba nje kwa kutumia wasichana wa Kitanzania wajue kwamba kufanya hivyo ni kosa la jinai. Aliwataka Watanzania wanaoishi huko waishi kwa kufuata misingi ya nchi na taratibu husika ili kulinda heshima ya nchi.
 
Wakat i huo huo, Waziri Membe alisema wizara yake kwa kushirikiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu, watatuma timu kwenda nchini humo ili kutambua watu wanaoendesha biashara hiyo ili kuikomesha.
 
Katika hatua nyingine, Waziri Membe, alisema Tanzania imekubali kupeleka wanajeshi wake Sudan Kusini kwa ajili ya kushiriki wengine kulinda amani. Alisema Tanzania imefikia hatua hiyo baada ya kuombwa kutokana na kazi nzuri ambayo wanajeshi wa JWTZ wamefanya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
 
"Kwa sasa hivi maandalizi hayo yapo katika hatua za mwisho na Tanzania itaendelea kuimarisha diplomasia ya ushirikiano baina ya nchi jirani katika kulinda na kudumisha amani,"alisema Membe.
 
Kwa upande wa mgogoro, alisema Juni, mwaka huu ujumbe wa Tanzania utakutana na jopo la usuluhishi wa mgogoro huo kwa lengo la kujadili faida na hasara za mpaka huo kuwa katikati ya Ziwa Nyasa.
 
Alisema mkutano huo ulikuwa ufanyike Mei, mwaka huu,lakini kutokana na Malawi kuwa na uchaguzi, mkutano huo umesogezwa mbele.
 
Akizungumzia uhusiano wa Tanzania na Rwanda, Waziri Membe, alisema kumekuwa na msuguano sana baina ya nchi hizo, lakini Tanzania haina ugomvi na majirani zake.

0 Responses to “KUHUSU SAKATA LA WATANZANIA KUFANYISHWA UKAHABA CHINA, WAZIRI MEMBE ATOA KAULI.”

Post a Comment

More to Read