Wednesday, March 12, 2014
RAIS JK ATANGAZA KIAMA CHA MAJANGILI.
Do you like this story?
Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali imenuia
kumaliza kabisa ujangili nchini, ikiwa ni hatua ya kunusuru wanyama walio
hatarini kutoweka katika hifadhi za taifa.
Hakusita kusisitiza kwamba, nia ya dhati ya Serikali
ni kuhakikisha mkakati huo unakamilika, japokuwa kumekuwa na changamoto
zinazotokana na ukubwa wa hifadhi hizo na uhaba wa vitendea kazi pamoja na
askari wa wanyamapori.
Akizungumza wakati wa kupokea magari 11 ya kisasa
kwa ajili ya kusaidia operesheni ya kupambana na ujangili kutoka kwa Shirika la
Frankfurt Zoological Society (FZS) la Ujerumani, Kikwete alisema tatizo hilo
limekuwa la muda mrefu, lakini juhudi za kulikomesha zinafanyika.
Alisema, pamoja na ukubwa wa tatizo hilo, bado kuna
tatizo la uhaba mkubwa wa wafanyakazi wanaotakiwa kudhibiti majangili, ambapo
kwa sasa kuna wafanyakazi 1,155 sawa na asilimia 24 tu ya mahitaji halisi ya
wafanyakazi 4,000 wanaohitajika.
"Mwaka uliopita, Serikali ilisimamia ajira ya
wafanyakazi 449 na sasa kuna ajira ya wafanyakazi 500.
Kwa maana hiyo tutafikisha wafanyakazi wapya 949 na
kufanya mahitaji ya wafanyakazi wapya kuwa 4,000 zaidi ili kuwezesha
utekelezaji wa majukumu kwa viwango vya kimataifa," alisema.
Kwa mujibu wa viwango vilivyopo sasa, mfanyakazi
mmoja anasimamia eneo la kilometa za mraba 169 ikilinganishwa na viwango vya
kimataifa vya kilometa za mraba 25 kwa kila mfanyakazi mmoja.
Rais Kikwete amesema kwa sasa Serikali itaendelea
kuajiri idadi hiyo ya wafanyakazi kila mwaka kwa miaka mitatu ijayo ili
kuhakikisha pengo lililopo linazibwa.
Alisisitiza kuwa, kampeni dhidi ya ujangili ni suala
la kimataifa na Tanzania au nchi zilizoathirika hazitaweza kulikabili bila
ushirikiano wa kimataifa.
Amesema upo ulazima wa kuteketeza mitandao yote ya
ujangili na kuwawajibisha ipasavyo watakaonaswa, kwani kwa kufanya hivyo
kutasaidia kulinda urithi huo wa dunia.
Ukosefu wa vifaa
Akifafanua, Rais Kikwete alisema kuongeza idadi hiyo
ya wafanyakazi pekee haitakuwa na maana iwapo hawatakuwa na vifaa maalumu vya
kisasa vitakavyowawezesha kukabiliana ipasavyo na tishio la ujangili.
Katika mkakati wa maboresho hayo, Kikwete alisema
wanafanya jitihada za kuongeza idadi ya magari, kuongeza vifaa vya kisasa kwa
ajili ya doria na vifaa vya mawasiliano, ambavyo vinahitaji uwezo mkubwa wa
kifedha ambao utaweza kutekelezwa na serikali kwa kipindi kirefu iwapo
haitapata msaada wa uwezeshaji kutoka kwa wadau.
Msimamo wa Wizara
Akizungumzia msimamo na mikakati ya Wizara ya Maliasili
na Utalii, Waziri Lazaro Nyalandu alisema kutokana na ukubwa wa tatizo,
wanahitaji vifaa vya kisasa zaidi, ikiwamo helikopta na ndege zisizo na rubani
kwa ajili ya kufanya doria kwenye maeneo yote ya mbuga na hifadhi za taifa.
Aliwatahadharisha wafugaji wanaopenda kuingiza
mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi, akiwataka kuondoa mifugo yao mapema kwa
kuwa katika operesheni hiyo hakuna atakayeachwa.
"Katika operesheni hii, hakuna jangili wala
mfugaji atakayeachwa iwapo atakutwa kwenye maeneo ya hifadhi," alisema.
Alifafanua kwamba, msaada huo wa magari utapelekwa
maeneo tofauti, matano kanda nane za Selous, mengine matano Hifadhi ya
Serengeti na moja Hifadhi ya Maswa.
Mwaliko wa vyombo vya habari
Nyalandu amesema Wizara yake imevialika vyombo vyote
vya habari vya kimataifa kwa ajili ya kuja kupata taarifa sahihi kuhusu kampeni
dhidi ya ujangili zinavyotekelezwa ili kuepuka ripoti za upande mmoja kwa ajili
ya kuweka usawa.
Amesema hatua hiyo ilichukuliwa na wizara yake
walipokwenda kwenye mkutano maalumu na Rais Kikwete ulioandaliwa na mtoto wa
Mfalme wa Uingereza, Prince Charles kwa ajili ya kuangalia namna ya kulinda
wanyama walio hatarini kutoweka duniani, wakiwemo tembo na faru.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS JK ATANGAZA KIAMA CHA MAJANGILI.”
Post a Comment