Wednesday, March 12, 2014

WASOMI WALIPONDA BUNGE LA KATIBA.




Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Dk Charles Kitima.


Baadhi ya wasomi nchini wameuponda utaratibu wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutumia muda mrefu kutengeneza kanuni na kusema kitendo hicho ni matumizi mabaya ya fedha za walipakodi.

Hatua hiyo imekuja baada ya wajumbe wa Bunge hilo kutoleana matusi na kupingana bila hoja za msingi katika kujadili kanuni za kuongoza bunge hilo.

Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Dk Charles Kitima alisema jana kuwa kitendo cha wajumbe hao kulumbana na kutukanana hadharani, kimewakatisha tamaa wananchi.

“Wajumbe wametumia muda mwingi wavijadili vifungu ambavyo havina maana kama vile kujadili mavazi, wananchi wanaona kwa mwenendo huo wanaweza wasipate Katiba inayofaa,” amesema Kitima.

Amesema wajumbe hao wanatakiwa kubadilika na kuachana na malumbano yasiyo na tija ili watekeleze kazi waliyotumwa na wananchi.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika cha Moshi, Prosper Kimaro alisema wananchi walidhani kwamba kazi hiyo ingefanyika kwa umakini na kwa wakati.

“Matokeo yake wananchi wamewasikia wajumbe hao wakitukanana hadharani, wanajiuliza watu wa aina hiyo watatengeneza katiba inayofaa kweli,” amesema.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Musoke alieleza kutokuridhishwa na uendeshwaji wa mijadala bungeni na kuushauri uongozi wa bunge hilo kusimamia nidhamu ili kudhibiti vurugu ambazo zimekuwa zikitokea.

“Sidhani kama Bunge hili litakamilisha kazi yake ndani ya muda uliopangwa kwa sababu wajumbe wanatumia muda mwingi kutukanana na kubishana bila sababu ya msingi, wakisahau hoja ya msingi iliyo mezani,” amesema Musoke.

Naye Profesa Max Mmuya kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa chuoni hapo, alisema kuwa kinachoendelea bungeni ni mfungamano wa siasa za ndani ya vyama.

Amesema wabunge wanalumbana ili kutetea misimamo waliyokubaliana katika vyama vyao.
“Wajumbe wanapokutana katika vikao vyao vya chama hujadili mambo ambayo ni muhimu kwao,” amesema Mmuya.

0 Responses to “WASOMI WALIPONDA BUNGE LA KATIBA.”

Post a Comment

More to Read