Tuesday, March 18, 2014

WASOMI, WAJUMBE WATOFAUTIANA KUHUSU MZOZO WA KANUNI.




Hatua ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupiga kelele na kulivunja jana wakipinga uvunjaji wa kanuni, imepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wasomi na wanaharakati, huku baadhi wakisema ilikuwa ni sahihi na wengine wakipinga.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Haji Semboja amesema kitendo hicho ni matokeo ya kutokufuatwa kwa kanuni na taratibu.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni ya Bunge hilo, Profesa Costa Mahalu alishauri kuitwa haraka Kamati ya Bunge Maalumu la Katiba ili kunusuru vikao vya Bunge hili kuendelea.
Akizungumza baada ya kuvunjika kikao hicho jana jioni, Profesa Mahalu alisema hoja ya kuwa Mwenyekiti Sitta amevunja kanuni kwa kuanza kumpa nafasi Jaji Warioba badala ya kuanza na Rais Kikwete zitamalizwa kwa mazungumzo.

Profesa Mahalu alikiri kuwa kanuni zilizopitishwa ziliweka utaratibu, lakini akasema kwa kuwa suala la kanuni ni la kisheria, kila mtu anaweza kuwa na tafsiri yake.

“Kwa mazingira haya, siwezi kusema nani ana makosa kwani kila mtu anavutia kwake, lakini muhimu hapa ni kukaa na kufikia maelewano,” amesema.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Amir Kificho alipotakiwa kuelezea hatua zitakazochukuliwa baada ya Bunge kusitishwa, aliomba kupewa muda kwa sababu jambo hilo ni zito na walikuwa wakienda kwenye vikao.
Kwa upande wake, Dk. Hamidu Shungu wa UDSM aliwapongeza wajumbe kwa hatua hiyo akieleza kwamba wamefanikiwa kuzuia jambo hilo.

“Wajumbe walikuwa sahihi kwa kuwa Rais ni mkuu wa nchi anapohutubia mahali kama hapo, hiyo pia inatafsiriwa ndiyo uzinduzi, sasa Jaji Warioba kuwasilisha hiyo rasimu kabla Bunge halijazinduliwa inakuwa na maana tofauti,” alisema Dk. Shungu.
Alidai kwamba hatua hiyo ya wabunge imezuia mambo ambayo labda yalikusudiwa na ambayo pengine yangeegemea kwa kile anachokiamini au kukitaka Rais, hivyo kubadili mawazo ya wajumbe.

Sitta hakuwa tayari kuzungumzia utata uliojitokeza baada ya msaidizi wake kuomba waandishi wa habari kutokumhoji.

0 Responses to “WASOMI, WAJUMBE WATOFAUTIANA KUHUSU MZOZO WA KANUNI.”

Post a Comment

More to Read