Sunday, March 30, 2014
WAZIRI MKUU MHE. PINDA ASHIRIKI MAZISHI YA RC TUPA.
Do you like this story?
![]() |
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akimfariji Mzee Gabriel Tupa baba mzazi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa katika mazishi yaliyofanyika nyumbanikwa marehemu Kilosa achi 29, 2014. |
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameongoza viongozi
mbalimbali na mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuuaga mwili wa aliyekuwa
Mkuu wa mkoa wa Mara ambaye alifariki dunia ghafla Machi 25, 2014 akiwa
ziarani wilayani Tarime.
Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa marehemu
John Gabriel Tuppa kwa wakazi wa mji wa Dodoma ilifanyika leo mchana (Ijumaa,
Machi 28, 2014) kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere ambako ibada ya kumwombea
marehemu ilifanyika. Baadaye mchana, mwili wake ulisafirishwa kwenda wilayani
Kilosa, mkoani Morogoro kwa mazishi.
Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya
kutoa heshima za mwisho, Padri Chesco Msaga ambaye aliongoza ibada hiyo,
alisema Mungu aliwaumba wanadamu ili wampende na wamtumikie na kwamba marehemu
Tuppa alilitimiza jambo hilo vilivyo.
Alisema wakati wa uhai wake, Bw. Tuppa
alipenda haki na popote alipokwenda alitetea haki za wanyonge. “Sote ni
mashahidi wa jinsi alivyopenda watu na jinsi alivyowatumikia watu. Alikuwa
mnyenyekevu, aliwasikiliza wengine na alithamini michango ya wengine. Na sisi
tunapaswa kuiga hilo,” alisema.
Naye Dk. Right Mmbaga, akitoa salamu za
rambirambi kwa niaba ya Baraza la Wazee la Dodoma Mjini alisema: “Wale
watumishi ambao bado wako kazini na walipata nafasi ya kufanya kazi na Bw.
Tuppa, wajifunze kutoka kwake na wafuate nyayo zake kama njia ya kumuenzi.”
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba,
akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, alisema Chama cha Mapinduzi
kimempoteza kamisaa makini sana aliyekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu (CDA), Bw. William Lukuvi aliwaasa wakazi wa Dodoma kuenzi mambo
ambayo Bw. Tuppa aliwafanyia wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma hata kama
walikuwa hawayaoni.
“Alikuwa na upeo wa kufanya kazi kwa spidi
lakini kwa utulivu. Wakati tumeanza naye kazi hapa Dodoma mwaka 2006, kulikuwa
na shule sita tu za sekondari lakini katika kipindi cha miaka miwili
alifanikisha kusimamia ujenzi wa shule za sekondari 30,” alisema Bw. Lukuvi
ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Makanisa ya
mkoa wa Dodoma, Askofu Dk. Yohana Masinga alisema viongozi hawajui kwamba wakishateuliwa,
wao ni watumishi wa Mungu kwa sababu wanawaongoza watu walioumbwa kwa sura na
mfano wa Mungu.
.
Akinukuu neno la Mungu kutoka kitabu cha
Waebrania sura ya 13 aya ya 7, linalosema wakumbukeni waliokuwa wakiwaongoza,
ichunguzeni miisho ya mwenendo wao na iigeni imani yao, Askofu Masinga
aliwataka wote waige mfano wa utendaji kazi wa Bw. Tuppa.
“John Tuppa alikuwa ni mtendaji na kanisa
limempoteza mtu makini. Ninawaomba viongozi wa nchi hii waige mfano wa John
Tuppa. John Tuppa awe ni mfano kwao, na wafanye hivyo kwa ukombozi wa nchi
yetu,” alisema.
Bw. Tuppa anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumamosi,
Machi 29, 2014) wilayani Kilosa. Alizaliwa Januari mosi, 1950. Amewahi kuwa
Mkuu wa Wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa
kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mwaka 2011. Ameacha mke na watoto watano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MKUU MHE. PINDA ASHIRIKI MAZISHI YA RC TUPA.”
Post a Comment