Sunday, March 23, 2014

YANGA ,MBEYA CITY VITANI.




Mabingwa watetezi Yanga baada ya kutoka sare mara mbili mfululizo leo watashuka kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kuwakabili Rhino Rangers kwa lengo moja tu la kusaka ushindi ili kuendelea kuipa  presha Azam FC kileleni wa Ligi Kuu Bara.

Azam inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi nne kwa Yanga ingawa vijana hao wa Jangwani wanajivunia kuwa na akiba ya mchezo mmoja mkononi, hivyo watataka kushinda ili kuipiga kumbo Azam kileleni.

Tangu walipotolewa katika Ligi ya Mabingwa na Al Ahly, Yanga wametoka suluhu 0-0 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, kabla ya kutoka sare 1-1 na Azam Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wakongwe hao wa soka la Tanzania, wapo katika nafasi ya pili kwenye  msimamo wa ligi wakiwa na pointi 40, wakati Azam  inakalia kiti cha uongozi ikiwa na pointi 44.

Wapinzani wao Rhino kwa sasa wanakamata mkia ikiwa pointi 13 baada ya kucheza mechi 20 na kuonja ushindi mechi 2, sare saba na kupigwa mara 11.
Endapo Yanga itafanikiwa kuizamisha Rhino itafikisha pointi 43 ambazo zitapunguza pengo kati yake na Azam yenye  pointi 44, pia itaepuka hatari ya kushushwa chini ya Mbeya City iliyoko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 38 na ambayo leo itaumana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema matokeo ya sare ya bao 1- 1 waliyoyapata  dhidi ya Azam yameharibu mipango yao lakini amewataka wachezaji wake kusahau yote na kuhakikisha wanashinda kila mechi iliyo mbele yao wakianzia na  Rhino Rangers.

Yanga imebakiwa na mechi  saba dhidi ya  Rhino, Prisons, Kagera Sugar, Mgambo, JKT Ruvu, Oljoro JKT na Simba wakati Azam imebakiwa na mechi dhidi ya  Oljoro JKT, Mgambo JKT, Simba, Ruvu Shooting, Mbeya City na JKT Ruvu.

Pluijm amesema kuwa  walikuwa na kila sababu ya kuibuka na ushindi katika mechi yao ya juzi Jumatano dhidi ya Azam kwani walipata nafasi nyingi za kufunga lakini  bado jinamizi la kukosa mabao linazidi kuwaandama washambuliaji wake.
Kocha huyo wa Uholanzi anaamini kama  wangeshinda mchezo huo  wangejiwekea mazingira mazuri zaidi ya kutwaa ubingwa lakini sare hiyo imewarudisha nyuma  na sasa ni kama wanaanza upya mapambano.

“Hatupaswi kukata tamaa na matokeo hayo ingawa tulistahili kushinda kwani tulitengeneza nafasi nyingi hatukuzitumia,  kipindi cha kwanza tulicheza vizuri sana, lakini kipindi cha pili tulipoa jambo ambalo lilitugharimu.

“Sasa hivi kubwa ni kucheza kwa malengo na kuhakikisha tunashinda mechi zote tulizobakiwa nazo huku tukiombea mpinzani wetu apoteze mechi mbili tu, nawaamini vijana wangu hawataniangusha, ingawa si jambo rahisi kwani tuna mechi tatu  za ugenini hivyo inabidi tufanye kazi kubwa,” alisema Pluijm.

0 Responses to “YANGA ,MBEYA CITY VITANI.”

Post a Comment

More to Read