Wednesday, April 30, 2014
DKT BILAL MGENI RASMI UZINDUZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU.
Do you like this story?
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Gharib Bilal, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2014, katika uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba, mkoani Kagera Mei tarehe 2.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akiongea na
Waandishi wa Habari Mjini Bukoba kuhusu Mbio hizo.
Mwenge huo utakaobeba ujumbe
usemao “Katiba ni Sheria Kuu ya Nchi” wenye kauli mbiu “Jitokeze kupiga
kura ya maoni tupate Katiba Mpya” utakimbizwa katika Halmashauri/Manispaa
165 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kilele chake kitakuwa Mkoani Tabora
tarehe14/10/2014.
Ujumbe kuhusu mabadiliko ya
Katiba kwa mwaka huu, umeandaliwa mahususi kwa lengo la kuwahimiza wananchi
kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya
unaoendelea hivi sasa ambao mwisho wake ni wananchi kupiga kura ya maoni ili
tupate Katiba Mpya iliyoboreshwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Amesema Dkt.
Mukangara.
Amesema kuwa ujumbe huu
utaambatana na kauli za uhamasishaji kuhusu mapambano dhidi ya UKIMWI, Malaria,
Rushwa na Matumizi ya Dawa za Kulevya.
Dkt. Mukangara ameeleza kuwa nchi
yetu bado inakabiliwa na changamoto ya ugonjwa hatari wa UKIMWI, Malaria, matumizi
ya dawa za kulevya na rushwa, hivyo mwaka huu kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru
Serikali itaendelea kuwahimiza wananchi kupambana kwa dhati ili kumaliza
changamoto hii inayoathiri maisha ya Watanzania.
“Hata hivyo, Mbio za Mwenge wa
Uhuru pamoja na kuendelea kuhimiza umuhimu wa amani, umoja na mshikamano wa
Kitaifa; Serikali kupitia Mbio hizi imekuwa ikiwahamasisha Wananchi, Mashirika,
Taasisi na Wadau mbalimbali kuchangia kwa hali na mali kufanikisha miradi
mbalimbali ya maendeleo”. Amesema Dkt. Mukangara.
Amekumbusha kuwa falsafa ya
Mwenge wa Uhuru ni kumulika maovu ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu, kuleta
matumaini ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima
palipojaa dharau.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “DKT BILAL MGENI RASMI UZINDUZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU.”
Post a Comment