Wednesday, April 30, 2014

NI HATARI! MOURINHO AWAPA ZA USO WAJUAJI WA MPIRA KULIKO YEYE.




ZIKIWA zimebaki saa chache kushuhudia timu itakayoungana na Real Madrid katika mchezo wa fainali ya UEFA mei 24 mjini Lisbon nchini Ureno kati ya Chelsea au Atletico, Jose Mourinho ametetea mbinu yake ya kupaki basi inayolalamikiwa na makocha wengi.

Mourinho amesema kuwa kuna falsafa nyingi za soka na anashangaa wanaolalamika juu ya mbinu zake kwasababu asingefanya hivyo angekuwa anafungwa mara nyingi.

Kocha huyo raia wa Ureno alilalamikiwa `kupaki basi` na Atletico Madrid kwenye uwanja wa Vicente Calderon na kulazimisha suluhu ya bila kufungana.

Jumapili iliyopita, alitumia mbinu kama hiyo na kuwafunga Liverpool mabao 2-0 uwanja wa Anfield na kufufua matumaini kidogo ya kutwaa ubingwa, lakini kocha wa majogoo wa jiji Brendan Rodgers alimlalamikia Mourinho kwa kupaki basi na kusema anacheza mpira wa kizamani.

Japokuwa wengi wanalalamika kuwa Chelsea wanatumia mbinu za zamani nje ya mpira wa kisasa, Mreno huyo amewashangaa na kusema kikosi chake kina nguvu na kucheza mpira safi.

Mourinho katika mkutano na waandishi wa habari amesema: “Unajua, siku hizi kuna wataalumu wengi wa soka na wanafahamu zaidi mpira kuliko mimi, wana mitazamo ya juu, hakika inastaajabisha”.

“Lakini ukweli utabaki kuwa ukweli: kama timu haijilinda vizuri na kufunga mabao mengi, basi kutakuwa na tatizo kubwa”.

“Timu bila usawa sio timu. Mpinzani anapokuwa na mpira lazima ujitahidi kumzuia asikufunge. Tunapokuwa na mpira tunajaribu kufunga. Huo ndio mpira-mpira ninaoujua”.

“Nakumbuka nilisema mara ya kwanza nilipofika hapa, kama una kipa kama Petr Cech anayeweza kupiga mpira mpaka kwenye boksi la mpinzani , halafu kuna mshambuliaji kama Didier Drogba anayejaribu kila mpira wa juu, kwanini ucheze mipira mifupi?  Ukifanya hivyo labda ni mpumbavu”.

“Kama wapinzani wako wanashambulia sana kwa kushitukiza na kuna nafasi katika safu yako ya ulinzi na unawapa nafasi utakuwa mpumbavu”

0 Responses to “NI HATARI! MOURINHO AWAPA ZA USO WAJUAJI WA MPIRA KULIKO YEYE.”

Post a Comment

More to Read