Wednesday, April 30, 2014
MTIHANI MPYA KIDATO CHA NNE HUU HAPA, KUSAMBAZWA MEI 10.
Do you like this story?
Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari, Paulina Mkonongo,
alitangaza utaratibu huo jana na kufafanua kwamba lengo ni kubaini
wanaohitaji msaada kabla ya mtihani wa mwisho, ili kuboresha taaluma darasani.
Kwa mujibu wa Paulina, mtihani huo wa BRN, utafanyika kwa masomo machache lakini yanayosomwa na wanafunzi wote ambayo ni
Baiolojia, Hisabati, Kiswahili na Kiingereza.
Paulina alisema
mtihani huo wa majaribio, tayari umeanza kuandaliwa na utasambazwa kwa maofisa
Elimu nchini ifikapo Mei 10 mwaka huu, na barua kuhusu kufanyika kwa mtihani
huo imeshatumwa kwa makatibu tawala wote, ili kuanza maandalizi.
Matokeo ya mtihani
huo, yanatarajiwa kutumika kubaini mada ngumu kwa wanafunzi, wanaohitaji
msaada na kuwapa walimu mwanga kuhusu wapi wanafunzi hao wanahitaji msaada na
lengo ni kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Tayari tangu
mwaka jana mikoa 12 ilianza kushiriki katika programu iliyohusisha mafunzo kwa
walimu 4,064 wa masomo husika, na mikoa 13 iliyosalia itashiriki programu hiyo
mwaka huu.
Mafunzo ya walimu wa
mikoa hiyo 13 kwa mujibu wa Paulina, yatafanyika Juni 2014 na programu ya
mafunzo rekebishi kwa wanafunzi wenye upungufu, itaanza Julai mwaka huu
kulingana na matokeo ya mtihani watakaofanya.
“Tutatoa mtihani wa majaribio kwa wanafunzi wa kidato cha
nne, ili kubaini maeneo yenye wanafunzi wanaohitaji msaada zaidi na kutoa
utaratibu wa mafunzo rekebishi na mafunzo kazini, ili kuwajengea uwezo
walimu wa kuwasaidia wanafunzi walioko kwenye hatari ya kutofanya vema,”
alisema Paulina.
Hata hivyo, Paulina alisema katika utekelezaji utoaji wa
mtihani huo, wanakabiliwa na changamoto ya kuwapatia mafunzo wakuu wa shule
zisizo za serikali, kuchapisha kitabu cha mwongozo na ziara za wasimamizi wa
elimu katika ngazi mbalimbali kutoa ushauri.
Tayari walimu wakuu 3,001 wa shule za Serikali wamepatiwa
mafunzo na Taasisi ya Uongozi wa Elimu Bagamoyo (ADEM) katika maeneo
yaliyoainishwa, huku kitabu hicho cha mwongozo kikiwekwa kwenye tovuti ya
Wizara.
Paulina alisema mikakati endelevu iliyopo, inalenga
kuendeleza mafunzo ya walimu kazini, ili kuwajengea uwezo kulingana na wakati
na mahitaji ya mitaala.
Mbali na mafunzo hayo, pia wanalenga kuwajengea walimu tabia
ya kutunga mitihani bora ya kupima mchakato wa ufundishaji, kubaini wanafunzi
wanaohitaji kusaidiwa zaidi, kubaini mada ngumu na kutoa mafunzo rekebishi kwa
wanafunzi.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania
(NECTA), Dk Charles Msonde, alisema vitabu rekebishi vitaonesha wanafunzi
waliofanya vizuri katika kila swali, waliojibu vibaya na swali lilikuwa
likitaka nini.
Vitabu hivyo vitasaidia walimu na wanafunzi kubaini makosa
mbalimbali yanayofanywa na watahiniwa wakati wa kujibu maswali na kutumia mbinu
bora za kujibu maswali.
“Mwisho wa vitabu hivyo, kuna mada zilizofanywa vizuri na
vibaya na jinsi ya kusaidia walimu wahakikishe wanafunzi wanafaulu mada hizo,”
alisema.
Vitabu hivyo kwa shule za msingi vimetolewa vya masomo ya
Kiswahili, Hisabati, Kiingereza, Sayansi na Maarifa ya Jamii kwa ajili ya
mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2012 na 2013.
Kwa sekondari, vimetolewa kwa masomo ya Hisabati, Uraia,
Historia, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Baiolojia, Kemia na Fizikia kwa
mwaka huo.
Dk Msonde alisema Baraza pia limepewa jukumu la kupanga
shule katika makundi ya ubora wa ufaulu, ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika
shule za msingi na sekondari, na kuwajengea walimu na wanafunzi hali ya
ushindani na kujitambua kama shule imepanda au imeshuka.
Makundi ya ufaulu yatapangwa kwa kutumia rangi za kijani kwa
shule zenye ufaulu wa juu, njano kwa zenye ufaulu wa kati na nyekundu kwa shule
zenye ufaulu wa chini kwa shule za msingi na sekondari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MTIHANI MPYA KIDATO CHA NNE HUU HAPA, KUSAMBAZWA MEI 10.”
Post a Comment