Tuesday, April 22, 2014

POLISI MOROGORO YAFUATA NYAYO ZA MBEYA CITY FC.




BAADA ya kurejea ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015, klabu ya Polisi Morogoro ameanza tambo za kuja na muonekanao mpya.

Afisa habari wa klabu hiyo, Clemence Banzo ameueleza mtandao huu kuwa wapo katika mikakati mikubwa ya kuijenga timu yao kwa kusajili wachezaji chipukizi na kuimarisha masuala ya utawala mithiri ya Mbeya City FC.
“Kiukweli Mbeya City wametupa fundisho kubwa sana. Mafanikio yao yametugusa, na ipo haja ya kuiga nyayo zao”.

“Kwanza tunatarajia kufanya usajili usiojali majina kama wao. Pili tunaanza maandalizi ya mapema ili kujiimarisha zaidi”. Alisema Banzo.

Banzo aliongeza kuwa Polisi Moro ya sasa itakuwa tofauti na ya zamani kwasababu wanataka kuipeleka zaidi kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro.

‘Mashabiki ni nguzo muhimu sana katika soka, angalia Mbeya City jinsi walivyo na nguvu kwasababu ya watu wengi kuwa nyuma yao. Nasisi Polisi tunaona ipo haja ya kuipeleka timu hii kwa wananchi”.

“Tunaanza mchakato wa kufungua matawi maeneo tofauti nchini, lengo likiwa ni kuwa na uhusiano wa karibu na mashabiki wetu”. Alisema Banzo.

Aidha, afisa habari huyo alisema kuwa wamefanya kazi kubwa kurudi ligi kuu, hivyo wanataka kufanya jitihada za kushiriki kwa muda mrefu.

“Ni rahisi kushuka daraja, lakini kurudi ni changamoto kubwa. Tunamshukuru Mungu ndani ya mwaka mmoja tumerudi ligi kuu, lakini changamoto iliyopo mbele yetu ni kuwa na timu ya ushindani na si ushiriki”. Alisema Banzo.

Polisi Morogoro ni moja ya timu tatu zilizopanda kushiriki michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015.
Timu nyingine ni Ndanda fc ya Mkoani Mtwara na  Stand United ya shinyanga.


Timu zilizoshuka daraja ni Rhino Rangers ya Tabora, JKT Oljoro ya Arusha na Ashanti United ya Dar es salaam.
Ujio wa Ndanda fc unatabiriwa kuwa mzuri kutokana na uzalendo wanaounesha mashabiki wa soka mkoani Mtwara.

Baada ya timu hiyo kupanda ligi kuu, mamia ya mashabiki walijitokeza kuipokea timu uwanja wa ndege na kupanga foleni barabarani kuishangilia  inapopita mitaani.
Baada ya hapo walianzisha slogani ya `Ndanda fc kwa roho safi`, inayomaanisha wanaisapoti timu yao kwanza na kuachana na Simba na Yanga.
Hata watu wa Shinyanga wameonekana kuwa na furaha kubwa na timu yao kupata nafasi ya kucheza ligi kuu, hivyo wanatarajiwa kuiunga mkono kama ilivyo kwa wakazi wa Mbeya.
Kama timu hizi zitapata nguvu kama ya Mbeya  City fc basi itakuwa changamoto nyingine kwa timu za juu, Azam fc, Yanga na Simba.

0 Responses to “POLISI MOROGORO YAFUATA NYAYO ZA MBEYA CITY FC.”

Post a Comment

More to Read