Tuesday, April 1, 2014

WANANCHI WAPINGA GHARAMA MPYA ZA MATIBABU NA HUDUMA MPYA YA FAST TRACK KATIKA HOSPITALI YA MKOA.




Baadhi ya wananchi mjini Shinyanga wameulalamikia uamuzi wa hospitali ya serikali mkoani humo kuongeza gharama za matibabu na kuanzishwa kwa huduma maalumu kwa watu wenye fedha maarufu kwa jina la Fast Track na kutaka uamuzi huo utazamwe upya kwani itawafanya wasio na uwezo wakimbilie kwa waganga wa kienyeji.

Malalamiko ya wananchi hao yanatokana na uongozi wa hospitali hiyo kutangaza kuanza kutumika kwa viwango vipya vya matibabu kuanzia leo Aprili mosi, ambapo huduma ya cheti itatolewa kwa gharama ya shilingi 5,000/= badala ya bei ya zamani ya shilingi 1,000/= na gharama za kitanda itakuwa pia shilingi 5,000/= kwa wiki.

Wakazi hao wa Shinyanga walisema ongezeko la gharama za matibabu litachangia kwa kiasi kikubwa wananchi wasio na uwezo kushindwa kwenda hospitali na badala yake kurejea enzi za ujima kwa kukimbilia kwa waganga wa kienyeji.

“Kwa kweli pamoja na kwamba jamii tunapaswa kuchangia gharama za matibabu kama ilivyo sera ya afya hapa nchini, lakini ongezeko la kutoka shilingi 1,000/= hadi shilingi 5,000/= halikuzingatia hali halisi ya kipato cha mtanzania kwa hivi sasa, wengi tutashindwa kutibiwa maana hata mishahara yetu haijaongezwa”,alisema mmoja wa wananchi hao aitwaye Joseph Hamis.

“Ni vizuri uongozi wa hospitali yetu ukaliangalia suala hili vinginevyo watu watashindwa kwenda kupata huduma za matibabu katika hospitali ya serikali na kuanza kujitibu kienyeji au mitaani ambako huduma zake si salama sana, kila siku tunasikia zahanati za watu binafsi zinavyofungiwa kutokana na ukiukwaji wa taratibu,” aliongeza.

Naye Khadija Kassim alisema uanzishwaji wa huduma ya matibabu ya haraka kwa watu wenye fedha utatengeneza matabaka ya walionacho na wasiokuwa nacho katika kupata huduma za afya kwa vile ni wazi watu wenye fedha ndiyo watakaopewa kipaumbele zaidi na kushauri kusitishwa kwa mpango huo mara moja.

“Kuanzisha utaratibu wa Fast Track katika hospitali ya umma kutasababisha matatizo makubwa, maana madaktari wetu wataweka kipaumbele zaidi katika kuwashughulikia watu wenye fedha na sisi masikini tutabaguliwa, hii ni hatari ni vizuri mpango huu ukasitishwa, isije kuwa mfano wa tuisheni shuleni,” alisema Khadija.

Akijibu malalamiko hayo kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Maguja Daniel alikiri kuanza kutumika kwa viwango vipya vya matibabu katika hospitali yake hali iliyosababishwa na ongezeko la gharama za uendeshaji ikiwemo kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania na kwamba uamuzi huo una baraka zote za bodi ya hospitali.

Kuhusu utaratibu wa huduma ya haraka (fast track) itakayokuwa na malipo ya shilingi 10,000/= kwa ajili ya cheti, alisema hautaathiri matibabu kwa wagonjwa wengine wa kawaida kwa vile huduma hiyo itatolewa baada ya muda wa kawaida wa saa za kazi saa 9.30 mchana na haitokuwa nyakati za asubuhi.

“Ni kweli kuanzia Aprili Mosi ,2014 huduma zote za matibabu katika hospitali yetu zimepanda kuanzia pale mtu anapochukua cheti kwa ajili ya kwenda kuonana na daktari itakuwa ni shilingi 5,000/= badala ya shilingi 1,000, akilazwa shilingi 5,000/= kwa siku saba, upasuaji mdogo sasa ni shilingi 40,000/= na mkubwa shilingi 80,000/=,”

“Kwa upande wa vipimo vidogo vya kawaida kama vile B/S, choo ndogo na kubwa itakuwa shilingi 2,000/= badala ya shilingi 300/=, tohara shilingi 40,000/=, ushonaji majeraha machache shilingi 20,000/=, michubuko shilingi 10,000/= ambapo kwa atakayepasuliwa jipu atatozwa shilingi 40,000/=,” alieleza Dkt. Daniel.

Hata hivyo alisema viwango hivyo ni kwa hospitali  hiyo ya mkoa ambayo ni ya rufaa kwa ngazi ya mkoa na kwamba ni vyema wakazi wa mjini Shinyanga wakajenga utaratibu wa kuanzia kupata matibabu katika hospitali za manispaa ambako pia kuna huduma zote na inaposhindikana ndipo waende katika hospitali hiyo.

0 Responses to “WANANCHI WAPINGA GHARAMA MPYA ZA MATIBABU NA HUDUMA MPYA YA FAST TRACK KATIKA HOSPITALI YA MKOA.”

Post a Comment

More to Read