Friday, May 23, 2014

CECAFA NILE BASIN CUP: PAZIA KUFUNGULIWA LEO KWA VICTORIA UNIVERSITY KUVAANA NA MALAKIA FC, MBEYA CITY FC KUWASILI KHARTOUM MCHANA


Victoria University wanaanza kampeni yao leo

Wakati huo huo CECAFA wamesema Mbeya City wanawasili leo ijumaa nchini Sudan na wanatarajia kutua Khatoum mchana wa leo.


MICHUANO mipya ya CECAFA Nile Basin Cup inatarajia kuanza kutimua vumbi nchini Sudan leo ijumaa kwa mechi tatu kupigwa kwenye viwanja viwili tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na CECAFA asubuhi hii, Victoria University kutoka nchini Uganda atakabiliana na Malakia FC kutoka Sudan Kusini katika uwanja wa Al-Merreikh mjini Khartoum majira ya saa 11:30 jioni.
Baadaye katika uwanja huo huo, wenyeji, Al-Merreik wataoneshana kazi na timu ya Polisi kutoka visiwani Zanzibar majira ya saa 2:00 usiku.

Mbali na mechi hizo za Khartoum, mechi nyingine itapigwa mjini Shandi, ambapo wenyeji Al-Shandi watavaana na wageni, Dkhill FC kutoka nchini  Djibouti.

Kueleka katika mechi za leo, makamu wa rais wa CECAFA, Lawrence Mulindwa amezitaka timu zote kucheza mpira kwa kiwango cha juu na kuzingatia nidhamu wakati wote wa mashindano.

Aidha, Mulindwa ameishukuru serikali ya Sudan kwa kukubali kudhamini michuano hii mipya.

“Sisi kama CECAFA tunaishukuru sana serikali ya Sudan kukubali kudhamini mashindano haya. Tunaomba vyombo vya habari vitoe sapoti kwa mashindano haya”. Alisema Mulindwa katika mkutano na waandishi wa habari jana jioni katika Hoteli ya Grand Holiday Villa.

Akizungumza katika mkutano huo huo, katibu mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alikanusha taarifa zilizoenea kuwa mashindano hayo yapo kwa ajili ya mambo ya siasa.
“Mashindano haya hayahusiana na siasa hata kidogo. Mto Nile unashikilia maisha ya mamilioni ya watu (hususani hapa Sudan na Misri) na sisi kama wadau wa soka tunatakiwa kuhakikisha maji yanatunza maisha ya watu bila matatizo”. Amesema Musonye wakati akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari.

Kuhusu klabu mbili za Misri zilizojitoa katika mashindano hayo, Musonye alisema timu hizo mbili zilitaka mashindano yasogezwe mpaka mwezi julai, jambo ambalo haliwezekani.

Mbeya city fc wataanza kampeni zake kesho majira ya 11:30 jioni, mjini Khartoum dhidi ya AcademieTchite ya Burundi.
Nao AFC Leopards kutoka Kenya watasili kesho jumamosi kwa ndege ya shirika la Rwanda.

0 Responses to “CECAFA NILE BASIN CUP: PAZIA KUFUNGULIWA LEO KWA VICTORIA UNIVERSITY KUVAANA NA MALAKIA FC, MBEYA CITY FC KUWASILI KHARTOUM MCHANA”

Post a Comment

More to Read