Tuesday, May 13, 2014
KIINGILIO MECHI YA TAIFA STARS 5,000, RAMBIRAMBI MSIBA WA MKUFUNZI KASINDE
Do you like this story?
Kiingilio cha chini cha mechi ya
kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika 2015
nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (Mighty Warriors)
itakayochezwa Jumapili (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh.
5,000.
Washabiki watakaolipa kiingilio
hicho ni kwa wale watakaokaa kwenye viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani.
Kwa upande wa VIP B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati kwa VIP A itakuwa
ni sh. 20,000.
Tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa
siku moja kabla ya mechi hiyo katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam, na
uwanja siku ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Mart Nooij inatarajia kurejea
jijini Dar es Slaam kesho (Mei 14 mwaka huu) kutoka Mbeya kuendelea na
maandalizi ya kuikabili Zimbabwe.
RAMBIRAMBI MSIBA WA
MKUFUNZI KASINDE
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mkufunzi wa waamuzi nchini,
Omari Kasinde kilichotokea jana (Mei 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Mbali ya kuwa Mkufunzi, Kasinde
ambaye anazikwa leo (Mei 13 mwaka huu) mchana katika Makaburi ya Kisutu, Dar es
Salaam pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati iliyopita ya Waamuzi ya TFF
iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Kapteni mstaafu Stanley Lugenge.
Msiba huo ni mkubwa katika fani
ya mpira wa miguu nchini kwani, Kasinde enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa
katika mchezo huu tangu akiwa mwamuzi na baadaye mkufunzi na kiongozi..
TFF tunatoa pole kwa familia ya
marehemu Kasinde, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na
Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa na subira
na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina
lake lihimidiwe. Amina.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KIINGILIO MECHI YA TAIFA STARS 5,000, RAMBIRAMBI MSIBA WA MKUFUNZI KASINDE”
Post a Comment