Tuesday, May 13, 2014
HATARI: JENGO LAPOROMOKA HUKO ZANZIBAR, TAZAMA PICHA ZOTE HAPA.
Do you like this story?
Mamlaka ya
Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya
Usafiri zimekumbushwa kuendelea kuzuia uingiaji wa gari kubwa zenye uzito
wa zaidi ya Tani Mbili katika eneo la Mji Mkongwe ili kunusuru majengo yaliyono
ndani ya mamlaka hiyo.
Kumbusho hilo
limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alipofanya ziara fupi kukagua athari ya nyumba iliyoporomoka ukuta
na Dari yake juzi usiku iliyopo Mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja
Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif
alisema ukaidi wa baadhi ya madereva wa gari kubwa kupitisha Gari gari
zao katika eneo hilo umesababisha uchafuzi wa mandhari na haiba ya Mji mkongwe
wa Zanzibar ambao hivi sasa uko katika urithi wa Kimataifa.
“ Jeshi la
Polisi wakati huu litahitajika kuwa na kazi ya ziada katika kuhakikisha agizo
lililotolewa na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar linatekelezwa ipasavyo
“. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar akimpa pole Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Salim
Ahmed Salim kwa hasara aliyoipata alimtaka kuwasiliana na Uongozi
wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar katika juhudi zaujenzi
wa nyumba hiyo utakaozingatia mpango halisi wa uhifadhi wa Mji huo.
Akitoa
ufafanuzi wa athari nyingi zilizojitokeza ndani ya nyumba za Mji Mkongwe, Mkuu
wa Kitengo cha Ushirikiano na Utafiti cha Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa
Zanzibar Bibi Madina Haji Khamis alisema ujenzi usiozingatia utaalamu wa
Mamlaka husika pamoja na upitishwaji wa gari kubwa ndio sababu kubwa za
msingi za athari hizo.
Bibi Madina
alifahamisha kwamba baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo walikuwa
wakipandishia kuta wakati wa ujenzi au matengenezo zaidi ya uwezo wa
msingi wa nyumba hizo hali inayoleta athari ya mipasuko ya nyumba hizo
sambamba na mitetemeko ya gari kubwa zinazopitishwa pembezoni mwa nyumba hizo.
Mapema
Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Salim Ahmed Salim alimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba dalili za kuanguka kwa jengo hilo
zilijionyesha mapema kutokana na kuvimba na baadaye kupasukwa kwa eneo la mbele
la ukuta wa nyumba hiyo.
Bwana Salim
alifahamisha kwamba kutokana na hali hiyo alilazimika kuuarifu Uongozi wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliolazimia baadaye kwa
kushirikiana na jeshi la Polisi kuchukuwa hatua za kuifunga bara bara hiyo.
“ Nilijaribu
kuufuata Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe uniruhusu kuifanyia
matengenezo makubwa nyumba yangu ili baadaye niitumie kwa makazi na
familia nyangu lakini bado sijapata jibu na huku inaporomoka “. Alieleza Bwana
Salim Ahmed Salim.
Nyumba hiyo
ya ghorofa moja mpaka inaporomoka ukuta na dari yake majira ya saa sita juzi
usiku lakini hamna watu waliokuwa wakiishi ndani yake.
Mamlaka ya
Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi nyengine zimelazimika
kuzuia Gari zote zinazotumia Bara bara hiyo kutoka Vuga kuingia
Shangani au kupitia Serena ili kujaribu kuepuka hatari katika kipindi
hichi cha Mvua za Masika.
Kwa mujibu wa
hali halisi ilivyo hivi sasa gari zote zinazokusudia kuingia ndani ya eneo la
Mamlaka ya Mji Mkongwe zinalazimika kutumia Bara bara itokayo Malindi na
zisizidi uzito wa zaidi ya Tani mbili.
Mamlaka ya
Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa miaka kadhaa sasa imo ndani ya Ramani ya
Dunia ya urithi wa hifadhi ya Kimataifa chini ya usimamizi wa Shirika la Umoja
wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni { UNESCO }.
Wakati huo
huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo na
ujumbe wa Kampuni ya uwekezaji vitega uchumi vya sekta za Afya, Kilimo, Umeme,
viwanda vidogo vya mazao ya Baharini ya Lucky Exports kutoka Nchini India.
Kampuni hiyo
ambayo imefungua Matawi yake katika mataifa mbali mbali Barani Afrika tayari
imeshapata usajili wa kufungua Tawi lake Nchini Tanzania.
Katika
mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar Meneja wa Kampuni hiyo Bwana
Ravi Rai alisema Taasisi yake imelenga kutoa huduma za afya pamoja na
viwanda vidogo vidogo vya mazao ya Baharini.
Bwana Ravi
Rai alisema wakati Uongozi wa Taasisi yake ukisubiri kuanza na hatimae
kukamilisha taratibu zote za uwekezaji uwekaji wa miradi hiyo umekusudia
kusaidia kutoa ajira kubwa kwa wazalendo pamoja na kuongeza mapato ya Taifa.
Alifahamisha
kwamba utafiti wa wataalamu wa Taasisi hiyo utafanywa ili kuangalia
miradi ambayo kampuni hiyo inaweza kuiwekeza hapa Zanzibar na Tanzania kwa
ujumla.
“
Tunafarajika kuona kwamba miradi yoyote tutakayoamuwa kuitekeleza kwenye
uwekezaji wa mataifa mbali mbali duniani na hasa tukilenga zaidi Bara la Afrika
inafadhiliwa na Serikali ya India “. Alisema Meneja huyo wa Lucky Exports.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema
miradi iliyofikiriwa kuanzishwa na Uongozi wa Kampuni hiyo hapa Zanzibar
ya Sekta ya Afya na Viwanda Vidogo vidogo vya mazao ya Baharini itasaidia
kustawisha maisha naustawi wa Jamii Nchini.
Balozi Seif
aliuagiza Uongozi wa Kampuni hiyo ya Lucky Exports kutoka Nchini India
kurahisisha maombi yao ya uwekezaji ili taasisi zinazohusika na uwekezaji
ziweze kuyapitia na kutoa maamuzi yanayostahiki kwa wakati muwafaka.
Kampuni ya
Uwekezaji ya Lucky Exports ya Nchini India ambayo tayari imeshafungua matawi
yake katika Mataifa ya Ethiopia, Guinea Bisau, Malawi na Tanzania
inajihusisha zaidi na uwekezaji wa miradi ya Afya, Kilimo, Viwanda vya mazao ya
Baharini, Umeme pamoja na huduma za Reli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “HATARI: JENGO LAPOROMOKA HUKO ZANZIBAR, TAZAMA PICHA ZOTE HAPA.”
Post a Comment