Monday, May 5, 2014

PRISON HAWANA UTANI KABISA, MWAMWAJA AHITAJI `MAJEMBE` YA KAZI.




KOCHA wa Tanzania Prisons, `Wajelajela`, Mkongwe David Mwamwaja amekabidhi ripoti yake kwa viongozi ili kuanza mipango ya usajili mapema.

Katibu mkuu wa klabu hiyo, Inspekta Sadick Jumbe amesema Mwamwaja amekabidhi ripoti yenye mapendekezo yake siku mbili zilizopita na tayari ameshaiwasilisha makao makuu kwa lengo kuipitisha na kuanza utekelezaji.

Jumbe alibainisha kuwa Mwamwaja amependekeza kuongezewa nguvu katika sehemu tatu ambazo ni nafasi ya mlinda mlango, ulinzi na ushambuliaji.
“Mwalimu ameshauri tutafute kipa mwenye uzoefu na kiwango cha juu”.
“Pia tuongeze beki wa kati ili kuimarisha safu ya ulinzi. Zaidi imetuomba kuongeza nguvu  kwenye safu ya ushambuliaji ”.

“Angalia timu ilikuwa inamtegemea zaidi Michael Peter katika ufungaji, sasa Mwamwaja amesema lazima atafutwe mtu mwingine wa kusaidiana na kijana huyu”. Amesema Jumbe.

Jumbe aliongeza kuwa utaratibu wao ni kuwa,  kila wanapopokea ripoti ya mwalimu huwa wanaipeleka makao makuu ya Jeshi la Magereza ambao huijadili na kuipitisha.

Wakishaipitisha wanairudisha kwa viongozi wa klabu tayari kwa utekelezaji.

“Siku mbili tatu zijazo natarajia kurudishiwa ripoti hii, tunaanza usajili mapema”. Amesema Jumbe.
Akizungumzia maaandalizi ya msimu ujao, Jumbe alisema wanajipanga mapema ili kufuta makosa ya nyuma.
“Misimu miwili tumekuwa tukipambana nafasi za chini na pengine  kukwepa kushuka daraja”.

“Tumeshamwambia Kocha wetu Mwamwaja kuwa msimu ujao tunahitaji kushika nafasi za juu”.
“Ili kufanikiwa hili, tunatarajia kutekeleza kila pendekezo lake kwa asilimia mia 100”. Aliongeza Jumbe.
Hata hivyo, hakusita kuwashukuru mashabiki wao kwa sapoti kubwa waliyoipatia klabu yao hadi kufanikiwa kubakia ligi kuu.

“Natumia fursa hii kuwapongeza kwa moyo wa uvumilivu. Tunajua wanaipenda timu yao, kikubwa, tunajipanga vizuri msimu ujao na tunawategemea sana”. Alimaliza Inspekta Jumbe.

0 Responses to “PRISON HAWANA UTANI KABISA, MWAMWAJA AHITAJI `MAJEMBE` YA KAZI.”

Post a Comment

More to Read