Monday, May 5, 2014

RODGERS ATAMBA KUTWAA `NDOO` KWA KUPIGA MAGOLI MENGI MECHI ZA MWISHO.





KOCHA wa Liverpool, Brendan Rodgers bado ana matumaini ya kuchukua ubingwa licha ya kutolewa kileleni na Manchester City.

Vijana wa Manuel Pellegrini walipanda kileleni kwa wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa baada ya kushinda mabao 3-2 dhidi ya Everton kwenye uwanja wa Goodison Park jumamosi iliyopita, huku wakisubiri mechi ya leo baina ya Liverpool na Crystal Palace.

Kama timu zote zitashinda mechi zao mbili za mwisho, bingwa atapatikana kwa tofauti ya magoli, na Rodgers anaamini timu yake itafunga mabao mengi zaidi katika mechi zake za mwisho ili kujiweka mazingira mazuri ya kubeba taji.

“Kama kuna timu itakayofunga mabao mengi na kubadili mambo tutakuwa sisi”. Aliwaambia waandishi wa habari.

“Hakuna swali hapo. Hilo ndio lengo letu. Hakuna swali kuhusu hilo. Nimeona siku za nyuma. Chelsea waliwafunga Wigan 8-0 katika mchezo wa mwisho wa msimu (kipindi Chelsea walipotwaa ubingwa mwaka 2010).

“Siwadharau hata kidogo Newcastle, lakini kama kuna timu yoyote iliyoonesha uwezo wa kufunga magoli, ni sisi. Sisi sio watu wa 1-0. Tulionesha hilo mwanzoni mwa msimu, lakini tulichokionesha tangu mwanzoni ni kwamba tunao uwezo wa kufunga magoli mengi”. Aliongeza Rodgers.

City wanajiombea ushindi katika mechi zao mbili za mwisho dhidi ya Aston Villa na West Ham, zote zitapigwa Etihad, lakini Rodgers anaamini hawatazoa pointi zote sita.

“Ni kazi ngumu kwa City,” Aliongeza. “Aston Villa ni timu bora,  tena inayoshambulia kwa kushitukiza na wanakuwa wazuri zaidi wanapokuwa ugenini, na West Ham siku hiyo watatoa upinzani mkubwa”.

Rodgers pia alisisitiza kuwa kikosi chake hakijaathirika hata kidogo na matokeo ya kupigwa mabao 2-0 na Chelsea wiki iliyopita kwenye uwanja wa Anfield.

“Hakuna aliyekata tamaa na matokeo ya wiki iliyopita; si wachezaji, viongozi wala mashabiki”. Alieleza.

“Baada ya mchezo kuna siku nyingi za kujipanga kwasababu mabingwa siku zote wanachukua baiskeli yao na kuanza tena safari na hiki ndicho kitu nilichopandikiza katika timu hii”

0 Responses to “RODGERS ATAMBA KUTWAA `NDOO` KWA KUPIGA MAGOLI MENGI MECHI ZA MWISHO.”

Post a Comment

More to Read