Sunday, May 18, 2014

RAPA WA HIP HOP MWENYE" MASTERS"AMBAYE HATAKI KAZI.




Hata hivyo hii ni tofauti na msanii wa Hip Hop kutoka Kundi la Weusi, Nickson Simon maarufu kama Nikki wa II ambaye ana shahada ya Uzamili katika maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDMS).

Nikki wa II ambaye pia ni mshindi wa tuzo za muziki za Kilimanjaro 2014 KTMA kupitia wimbo Bora wa Hip Hop “Nje ya Box”, aliowashirikisha G Nako na Joh Makini wote kutoka Kundi la Weusi, anasema licha ya kwamba amehitimu elimu ya juu na kupata alama kubwa, hayupo tayari kuajiriwa.

Rapa huyu ambaye ni mdogo wa damu wa mwanamuziki John Simon maarufu kama Joh Makini wiki hii ameachia wimbo wake mpya “Sitaki Kazi” wimbo ambao umebeba maudhui makubwa yenye kutoa elimu kwa vijana wa rika na elimu za aina zote. 

Msanii huyu aliyeibukia katika fani mwaka 2008 na wimbo wake “Good Boy” aliokuwa amemshirikisha Rama Dee, anasema hisia alizonazo ndizo zilizomfanya atunge mistari ya wimbo huo, kutokana na maisha halisi ya vijana wa sasa.

“Niliimba wimbo huu kutokana na kuwaona vijana wengi wenye elimu ya juu wakihangaika kupita huku na kule na vyeti vyao wakitafuta ajira, kwangu mimi naona ni utumwa kwa msomi kutegemea kufanya kazi za watu wengine, badala ya kuibua cha kwako ili utoe ajira kwa wengine,” anasema.

Hata hivyo anabainisha kuwa namba ya vijana wanaohitimu stashahada, shahada ya kwanza na kuendelea inazidi kuwa kubwa na ajira ni za kubahatisha.

“Ndani ya mistari ya wimbo “Sitaki Kazi” kuna mistari inayoelezea namna kijana anavyoweza kutatua tatizo la ajira kwa kubuni vitu mbalimbali ambavyo vitazalisha pato na kuweza kuajiri maelfu ya vijana wanaohitimu mwaka hadi mwaka,” anasema rapa huyo.

Anasema ingawa nchi haina utaratibu maalumu wa kuwaandaa vijana pindi watakapomaliza elimu zao, kuna haja ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili kwa vijana husika.

“Tatizo kubwa katika nchi yetu hakuna mtu au utaratibu ambao unawaandaa vijana, lakini sisi wenyewe lazima tutambue kwamba hii ni karne ya kutengeneza ajira yetu wenyewe, ndiyo maana nimeimba wimbo huu ili kubadilisha mtizamo na fikra za vijana ambao wanategemea ajira, ni lazima jamii ibadilike,” alisema Nikki wa II.

Nikki anasema katika usanii alionao anajivunia kufanya kazi hiyo kwani ni kujiajiri inayomwingizia kipato kikubwa ukilinganisha na ajira ya ofisini ambayo ingembana na asingeweza kupata fedha ya ziada nje ya mshahara.

0 Responses to “RAPA WA HIP HOP MWENYE" MASTERS"AMBAYE HATAKI KAZI.”

Post a Comment

More to Read