Saturday, May 10, 2014

SOKOINE WAMESTAHILI KUPEWA TAIFA STARS, MALINZI WAPATIE NYASI BANDIA.




UWANJA wa kumbukumbu ya Sokoine uliopo jijini Mbeya ni moja ya viwanja vikongwe nchini Tanzania, lakini kwasasa umeanza kurudi katika ubora wake kutokana na marekebisho makubwa yanayofanyika.

Meneja wa uwanja huo, Modestus Mbande Mwaluka siku zote anasisitiza kuwa wamiliki wa uwanja huo, CCM kwa kushirikiana na wadau wa soka wanahakikisha wanaukarabati mpaka kufikia hadhi ya kimataifa.
Lengo la watu wa Mbeya ni kuona uwanja huo unatumika katika mashindano makubwa ya kimataifa, hasa kama Mbeya City fc au Prisons watafuzu michuano ya Afrika mwakani.

Kwa miaka mingi viwanja vya Uhuru, Taifa na CCM Kirumba vimekuwa vikitumika katika mechi za kimataifa kwa ngazi ya klabu na timu ya Taifa.
Japokuwa uwanja wa Uhuru bado upo katika matengenezo, lakini kabla ya kujengwa kwa uwanja wa kisasa wa Taifa, ulikuwa unatumika zaidi kwa mechi za kimataifa.

Uwanja wa CCM Kirumba mara nyingi unatumika kama mbadala wa viwanja vya Dar es salaam. Pia Shk. Amri Abeid ni uwanja ulikuwa unatumika katika mechi za kimataifa miaka ya nyuma kabla ya kudoda.

Kwa maana hiyo, mpira wa Tanzania kwa ngazi ya kimataifa ulikuwa anaonwa zaidi katika viwanja hivyo, lakini Dar es salaam ndio kitovu cha soka la Tanzania.
Kwasasa kumekuwa na mabadiliko hasa baada ya kuiona Taifa stars ikicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Malawi mei 4 mwaka huu kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa  Stars kuchezea uwanja wa sokoine Mbeya, hivyo  ilikuwa fursa muhimu kwa wakazi wa jiji hilo.
Mwenyekiti wa chama cha soka mkoani Mbeya,  MREFA, Elias Mwanjala alikaririwa na mtandao huu akisema kuwa fursa waliyoipata ni muhimu sana, na watahakikisha wanaboresha zaidi ili kuwavutia TFF.

Mwanjala alisisitiza kuwa hawatawavutia TFF kwa maneno bali ni kwa vitendo zaidi ambapo wataendeleza nguvu yao ya kuuboresha uwanja huo wenye historia ndefu.

Watu tuliofika katika uwanja wa Sokoine, hakika ilikuwa rahisi kugundua kuwa hawa jamaa wamejipanga vizuri. Uwanja upo katika hali nzuri na unavutiwa kwa wachezaji na watazamaji.

Ubora wa uwanja unaangaliwa katika vitu vingi, lakini sehemu ya kati `pitch` ni muhimu zaidi. Macho ya wengi yalilenga kutazama sehemu ya kati iliyovutia kwa nyasi za asili.

Sokoine hakuna nyasi za bandi kama ilivyo kwa viwanja vingine kama Karume jijini Dar es salaam, lakini `pitch` yake ipo katika hali nzuri.
Baada ya msimu wa 2012/2013 kumalizika, uwanja huu ulikuwa miongoni mwa viwanja vilivyofungiwa na TFF na kuwataka wamiliki kufanya marekebisho.
Tanzania Prisons ndio walikuwa wenyeji wa uwanja huo  katika michuano ya ligi kuu, wakati Mbeya City walikuwa wanautumia kwa mechi zao za ligi daraja la kwanza.
Kwa wakati ule uwanja wa Sokoine ulikuwa katika hali mbaya kuanzia sehemu ya kati, majukwaa, vyumba vya kubadilishia nguo na vyoo.

Wengi waliulaumu sana uwanja huu, na kama una kumbukumbu nzuri, kocha wa zamani wa Yanga, Mbelgiji, Tom Saintfiet aliuponda sana uwanja wa sokoine wakati walipocheza na Tanzania Prisons na kulazimisha suluhu ya bila kufungana.

Kulikuwa na ukweli kwasababu uwanja ulikuwa mbovu hasusani sehemu ya kati `Pitch`.
Baada ya msimu huo kumalizika, TFF waliufungia uwanja huo na kuwataka wamiliki kufanya marekebisho. Hapo ndipo mambo yalianzia. Meneja wa uwanja aliwahi kukaririwa akisema sasa wanajipanga kufanya mambo makubwa.

Kizuri wamekuwa watendaji na wamekwepa siasa. Kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi kuufanya uwanja uwe bora.
Kwa mwenye kumbukumbu nzuri, Prisons waliathirika mechi za kwanza za msimu wa 2013/2014 kwasababu uwanja wa Sokoine haukuwa tayari baada ya kupandwa nyasi.
Hakika ilitakiwa subira, lakini baadaye kidogo uwanja ukawa bora na kuendelea kutumika.
Baada ya hapo wakaanza kuhangaikia kuboresha miundo mbinu ya uwanja kama vile majukwaa, vyumba vya kubadilishia nguo, vyoo na maeneo mengine. Kwasasa wamefikia sehemu nzuri mpaka kufikia kukidhi mechi ya Taifa stars.

 Jana shirikisho la Tanzania TFF limetangaza kusimamisha mechi za ligi ya mabingwa wa mikoa zilizotakiwa kupigwa uwanja huo kutokana na marekebisho yanayofanyika kwa ajili ya ukaguzi wa CAF.

Mechi za RCL za kituo cha Mbeya sasa zitachezwa kwenye Uwanja wa CCM Vwawa uliopo Mbozi mkoani Mbeya.
Ukaguzi huu wa CAF ni mafanikio makubwa kwa watu wa Mbeya kwasababu muda wowote uwanja huo unaweza kupewa hadhi ya kutumika katika mechi za kimataifa.

Tayari kuna taarifa za chini kwa chini kuwa Taifa stars inaweza kuchezea uwanja wa Sokoine dhidi ya Zimbabwe mei 18 mwaka huu katika mechi yake ya awali kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.

Kama watapewa hadhi hiyo, basi yatakuwa mafanikio makubwa kwa chama cha soka mkoani Mbeya na wamiliki wa uwanja huo,CCM.
Rais wa TFF Jamal Malinzi alifurahishwa sana na wapenzi wa soka walivyojitokeza kuishangilia Taifa stars dhidi ya Malawi.
Zilikusanywa milioni 31 kutokana na kiingilia cha shilingi 5,000/=. Haikuwa haba kutokana na mazingira ya Taifa stars.

Licha ya kufika uwanjani kushangilia, kulikuwa na utofauti mkubwa sana wa ushangiliaji kwa watu wa Mbeya. Kwa muda mwingi walikuwa wanaishangilia Taifa stars tofauti na ilivyozoelekea Dar es salaam ambapo mashabiki wakati fulani wanaizomea timu.
Mashabiki walikuwa kivutio kikubwa,  na wachezaji wa stars walijisikia vizuri na kutamani kucheza mechi zao mikoani.

Kwa mafanikio haya ya Mbeya, ipo haja ya Rais Malinzi kufanya jitihada za kuwasaidia Mbeya kupata nyasi za bandia ili uwanja huo uwe bora zaidi na wa kisasa.
Tayari wataalamu wa nyasi za bandia kutoka FIFA walishafika nchini na kwenda kukagua viwanja vya kanda ya ziwa.

Malinzi ajaribu kutoa kipau mbele kwa uwanja wa sokoine kwasababu hata yeye alijifunza kitu kwenye mechi ya Stars. Alishituka na kufurahia sapoti kubwa ya mashabiki na kuahidi kuwaombea fedha FIFA ili uwanja huo upate nyasi za bandia.

Hilo ni suala zuri, lakini utekelezaji uwe wa haraka ili kubadilisha mazingira kwa Taifa stars. Hii ni timu ya watanzania na si timu ya Dar es salaam na Mwanza. Kuna haja ya kuwa na viwanja tofauti vyenye ubora wa juu ili kufikia mafanikio ya watanzania wengi kuiona Stars katika maeneo yao.
Mbeya mmestahili kupewa heshima hii kwasababu mnapenda mpira na ushangiliaji wenu ni wa hadhi ya kimataifa.

0 Responses to “SOKOINE WAMESTAHILI KUPEWA TAIFA STARS, MALINZI WAPATIE NYASI BANDIA.”

Post a Comment

More to Read