Saturday, May 17, 2014

TAIFA STARS WAKIZINGATIA MAMBO HAYA 10 WATAWAPIGA VIDUDE ZIMBABWE TAIFA


Samatta na Ulimwengu wanatua Dar leo mchana



ZIMEBAKI saa chache kuwapokea washambuliaji wawili wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya nchini demokrasia ya Congo, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu.

Kuwasili kwa nyota hawa wawili kumefufua matumaini kwa benchi la ufundi na jana kocha mkuu Mart Nooij alisema kuongezeka kwa Samatta na Ulimwengu kumekifanya kikosi chache kiwe na nguvu zaidi katika safu ya ushambuliaji.

Wanandinga hao wa Tanzania jana waliichezea TP Mazembe katika mechi ya kwanza ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya El Hilal Omdurani ya Sudan na kupigwa bao 1-0 ugenini.

Licha ya uchovu wa mchezo huo na safari waliyoianza leo asubuhi, haitawazuia kuitumikia timu yao ya taifa ya Tanzania, Taifa stars katika mchezo muhimu wa kesho dhidi ya Zimbabwe.

Taifa stars inahitaji kufunga magoli mengi katika mchezo wa kesho ili kujiweka mazingira mazuri ya kusonga mbele.
Kwa muda mrefu sasa Stars imekuwa ikivurunda, lakini kuja kwa kocha mpya kunawafanya watanzania wawe na hamu ya kufuatilia nini kitatokea.

Nooij ameiongoza Stars katika mechi moja tu dhidi ya Malawi kwenye uwanja wa sokoine jijini Mbeya na kutoka suluhu ya bila kufungana, lakini mechi ya kesho ni ya kwanza ya kimashindano kuiongoza timu ya taifa ya Tanzania.


Kila mtu ana hamu kuona mfumo wake wa uchezaji na jinsi atakavyowatumia wachezaji wa Stars ambao jana aliwasifu kuwa na vipaji vikubwa na uzoefu katika mashindano ya kimataifa.

Nooij alisema katika mchezo huo hawatacheza kwa kushindana mithiri ya vita dhidi ya Zimbabwe, bali wataingia na kucheza mpira kama walivyojiandaa.
Ili Taifa stars ifanye vizuri kesho, kuna baadhi ya mambo yanatakiwa kuzingatiwa na wachezaji. Najua wamefundishwa, lakini kilichobaki ni kuyatekeleza kwa nidhamu ya kimpira.

 Mosi; Wachezaji wetu watatakiwa kuwa shupavu, kucheza kwa kasi, kuzuia kufungwa, na kucheza kwa weledi mkubwa kwasababu nidhamu ya kimchezo ya wapinzani wao ni kubwa na wana watu wanaoweza kuamua matokeo wakati wowote akiwemo mshambuliaji hatari, Knowledge Musoma.

Pili; kila mchezaji wa Taifa stars atatakiwa kutimiza wajibu wa kazi yake kwa kuzingatia nafasi aliyopangwa. Kama ni mshambuliaji basi atazame zaidi kazi yake ya kufunga na si kuangalia kazi ya mwenzake. Japokuwa mpira wa kisasa ni kushirikiana, lakini watatikiwa kutimiza majukumu yao kwanza na baada ya hapo kuwasaidia wenzao. Sio beki muda wote anawaza kwenda kushambulia wakati jukumu lake la kwanza ni kulinda lango lake. Aende kushambulia kama kuna uwezekano na wapinzani hawawezi kuleta matatizo.

Tatu; wachezaji wa Taifa stars watatakiwa kucheza kitimu na si kibinafsi. Asitokee mchezaji anayetaka kuonekana ni nyota zaidi ya wengine. Wote watatakiwa kucheza kwa mtazamo wa kitimu na kusaidiana kwa kila namna. Kama ni mshambuliaji asilazimishe kufunga wakati hawezi. Atoe pasi kwa mwenye nafasi ili timu ipate matokeo. Hakuna faida ya kuonekana nyota wakati timu haina matokeo mazuri.

Nne; wachezaji wa Stars wanatakiwa kuulinda mpira. Wasiruhusu wapinzani kupora mipira kirahisi. Wakae na mpira, wacheze kwa kwenda mbele na kutengeneza nafasi za kufunga.

Tano; wasikate tamaa. Wanatakiwa kupambana dakika ya kwanza mpaka dakika ya mwisho. Hata kama watafungwa mapema, cha msingi ni kuendeleza mapambano mpaka kipyenga cha mwisho. Kama watajaribu kukata tamaa kwasababu wamefungwa au wameshindwa kupenya ngome ya Zimbabwe, basi malengo yao hayatatimia.

Sita; watakiwa kujenga mashambulizi ya kasi ili kuwavuruga Zimbabwe. Samatta na Ulimwengu watakiwa kwenda mbele kwa kasi, huku viungo wa stars wakijaribu kupiga pasi za mwisho. Kama watacheza kwa staili hii basi kuna uwezekano wa kufunga magoli mengi.

Saba; Taifa stars watakiwa kuimarisha zaidi safu ya ulinzi. Wasije kuacha nafasi za wazi, kwasababu itaweza kuwaathiri. Erasto Nyoni, Oscar Joshua, Nadir Haroub `Canavaro`, Agrey Moris na Kelvin Yondani watatakiwa kujenga ngome imara ili kuwanyima Zimbabwe haki ya kufunga.

Nane; watatakiwa kuwasoma wapinzani wao jinsi wanavyocheza na kuepuka kulazimishwa kucheza kama watakavyo Zimbabwe. Watatakiwa kutumia muda kusoma mchezo wa vijana hawa wa Mugabe.

Tisa; nahodha Nadir Haroub `Canavaro` na kocha Mart Nooij watatakiwa kuwahimiza wachezaji muda wote na kuwafanya wajitume dakika zote. Itakuwa muhimu kukumbushana majukumu.

Kumi: wachezaji kamwe wasifikirie kuwa  hawawezi. Lazima wajiamini hata kama Zimbabwe wataonekana kuwa bora zaidi yao.
Haya si mambo pekee yatakayowapa Taifa stars ushindi dhidi ya Zimbabwe hapo kesho. Yapo mengi lakini kwa leo haya yanatosha. Kama una yako pia toa maoni yako ili kwa pamoja tujenge.

Mtandao huu unawatakia kila la heri Taifa stars katika mechi ya kesho. Watanzania tuwe nyuma ya vijana wetu.

0 Responses to “TAIFA STARS WAKIZINGATIA MAMBO HAYA 10 WATAWAPIGA VIDUDE ZIMBABWE TAIFA”

Post a Comment

More to Read