Thursday, May 15, 2014

WANAFUNZI KAHAMA WAFANYA MITIHANI NJE WAKIWA WAMEKAA CHINI, ILI WASIANGALIZIANE.





Katika kufikia malengo ya Mpango wa matokeo makubwa sasa katika Sekta ya Elimu nchini,uongozi wa shule ya msingi majengo wilayani Kahama mkoani Shinyanga umeanzisha mbinu mpya ya ufanyaji mitihani kwa wanafunzi wao mbinu ambayo imepokelewa kwa mtazamo tofauti na baadhi ya wazazi wenye watoto katika shule hiyo.



Licha ya kuwa shule hiyo ina madawati ya kutosha uongozi wa shule hiyo umeanzisha mbinu hiyo mpya ambapo wanafunzi wanafanya mitihani yao wakiwa wamekaa chini katika uwanjani wa shule hiyo bila madawati  huku wakiwa umbali wa mita mbili kila mmoja na kuandikia kwenye magoti na chini ya mchanga.



Mwalimu mkuu wa shule hiyo William Ngulu alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi wa sababu ya wanafunzi kufanya mitihani chini licha ya kuwa shule hiyo ina madawati ya kutosha alisema kuwa hiyo ni mbinu ya kuwafanya wanafunzi wake wafanye mitihani kwa akili binafsi bila kuangaliziana.



Ngulu ameongeza kuwa mitihani hiyo hufanyika mida ya asubuhi tu wakati jua likiwa halijawa kali na kwamba hali hiyo inaleta mafanikio makubwa katika shule yake katika kufikia mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) BIG RESULT NOW.
Katika hatua nyingine Mwl Ngulu amesema kuwa mbinu hiyo wameanza kuitumia toka mwaka 2013 na ndiyo siri ya mafanikio ya shule hiyo kuwa ya kwanza kiwilaya katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2013.



Naye mwenyekiti wa mtaa wa majengo ambaye ni mzazi katika shule hiyo Noel Mseveni amesema kuwa swala hilo si jema na kwamba Kitendo hicho ni kuwazalilisha watoto na wazazi na kutoa mbinu mbadala ambapo ameshauri wanafunzi hao wafanye mitihani kwa awamu mbili za asubuhi na jioni ili kuwapa fursa wote wafanye mitihani wakiwa wameketi kwenye madawati.

Kwa upande wake Afisa elimu msingi katika halmashauri ya mji wa Kahama Aluko Lukolela Aluko amesema kuwa mbinu hiyo ameianzisaha yeye alipohamia wilayani hapo na kwamba imeleta mafanikio makubwa katika kuinua elimu.

Sambamba na hayo Aluko amepinga mbinu mbadala iliyotolewa na Mwenyekiti wa mtaa huo na kusema kuwa mbinu hiyo itasababisha kuvujisha mitihani hiyo kwani wanafunzi watakaofanya asubuhi watakuwa na nafasi kubwa ya kuwaambia maswali wenzao watakaoingia jioni.

Mbinu hiyo mpya iliyoanzishwa mjini kahama katika kuhakikisha wanafunzi wanafanya mitihani kwa akili zao wenyewe bila kuibiana majibu,inamfanya mkuu wa shule ya msingi majengo Mwl William ngulu kusema kuwa katika mwaka huu 2014 shule yake itaongoza tena ma kuwa ya kwanza kiwilaya katika shule za msingi za serikali

0 Responses to “WANAFUNZI KAHAMA WAFANYA MITIHANI NJE WAKIWA WAMEKAA CHINI, ILI WASIANGALIZIANE.”

Post a Comment

More to Read