Monday, May 5, 2014

WANAFUNZI WA KIKE WAASWA KUACHA KUKIMBILIA KUOLEWA.


 Mgeni ambaye ni mwenyekiti wa ccm mkoa wa Iringa  Jesca Msambatavangu akizungumza na wazazi na wanafunzi wa shule ya shule ya sekondari ya wasichana Iringa katika ukumbi wa shule hiyo hivi karibuni.

Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya wasichana wakiwa katika mahafali yao


WANAFUNZI wa kike wanaotarajiwa kuhitimu elimu ya kidato cha sita wameaswa kujiamini,kujitambua na kufahamu wajibu wao kwa jamii inayowazunguka kwa kutokukimbilia kuolewa kwa lengo la kujikomboa kifikra na kiuchumi na kutimiza ndoto za maisha yao.

Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa, Jesca Msambavangu,wakati wa harambee na mahafali ya 22 ya shule ya sekondari ya wasichana ya Iringa na kufanyika katika ukumbi wa shule hiyo mjini hapa.

Msambavangu alisema imeibuka kasumba kwa wanaume wengi kukimbilia kwa wasichana wadogo na kuwaharibia maisha yao kabla hawajatimiza ndoto zao za maisha kutokana na kupewa ujauzito na wanaume wenye nia mbaya na maisha ya mabinti.

Alisema ndoto nyingi za wasichana zinakatishwa na wanaume wakware na wasichana wengi wanamalengo ambayo wanataka kutimiza lakini kutokana na mabadiliko ya haraka kwa watoto wa kike yanaweza kukuletea madhara kuliko faida na kuwataka kukazania masomo.

“Asilimia kubwa ya wazazi wanataka mtoto wao asome afikie ngazi kubwa kama baadhi ya viongozi wa kike waliomadarakani lakini kwa tamaa za chips kuku wengi wenu mmekuwa mkiishia njiani, nawaomba sana watoto wangu msiende njia ambayo wakware watawadanganya na kuzimisha ndoto zenu za kuwa madaktari, walimu na viongozi wa baadaye someni sana” aliwaasa Msambavangu.

Amewataka wanafunzi hao kutambua thamani yao kuepuka kutumiwa vibaya na kushinda majaribu ya watu wanaotaka kuwavurugia safari ya maisha waliyoanza nayo tangu wakiwa wadogo kwa kuwakataa wanaume wenye fedha na wasiona fedha kwa kuongwa vitu vidogo vidogo vikiwemo simu na nguo.

Aidha aliwataka kuacha tabia ya wanafunzi kuchukua muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii kwa kufuatilia mambo yasiyo na msingi kwao na badala yake watumie mitandao hiyo kwa manufaa yao kielimu.

Katika harambee ya kuchangia ununuzi wa gari la shule Msambatavangu alichangia shilingi milioni 1.5 na kiasi kilichopatikana kilikuwa shilingi milioni 4 .6 kati ya shilingi milioni 25 zinazohitajika.

Awali mkuu wa shule hiyo Joyce Msigwa aliwashukuru wazazi wa wanafunzi kwa michango yao na kuongeza kuwa kuna changamoto kubwa ya usafiri wa wanafunzi katika shule hiyo na wanatarajia kukusanya fedha hiyo kuweza kuondokana na hali hiyo na kuwatakawadau kuwachangia kiasi cha fedha kilichobaki.

Alisema kuwa wanafunzi wanakabiliwa na wakati mgumu inapojitokeza dharula katika kutekeleza majukumu ya shule na wanafunzi wanapohitaji gari wakipatwa na matatizo hususani katika kipindi cha ugonjwa.

“Tunaomba wadau mbalimbali, wazazi na makampuni mbalimbali kutuchangia katika ununuzi wa gari la wanafunzi ambalo bei yake ni kubwa hivyo tunategemea sana misaada kutoka kwao na waandishi tunaomba sana mtusaidie kufikisha ujumbe kwa jamii kuweza kuwakomboa hawa mabinti wawe na usafiri wao yaliyokuwepo yote yameharibika” alisema Msigwa

0 Responses to “WANAFUNZI WA KIKE WAASWA KUACHA KUKIMBILIA KUOLEWA.”

Post a Comment

More to Read