Monday, June 23, 2014
KAMPUNI MBILI ZA UMEME KUANZISHWA BADALA YA TANESCO PEKE YAKE.
Do you like this story?
Mpango wa kuligawa Shirika la Umeme
(Tanesco) kuwa mashirika mawili umeiva, baada ya Serikali kupitisha
Mkakati na Mwelekeo wa Sekta Ndogo ya Umeme (ESI).
Mpango huo utekelezaji wake unaanza
Agosti mwaka huu, na lengo lake ni kuhakikisha uzalishaji wa umeme, unaongezeka
kutoka megawati 1,583 zinazozalishwa kwa sasa hadi kufikia uzalishaji wa
megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Ugawanyaji wa Tanesco maandalizi yake
yanaanza Julai mwaka huu na utekelezaji wake utatimia Desemba 2017,
ambako kutaanzishwa mashirika mawili.
Shirika moja litakuwa linashughulikia
uzalishaji wa umeme na lingine litakuwa la kushughulika na usafirishaji
na usambazaji wa umeme.
Lengo kubwa la kugawanywa kwa Tanesco
ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa kupatikana kwa nishati ya
umeme kwa bei rahisi, ikiwa ni pamoja na kukuza pato la mtu mmoja mmoja.
Habari zilizopatikana jana, zinasema
mwishoni mwa wiki Baraza la Mawaziri limebariki mkakati huo ;na sasa
kilichobaki ni kwa Wizara ya Nishati na Madini, kuutangazia umma juu ya kuwepo
mpango huo, unaotekelezwa chini ya mpango ujulikanao kama Electricity Supply
Industriy (ESI).
Ili kukamilisha mpango huo, Serikali
kwa sasa iko kwenye maandalizi kuhakikisha kuwa mpango huo kuligawanya shirika
hilo unatekelezwa mwaka 2017, Tanesco haitakuwa na madeni yoyote.
Kwa kuanzia mwaka huu, Wizara ya
Nishati na Madini imetenga Sh bilioni 565,71 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango
huo, ikiwa ni pamoja na kulipa madeni ya Tanesco ambayo Serikali inadaiwa.
Lengo la mkakati huo, ambao unaihusisha
Serikali, sekta binafsi, Tanesco, Ewura na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ni
kuinua pato halisi la Mtanzania kutoka pato la dola za Marekani 640 la sasa
hadi kufikia pato la dola za Marekani 3,000 kwa mtu ifikapo mwaka huo.
"Tumekuwa tunafanya vizuri kwenye
sekta ya umeme, lakini tunaamini tukitekeleza kikamilifu mkakati huu sekta ya
umeme itachangia ukuaji wa pato la taifa na pato la mtu mmoja mmoja," alisema Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi wakati akizungumza na mwandishi
jana.
Chini ya mkakati huo, idadi ya watu
waliounganishwa na umeme itaongezeka kutoka asilimia 24 ya sasa hadi kufikia
asilimia 50, huku idadi ya wananchi wanaopata huduma ya umeme, pia itaongezeka
kutoka asilimia 34 ya sasa hadi kufikia asilimia 75 mwaka 2025.
Maswi alisema mkakati huo utatekelezwa
chini ya Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 na Sera ya Nishati ya mwaka 2003, ambazo
zinatoa fursa ya Serikali kuvutia wawekezaji binafsi kushiriki katika kuzalisha
umeme.
Lakini, pia mkakati huo unalenga
kupunguza Serikali kugharimia uzalishaji wa umeme, badala yake sekta yenyewe ya
umeme, ndiyo itakayokuwa inatoa gawio kwa Serikali, kama ilivyo kwa nchi
nyingine, kama vile Thailand.
Mkakati huo pia unalenga
kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme ; na kuhakikisha kuwa mahitaji ya
umeme nchini na kwenye viwanda, yanatimizwa na wazalishaji wa sekta hiyo ya
umeme.
Ili kutekeleza mkakati huo, Serikali
imegawa utekelezaji wake katika hatua nne. Mkakati wa kwanza ni kuanzia Julai
2014 hadi Juni 2015, mkakati wa pili Julai 2015 hadi Juni 2018, awamu ya
tatu itaanza Julai 2018 hadi Juni 2021 wakati awamu ya nne, ambayo ni ya mwisho
utekelezaji wake utaanza Julai 2021 hadi Juni 2025.
Katika awamu ya kwanza, baadhi ya
shughuli zitakazofanyika ni kuunda timu maalumu ya wataalamu kutekeleza mpango
huo, kupitia upya Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 na kutekeleza mfumo wa
kupunguza mfumo wa hasara kutoka asilimia 19 hadi asilimia 18.
Pia, wataboresha mifumo itakayotumika
kwenye gridi ya Taifa wakati Tanesco itakapogawanywa. Pia, kutafanyika tathmini
za masoko, uwezo wa rasilimali watu na uanzishwaji wa mfumo wa masoko ya umeme.
Katika awamu ya pili ni kupunguza
mifumo ya hasara kutoka asilimia 18 hadi 16, kuigawa Tanesco kuwa na mashirika
mawili na kupunguza utendaji wa Tanesco kutoka makao makuu na kuzipa ofisi za
kanda mamlaka zaidi kabla ya mganyiko kufanyika.
Kwenye awamu ya tatu shirika la
uzalishaji wa umeme, litafanya tathmini kwenye ofisi zake za kanda, kuweka
mfumo wa uuzaji wa umeme kwa bei ya rejareja huku kampuni mbili zitakazokuwa
zimeundwa, zitapewa jukumu la kuhakikisha mifumo ya hasara inapungua kutoka
asilimia 16 hadi 14.
Katika awamu ya nne, Ewura itatakiwa
iandae viwango vya uzalishaji wa umeme katika sekta ndogo ya umeme,
kupunguza mifumo ya hasara hadi asilimia 12 na kuhakikisha asilimia 50 ya watu
wanakuwa wameunganishiwa umeme; huku watumiaji wa nishati hiyo wanafikia
asilimia 75 kupitia shirika la usambazaji pamoja na REA.
Kuwepo kwa ya Sheria ya Umeme na Sera
ya Nishati ambazo zinatoa fursa ya kuanzishwa kwa Sekta Ndogo ya Umeme (ESI).
Kuwepo kwa mpango wa fedha ambao hadi
kufikia mwaka 2017 mahitaji ya fedha katika sekta ya umeme, itakuwa ni dola za
Marekani bilioni 11.4, kiasi ambacho ni sawa na dola za Marekani bilioni
1.9 kwa mwaka zinahitajika kutekeleza mpango huo.
Nchi kujiwekea malengo kuwa idadi ya
watu watakaounganishwa ifikapo mwaka 2015 asilimia 30, asilimia 50 ifikapo
mwaka 2025 huku itakapofika mwaka 2033 asilimia 75 ya Watanzania watakuwa
wameunganishwa na umeme.
Kwa hali hiyo mkakati huo unafanya
Tanesco igawanywe na kuwa mashirika mawili ili kukidhi mahitaji halisi ya
nishati ya umeme.
Kutoa fursa kwa sekta ndogo ya umeme
kuchangia maendeleo kwenye dira ya taifa ya mwaka 2025, kuhamasisha upatikanaji
wa fedha na biashara katika sekta hiyo, upatikanaji wa umeme wa uhakika
na kwa bei nafuu.
Utekelezaji wa mkakati huo, utapata nguvu
zaidi baada ya kukamilika kwa bomba la gesi pamoja na ujenzi wa vinu vya
kuzalisha umeme wa gesi asilia, hali itakayofanya Watanzania kupata huduma ya
nishati ya umeme kwa bei rahisi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ KAMPUNI MBILI ZA UMEME KUANZISHWA BADALA YA TANESCO PEKE YAKE.”
Post a Comment