Monday, June 23, 2014
WAZIRI WA FEDHA WIKI HII ATAANZA KUJIBU HOJA ZA BAJETI YA SERIKALI 2014/2015
Do you like this story?
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum,
anasubiriwa wiki hii kutegua kitendawili cha hoja za wabunge, kuhusu punguzo la
kodi katika mishahara, vyanzo vipya vya mapato na utekelezaji wa miradi
wa maendeleo.
Leo ndio siku ya mwisho kwa wabunge
kujadili hotuba ya bajeti ya Waziri Saada na kesho Waziri ataanza kujibu
hoja akishirikiana na Naibu wake, Mwigulu Nchemba na Adam Malima.
Katika majibu yake, Waziri Saada
anatarajiwa kuonesha namna Serikali ilivyojipanga kusimamia nidhamu ya
makusanyo na matumizi ya fedha za Serikali, ikiwemo hatua aliyoitangaza ya
kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija.
Wabunge wengi, pamoja na kuipa Serikali
changamoto, walielezea kuridhika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika
majimbo yao, hasa miradi ya umeme vijijini na maji.
Pia ufikishaji wa bomba la gesi Dar es
Salaam ni moja ya miradi inayoipa Serikali sifa kwa kuwa matarajio ni Serikali
kuacha kutumia fedha nyingi katika ununuzi wa mafuta ya dizeli na petroli kwa
ajili ya uzalishaji umeme.
Aidha, bei ya nishati hiyo kutoka kwa
kampuni zinazofua umeme, inatarajiwa kushuka kutoka senti za Marekani 30 na 60
kwa uniti moja mpaka chini ya senti 18 za Marekani kwa uniti moja na kusaidia
Serikali kutekeleza nia yake ya kushusha bei ya umeme.
Nafuu hiyo ya bei ya umeme, mbali na
kuleta nafuu ya maisha kwa mwananchi mmoja mmoja mijini mpaka vijijini,
inatafsiriwa kuwa kivutio cha uwekezaji, kitakachochangia ongezeko la ajira na
ukuaji wa uchumi wa nchi ambao kwa sasa ni asilimia saba.
Katika mijadala ya wabunge, wengi
walipongeza hotuba ya Bajeti na kutaka maoni ya Kamati ya Bajeti, inayoongozwa
na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), yazingatiwe
kuboresha upatikanaji wa mapato.
Katika maoni ya Kamati hiyo, Chenge
alisema upo udhaifu wa Serikali katika utekelezaji wa bajeti, kutokana na
kuendelea kutegemea vyanzo vile vile vya mapato, huku matumizi yake yakiwa
makubwa ikilinganishwa na mapato.
Akiwasilisha taarifa yake, Chenge
alisema kamati yake imeshitushwa na ukuaji wa deni la taifa, akisema ilo ni
mzigo mkubwa. Alisema hivi sasa deni hilo ni tishio kwa uchumi wa taifa.
“Serikali imeendelea kuja na vyanzo
vile vile vya kiutamaduni vilivyozoeleka, ambavyo ni pombe, sigara, vinywaji
baridi na vinywaji vikali, wakati kuna vyanzo vingine vingi,” alisema Chenge.
Alitaja baadhi ya vyanzo vipya ambavyo
Kamati yake inaamini vinaweza kuingizia Serikali mapato mengi, ni pamoja na
uvuvi wa Bahari Kuu, kupiga mnada vitalu vya misitu na uwindaji wa kitalii,
kupiga mnada masafa ya mawasiliano pamoja na kodi za majengo.
Kwa mujibu wa Chenge, Kamati yake
inashangazwa na majibu yanayotolewa na Serikali kuhusu suala la ukusanyaji wa
mapato katika uvuvi wa Bahari Kuu, kwamba haiwezi kukusanya hadi itakapojenga
bandari maalumu ya uvuvi.
“Kwa taarifa rasmi za Serikali
zilizotolewa bungeni, Serikali inapoteza takriban Dola za Marekani milioni 222,
sawa na Sh bilioni 372.9. Kamati inahoji hadi hapo tutakapojenga bandari
maalumu ya uvuvi, tutakuwa tumepoteza mapato kiasi gani,” alihoji.
Alisema Kamati yake imechambua bajeti
ya mwaka 2013/2014 na kubaini kuwapo kwa madeni makubwa katika baadhi ya wizara
na taasisi mbalimbali za umma.
“Mfano Wizara ya Ujenzi imekuwa
ikitekeleza miradi ya ujenzi wa barabara bila kuwalipa makandarasi kwa wakati
na kwa kuzingatia mikataba yao na hivyo kujikuta ikianza kila mwaka wa fedha
ikiwa na malimbikizo makubwa ya madeni.
“Hali hii imesababisha Wizara hii
kutumia bajeti yake ya mwaka unaofuata kulipia madeni ya mwaka uliopita, badala
ya kutekeleza miradi iliyoidhinishwa kwa mwaka husika wa fedha,” alisema Chenge.
Akizungumza kuhusu deni la taifa,
Chenge alisema licha ya Serikali kusema deni hilo ni himilivu, lakini kwa
uhalisia deni hilo ni mzigo mkubwa kwa taifa linaloathiri uchumi wa nchi.
“Hadi kufikia Machi 2014, deni la taifa
linalojumuisha deni la Serikali na deni la nje la sekta binafsi lilifikia Sh
trilioni 30, ikilinganishwa na Sh trilioni 23 mwezi Machi, 2013,” alisema.
Chenge alitoa sababu kadhaa
zinazoifanya Kamati yake ishindwe kukubaliana na hoja ya Serikali kwamba deni
hilo ni himilivu.
“Mosi, kuna madai mengi ya ndani ambayo
hayajajumuishwa katika deni la taifa na taarifa zilizopo zinaonesha kuwa madai
haya yanaendelea kuongezeka.
"Sababu nyingine ni kwamba,
uwiano uliopo wa deni la taifa na pato la Taifa kiuchumi si wa kuridhisha, ukubwa
wa deni hili hauwiani na kiwango cha uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa sasa wa
asilimia saba.
"Pia alisema, udhaifu katika
usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na ucheleweshaji wa uhakiki wa madai ya
ndani ni sababu nyingine. Taarifa ya Waziri wa Fedha ya nusu mwaka inaonesha,
malimbikizo ya madai hadi Desemba, 2013 yalikuwa yamefikia Sh trilioni 2.09,
ambayo ni asilimia nne ya pato la Taifa,” alisema.
Wabunge wengi pia walisema punguzo la
Kodi katika Mshahara (Paye), kutoka asilimia 13 mwaka unaoisha wa fedha
2013/2014 mpaka asilimia 12 kwa mwaka ujao wa fedha 2014/2015, kuwa ni ndogo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI WA FEDHA WIKI HII ATAANZA KUJIBU HOJA ZA BAJETI YA SERIKALI 2014/2015 ”
Post a Comment