Sunday, June 22, 2014
MFUMO WA VYAMA VINGI VYA SIASA WAMFURAHISHA RAIS JAKAYA KIKWETE
Do you like this story?
Rais Jakaya Kikwete amesema mfumo wa
vyama vingi vya siasa ni mzuri, umeleta matumaini kwa kupanua wigo na kufungua
zaidi uwanja wa kisiasa na kuiwajibisha Serikali.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa
ili mfumo huo uboreshwe zaidi na uweze kuimarisha misingi mikuu ya maendeleo,
ni lazima uendeshwe kwa watu kufuata sheria na wala siyo kuingiza matumizi ya
nguvu, ambayo yanaweza kuvuruga nchi.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, aliyasema hayo juzi wakati alipotoa
Mhadhara kuhusu Usalama wa Taifa kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC)
Kunduchi, jijini Dar es Salaam.
Alikuwa anajibu swali la mwanafunzi wa
kozi ya pili kwenye chuo hicho kutoka Kenya, ambaye alitaka kujua jinsi gani
vyama vingi vya siasa, vinaathiri umoja wa kitaifa na kuibadilishaTanzania
kufuatia miaka zaidi ya 30 ya Tanzania, kuwa nchi yenye kuleta matumaini kwa
nchi nyingine za Afrika na Waafrika.
Rais Kikwete alisema: “Vyama vingi
ni vizuri. Mfumo wa vyama vingi unaleta matumaini kwa kupanua wigo wa kisiasa,
ambao haukuwa mpana kiasi hicho huko nyuma. Sasa mtu anaweza kuamua kujiunga na
chama chochote cha siasa anachokipenda yeye.”
Aliongeza kusema: “Ni mfumo ambao
unaiwajibisha Serikali. Ni mfumo mzuri kwa upanuzi wa demokrasia. Sasa watu
wanaweza hata kuamua kupunguza bajeti ya safari za Rais nje ya nchi. Wanadhani
kuwa Rais anaweza kufanikiwa zaidi na Tanzania kupita hatua za maendeleo haraka
zaidi kama Rais atabakia amejifungia ndani ya nchi.”
Rais Kikwete alizidi kujibu swali hilo:
“Jambo la maana ni kwamba tunahitaji aina mbalimbali ya mawazo. Mawazo ya
namna hiyo hayaathiri demokrasia. Mawazo ya namna hiyo yanasaidia hata chama
changu kuimarika zaidi.”
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema mfumo
huo, utavurugika, endapo baadhi ya watu wataendekeza matumizi ya nguvu na hoja
za nguvu, badala ya kupambana kwa hoja na nguvu ya hoja.
“Wasiwasi wangu ni kuingiza matumizi ya
nguvu katika ujenzi wa demokrasia. Ni makosa kwa watu kukimbilia kutumia nguvu
baada ya kushindwa kwenye hoja. Na hili halivumiliki na likitokea basi Serikali
itaingilia kati kudumisha amani,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MFUMO WA VYAMA VINGI VYA SIASA WAMFURAHISHA RAIS JAKAYA KIKWETE ”
Post a Comment