Wednesday, June 4, 2014
NAULI ZA DALADALA KUPANDA TENA.
Do you like this story?
HATIMAYE picha halisi ya gharama ya
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) awamu ya kwanza, imeonesha
nauli ya basi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwenda na
kurudi vituo vikubwa vikiwemo vya Kariakoo na Posta, itapanda kutoka nauli ya
chini ya Sh 400 ya sasa mpaka kati ya Sh 700 na Sh 800 kwa ruti moja.
Kwa wanafunzi, nauli kwa ruti moja
kwenda katika vituo hivyo vikubwa katika mradi huo ambao utaanza kwa majaribio
mwishoni mwa mwaka huu, zitapanda kutoka Sh 200 mpaka nusu ya nauli ya mtu
mzima kwa ruti husika.
Aidha, mfumo wa uendeshaji wa mradi huo
na nauli, umewekwa katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza ni usafirishaji wa
abiria kutoka maeneo ya ndani ya makazi ya watu mpaka katika vituo vidogo na
vikubwa vilivyopo barabara kuu za Dart, za Morogoro na Kawawa kwa sasa na
sehemu ya pili ni usafirishaji wa abiria kutoka katika vituo vilivyopo katika
barabara kuu ya Dart za Morogoro na Kawawa, kwenda vituo vikuu vikiwemo
Kariakoo na Posta.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es
Salaam, katika taarifa ya mwisho ya Makubaliano ya Dart, iliyotolewa katika
mkutano wa Mashauriano ya Uwekezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo wa Dart.
Mfumo wa nauli
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, abiria atakayelazimika
kusafiri na mabasi ya Dart kwa safari fupi ndani ya barabara zilizo katika
makazi ya watu, kwa mfano wa barabara inayopita Sinza; kutoka Bamaga mpaka
Shekilango, atalipa Sh 500, tofauti na sasa ambapo analipa Sh 400.
Kwa atakayetumia mabasi ya Dart kutoka
katika barabara ndogo zilizopo katika makazi ya watu, kwenda katika vituo
vikubwa vya Dart vilivyopo njia kuu za Morogoro na Kawawa ili kwenda Kariakoo,
Posta au Kimara, atalazimika kukata tiketi ya Sh 800, atakayoitumia kupata
usafiri kutoka barabara ndogo na katika barabara kubwa.
Mfano wa nauli hiyo, ni abiria
anayetoka maeneo hayo ya Sinza kwenda Kimara, Kariakoo au Posta, ambaye
atalazimika kukata tiketi ya Sh 800, itakayomwezesha kupakia basi la Dart
kutoka maeneo hayo mpaka Shekilango, ambako atabadilisha basi kwa tiketi hiyo
hiyo, kwenda Kariakoo, Posta au Kimara.
Aidha kwa abiria watakaolazimika
kutumia mabasi matatu ya Dart, kutoka katika barabara ndogo zilizopo katika
makazi ya watu, kupitia barabara kuu za Dart na kwenda katika eneo lililopo
katika barabara ndogo za makazi ya watu, watalazimika kulipa Sh 900 kwa mabasi
yote matatu.
Aina ya mabasi Kwa mujibu wa taarifa
hiyo, mabasi yatakayotumika kubeba abiria kwenye njia kuu, yatachukua watu
zaidi ya 150 kwa basi moja, ambapo abiria watakaopata viti vya kuketi ni 52 na
wengine wamewekewa eneo nadhifu la kusimama.
Kwa mabasi yatakayobeba abiria kutoka
njia ndogo zilizopo katika makazi ya watu, yatachukua watu zaidi ya 80, kati ya
hao abiria 42 ndio watakaopata nafasi ya kukaa na waliobakia wamewekewa nafasi
nadhifu ya kusimama.
Foleni, utaratibu
Kuhusu muda utakaotumika kwenye ruti
moja ya mabasi hayo ya Dart, abiria atatumia muda wa dakika zisizozidi 30
kufika anakokwenda, akitumia mabasi kwenye njia kuu, tofauti na sasa ambapo kwa
kutumia daladala abiria hutumia zaidi ya saa mbili kufika waendako.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
Jumanne Sagini, utaratibu wa ulipaji nauli kwenye mabasi ya Dart, utakuwa ni wa
kutumia mfumo wa kadi ambapo abiria anatakiwa anunue tiketi kabla ya safari.
“Hakuna kulipa nauli ndani ya basi,
abiria anatakiwa alipe kabla ya kuanza safari, na kama unapanda mabasi matatu,
unatakiwa kulipa nauli yote kwa mara moja kisha unapewa tiketi, unapoingia
kwenye basi msomaji atachukua tiketi yako na kuipitisha kwenye mashine na
kupunguza nauli ya safari hiyo, hadi hatua ya mwisho wa safari,” alisema
Sagini.
Alisema utaratibu huo, utapunguza au
kuondoa kero kwa abiria na katika mabasi madogo yanayobeba abiria kuwaunganisha
kwenye njia kuu, yatakuwa na vifaa vya mawasiliano baina ya dereva aliye
barabara ndogo na dereva aliye barabara kuu za Dart.
Tiketi kwa M-Pesa
Kwa mujibu wa Sagini, mradi huo
ukianza, abiria watanunua tiketi kwa kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu
kama vile M-pesa, Tigo-pesa, Pesa Fasta na Airtel Money.
Alisema ili kuzuia wizi na udanganyifu
kwenye vituo vya mauzo ya tiketi na kwenye vituo vya mabasi, zinafungwa kamera
na video ili kuimarisha ulinzi, na kuhakikisha mapato halali kwa ruti
zinazofanywa.
“Hii itasaidia kuondoa wizi na uhujumu
unaoweza kufanywa katika vituo vya abiria,” alisema Sagini.
Daladala kwaheri
Alisema kwa hatua hiyo, dalaldala za
sasa zitaondolewa katika zaidi ya njia 43 ambazo ziko kwenye barabara ya
Morogoro na barabara ya Kawawa na katika ruti nyingine, daladala hizo
zitaendelea kuondolewa hadi hapo ujenzi wa barabara zote za Dart utakapokamilika.
Katika mabasi hayo ya kubeba abiria
kwenye njia kuu za Dart, mabasi yanayoruhusiwa ni yale yatakayokidhi vigezo,
ambavyo ni pamoja na kuwa na upana wa meta 18 na uwezo wa kubeba abiria 150,
ambayo yanahitajika mabasi 145.
Kwa mabasi yatakayosogeza abiria hadi
njia kuu, yatatakiwa yawe na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 80 na upana wa
meta 12 na yatatakiwa mabasi 90.
Akitoa mwito kwa wawekezaji wa ndani na
nje, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Hawa Ghasia, alisema ni vyema katika sekta binafsi, wadau wa
usafiri na watu mbalimbali wachangamkie fursa hiyo.
Alisema Serikali kupitia mfumo wa
ushirikishaji sekta binafsi, umeona ni vyema kushirikisha wadau hao kwenye
mradi huo mkubwa Afrika Mashariki, ambao ukitumika vizuri ni chachu ya
maendeleo na ukuaji uchumi.
>>>Habarileo
>>>Habarileo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “NAULI ZA DALADALA KUPANDA TENA.”
Post a Comment