Wednesday, June 25, 2014
POLISI WATANGAZA MSAKO MKALI KWA WATUHUMIWA WA MAUAJI YA SISTA WA KANISA KATOLIKI.
Do you like this story?
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeanzisha msako mkali, kuwatafuta watu waliohusika na mauaji ya Mhasibu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makoka jijini Dar es Salaam, Sista Cresencia Kapuri (50), ambao utahusisha vikosi vyote vya Polisi. Vikosi hivyo ni Usalama Barabarani, askari wa doria wanaotumia pikipiki na magari, wapelelezi na askari Polisi wa kawaida.
Mauaji ya mtawa huyo, yalitokea juzi
mchana katika eneo la Ubungo Riverside, jijini humo, ambapo alipigwa risasi na
watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi na kumpora Sh milioni 20 pamoja na nyaraka
mbalimbali za ofisi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya
Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliwaambia waandishi wa habari ofisi
kwake jana kuwa Sista Cresencia wakati anapigwa risasi, alikuwa ameongozana na
wenzake, ambao ni Sista Brigita Mbaga (32) na dereva wao Mark Mwarabu,
aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up, yenye namba T213 CJZ.
Kova alisema wakati watawa hao,
wakitoka katika Benki ya CRDB Tawi la Mlimani City, walipofika Ubungo Riverside
kulipa deni la chakula katika duka la Thomas Francis, ndipo walitokea watu hao
wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi wakiwa na pikipiki, ambayo haikusomeka
namba, huku mmoja akiwa na bunduki aina ya SMG.
“Yule dereva wa gari la masista
walimpiga risasi katika kidole gumba cha mkono wa kulia na kisha kumpiga mtawa
huyo risasi ya kifuani na kupora kiasi hicho cha fedha na nyaraka hizo,” alisema Kova.
Alisema kuwa jambo kubwa walilogundua
ni kuwa matukio mengi ya ujambazi, hasa unaohusisha wananchi kuporwa kiasi
kikubwa cha fedha, yanaanzia katika mabenki, hivyo kuna uwezekano wa watu ambao
si waaminifu, wanafanya uhalifu huo.
Alisema kuwa katika matukio ya aina
hiyo, majambazi huwafuatilia wateja wanapoingia au kutoka katika benki
mbalimbali.
Alisema imeonekana kwamba mara nyingi
benki, zinapohitaji kusafirisha pesa nyingi, hutumia askari au taasisi nyingine
za usalama kusafirisha fedha zao.
“Tunawaomba mameneja wa benki zote,
kuhakikisha wanawahimiza wateja wake kutumia njia mbadala za kusafirisha pesa
nyingi, kama vile matumizi ya hundi, kufanya miamala bila kadi, matumizi ya
kadi za kutolea fedha (ATM) na njia nyingine ambazo ni salama.
“Matukio kama haya, yanaonesha ni wazi
huu utaratibu wa watu kutoa pesa nyingi kutoka benki na kwenda kufanya malipo
si salama. Kuna baadhi ya huduma, kwa mfano kuna baadhi ya nchi ambazo ni
sheria mtu haruhusiwi kutembea na fedha nyingi, kwa hiyo ni muhimu kwa sisi
wenyewe tukajielewa kwanza,” alisema Kova.
Alisema pia wanaomba mameneja wa benki,
kuhakikisha benki zao zinakuwa na kitengo maalumu cha ushauri wa masuala ya
usalama kwa wateja wao.
Alifafanua kuwa kama mteja atafika
katika benki zao na akahitaji kutoa fedha nyingi ni vyema wakamshauri ;na kama
atakaidi, benki ichukue hatua ya kutaarifu Polisi.
Aidha, alitaka wafanyabiashara na
taasisi mbalimbali, zisitumie njia za mkato katika usafirishaji na uhifadhi wa
pesa zao kwa faida ya usalama wa maisha na mali zao.
Aidha, Kova alisema katika kukabiliana
na uhalifu wa aina hiyo wa kutumia pikipiki, wamezikamata pikipiki 668, ambazo
wanazitilia shaka na wanazifanyia ukaguzi zaidi. Pia, zipo ambazo zimekamatwa
kuhusiana na makosa mengine ya barabarani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ POLISI WATANGAZA MSAKO MKALI KWA WATUHUMIWA WA MAUAJI YA SISTA WA KANISA KATOLIKI. ”
Post a Comment