Wednesday, June 25, 2014
SERIKALI YATUMIA MAWAZIRI WANNE KUJIBU HOJA YA UKOSEFU WA AJIRA NCHINI
Do you like this story?
SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu tatizo
la ajira nchini, huku wanasiasa waliozungumzia tatizo hilo kuwa ni bomu,
wakitakiwa kutoa ushauri wa namna ya kulitegua au kupunguza athari zake kama
likilipuka.
Mbali na ushauri huo, Serikali pia
imewataka wanasiasa wanaotumia tatizo hilo kisiasa, kuonesha mfano wa kusaidia
vijana katika majimbo yao kwanza, badala ya kusubiri siku wakipewa nchi.
Mawaziri wanne walitumia muda wao jana
kujibu hoja hiyo, ambayo ni hoja lulu kisiasa, kutokana na hali halisi kuwa
sehemu kubwa ya Watanzania ni vijana, hivyo inatazamwa na wanasiasa wengi kuwa
ndio watakuwa sehemu kubwa ya wapiga kura.
Kutokana na umuhimu wa ajira katika
siasa za leo, Naibu Spika, Job Ndugai hivi karibuni alisema Mtanzania mwenye
nia ya kugombea urais mwaka 2015, ili aeleweke kwa wananchi, ni lazima aeleze
mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima
lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule, lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza
darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na vyuo vikuu.
"Nazungumza kutoka moyoni kabisa.
Hizi ni dakika za mwisho za Serikali ya Awamu ya Nne, wale wanaojipanga kwa
Awamu ya Tano kama hawataongelea ajira, basi waandike wameumia,” alisema Ndugai.
Alianza Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudentia Kabaka, ambaye alikiri kuwa ajira ni tatizo, lakini akafafanua kuwa
si la Tanzania tu, bali pia ni tatizo la kimataifa.
Alisema katika utafiti uliofanyika
mwaka 2012, ilionekana ajira ya muda mrefu, inayompa mwajiriwa hifadhi kuwa
imeongezeka kwa asilimia 13.5. Ongezeko hilo limetolewa katika sekta ya umma,
ambayo imetoa asilimia 35.8 ya ajira huku sekta binafsi ikitoa asilimia 64.2 ya
ajira.
Kutokana na mchango mkubwa wa sekta
binafsi katika ajira, Kabaka alisema Serikali imekuwa ikiweka mazingira rafiki
kwa wawekezaji, ikiwemo ujenzi wa barabara, kuboresha upatikanaji wa nishati ya
umeme na mawasiliano.
Alisema wakati wanasiasa wanasema
Tanzania kuna tatizo kubwa la ajira, ambalo kitakwimu ni asilimia 11.7, nchini
Afrika Kusini ni asilimia 24.9.
“Sasa kabla ya kusema ukipewa nchi
utatoa ajira, tuoneshe kwanza katika jimbo lako. Umefanyaje kuongeza ajira
katika sekta isiyo rasmi…msidanganye wananchi na kuwachonganisha na Serikali,” alisema.
Kuhusu fursa ya kufanya mafunzo kwa
vitendo, Serikali imezungumza na Chama cha Waajiri (ATE) ili watoe fursa hizo
kwa wanafunzi wanaotoka katika vyuo mbalimbali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Asiye na
Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, aliamua kuonesha mfano kwa kuanza kutoa
ushauri.
Alitoa hatua kumi, alizotaka waajiriwa
watarajiwa walio katika soko ambao hawajapata ajira na walio vyuoni na
wanaojiandaa kujiunga na vyuo mbalimbali, ili wapate ajira.
Kwanza aliwataka wanafunzi wanaojiunga
na vyuo, kama wanataka kuajiriwa, wachukue fani za sayansi, teknolojia na uhandisi.
Pili, aliwataka wanaosomea uhandisi na
sayansi, wachanganye fani hiyo na fani ya usimamizi wa biashara.
Tatu, aliwataka wanaochukua fani za sanaa, pia kuchukua fani za usimamizi, kwa maana ya Shahada ya Uzamili ya Usimamizi (MBA).
Tatu, aliwataka wanaochukua fani za sanaa, pia kuchukua fani za usimamizi, kwa maana ya Shahada ya Uzamili ya Usimamizi (MBA).
Profesa Mwandosya pia aliwataka
waajiriwa watarajiwa, wasidharau lugha za Kiswahili na Kiingereza ;na
wazizungumze kwa ufasaha, lakini akawataka pia kuchukua lugha moja katika ya
Kifaransa, Kihispania, Kireno na Kichina.
Hatua nyingine waliyoshauriwa kuchukua
ni kutoogopa kushindana katika soka la nje, ikiwemo soko la Afrika Mashariki,
Afrika na sehemu nyingine duniani. Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, katika soko
hilo la ajira kuna Wakenya, Warwanda na Waganda.
Aliwataka wanafunzi vyuoni kuanza
kujijengea kichwani dhana ya kujiajiri, kwa kuwa ni jambo zuri ili wasingoje
kupata ajira za Serikali.
Wasomi hao pia walitakiwa waache
kuchagua kazi wala ngazi ya kuanzia kazi, kwa kuwa hata aliyesomea uhandisi
akianzia kazi ya fundi mchundo, atapanda haraka. Pia, aliwataka wajiamini, wawe
wabunifu na kujiunga katika vikundi ili wawezeshwe.
Credit: Habari Leo
Credit: Habari Leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ SERIKALI YATUMIA MAWAZIRI WANNE KUJIBU HOJA YA UKOSEFU WA AJIRA NCHINI ”
Post a Comment