Tuesday, June 3, 2014

TAIFA STARS BAADA YA KUITUNGUA ZIMBABWE, SASA YAANZA MAWINDO YA KUWANG`OA MSUMBIJI.




Timu ya taifa ya soka Tanzania Taifa Stars, chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij, inatarajia kuingia kambini Jumatano ijayo kwa ajili ya kujiwinda na mchezo dhidi ya Msumbiji  kuwania kupangwa hatua ya makundi ili kusaka tiketi ya fainali za AFCON zitakazochezwa Morocco hapo mwakani.

Taifa Stars imewasili kutokea Harare ambako ilifanikiwa kufuzu hatua inayofuata  baada ya kuingoa Zimbabwe kwa jumla ya magoli 3 - 2.

Stars ilishinda bao 1-0 katika mchezo wa kwanza jijini Dar es salaam na kufanikiwa kutoka sare ya 2-2 mjini Harare, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Shujaa wa Tanzania katika mchezo huo wa marudiano walikuwa ni nahodha Nadir Haroub `Canavaro` na mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu.

Afisa habari wa Shirikisho  la mpira wa miguu Tanzania TFF,  Boniface Wambura Mgoyo amesema timu hiyo inataraji kuingia kambini kwa mara nyingine kujiwinda dhidi ya Msumbiji Jumatano ijayo kwasababu mwalimu anatakiwa kupata muda wa kutosha kufanyia marekebisho  makosa yaliyojitokeza mechi zilizopita.

Taifa Stars inataraji  kucheza  dhidi ya Msumbiji hapo Julai 19 na 20 mwaka huu sanjari na timu nyingine za ukanda wa CECAFA Kenya, Uganda na Rwanda ambazo zimepenya hatua inayofuata.

Wakati huo huo, mtandao huu umekutana na John Jambele ambaye ni miongoni mwa  wadau ambao wanaonesha kufurahishwa na matokeo bora ya Taifa Stars ambapo anawataka wachezaji hao kukaza uzi zaidi na kutobweteka kwa hatua waliyofikia.

0 Responses to “TAIFA STARS BAADA YA KUITUNGUA ZIMBABWE, SASA YAANZA MAWINDO YA KUWANG`OA MSUMBIJI.”

Post a Comment

More to Read