Friday, June 20, 2014
VITAMBULISHO VYA KUPIGIA KURA KUTOLEWA UPYA, SASA WENYE MIAKA 17 RUKSA KUJIANDIKISHA.
Do you like this story?
VITAMBULISHO vya kupiga kura nchini,
vitatolewa upya kwa wananchi wote, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuboresha
daftari la kudumu la wapigakura. Mchakato huo wa kutoa vitambulisho upya,
utakaotekelezwa Septemba mwaka huu, utagharimu Sh bilioni 293 .
Tofauti na vitambulisho vya awali vya
karatasi vilivyotolewa kwa mara ya kwanza mwaka 2004, vipya vitakuwa vya
plastiki. Vimebadilishwa kutokana na matumizi ya teknolojia mpya katika
uandikishaji.
Teknolojia itakayotumika ni ya
Biometric Voter Registration (BVR), ambayo inachukua au kupima taarifa za mtu
za kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuzihifadhi katika Kanzidata (database)
kwa ajili ya utambuzi.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema hayo jana wakati akifungua mkutano
kati ya tume na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, kuhusu uboreshwaji wa
daftari la wapiga kura.
Alisema katika uboreshaji huo,
wapigakura wa zamani, kwa maana waliokuwa kwenye daftari la sasa, watatakiwa
kwenda katika vituo vya kujiandikisha kuchukuliwa taarifa zao hasa alama za
vidole, picha na saini zao katika mfumo mpya wa BVR na hatimaye kupewa
vitambulisho vipya.
Alisema vitambulisho hivyo vipya,
vitatolewa papo hapo uandikishaji ukikamilika na vitakuwa vya plastiki ngumu na
namba ya mpigakura itakayoonekana kwenye kitambulisho hicho, itakuwa ni ya
kudumu na pekee kwa mpiga kura husika.
“Vitambulisho hivi vitatumika kupiga
kura katika uchaguzi mkuu ujao pamoja na kura ya maoni ya Katiba mpya na
kuhitimisha matumizi ya vitambulisho vya wapiga kura vya awali,” alisema
Lubuva.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo
kuhusu maandalizi hayo kwa kutumia mfumo wa BVR, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius
Malaba alisema wapigakura watakaokuwa na kadi za zamani, watatakiwa kwenda na
kadi hizo katika kituo cha kujiandikisha kurahisisha kuhamisha taarifa zao za
awali katika mfumo mpya.
“Hata hivyo, kupotea ama kuharibika kwa
kadi ya awali, hakumzuii mpiga kura kwenda kituoni kujiandikisha na kupewa kadi
mpya,” alisema.
Wenye umri miaka 17 Alisema kundi
lingine litakalohusika katika uboreshwaji huo ni watu ambao ifikapo siku ya
uchaguzi mkuu mwakani, watakuwa wametimiza umri wa miaka 18.
Pia, wale ambao hawakuwahi
kujiandikisha katika madaftari yaliyopita kwa sababu mbalimbali, watahusika
katika uboreshaji wa daftari.
Alisema baada ya kukamilika kwa
uboreshwaji huo, daftari la awali litawekwa wazi katika maeneo husika na tarehe
za ukaguzi, zitatangazwa ili kila aliyejiandikisha kwenda kukagua na kuona kama
taarifa zake, zimeandikwa na kuchukuliwa kwa usahihi.
“Kipindi hicho pia kinatoa nafasi kwa
wapigakura waliojiandikisha katika kata kuweka pingamizi kwa wale
watakaoonekana wameandikishwa katika daftari lakini hawana sifa kama wasiokuwa
raia au wasiotimiza umri unaotakiwa kisheria,” alisema.
Alisema matumizi ya mfumo wa BVR,
yataweza kutoa majibu kwenye changamoto zilizojitokeza katika mifumo mingine
iliyotangulia na kuwezesha kuondoa wapigakura, waliojiandikisha zaidi ya mara
moja, kutambua wapigakura siku ya uchaguzi na kuhamisha wapigakura waliohama.
BVR ni uandikishaji tu Hata hivyo,
Lubuva alisema mfumo huo wa BVR utatumika kwa ajili ya kuandikisha wapigakura
pekee na si kwa ajili ya kupiga kura kielektroniki au vinginevyo.
Alisema matumizi ya mfumo huo,
yametokana na changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya Optical Mark
Recognition (OMR) na kufanya daftari la kudumu la wapigakura kuwa na kasoro na
kusababisha wadau wa uchaguzi kuhoji uhalali wake.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari,
Lubuva alisema vifaa kwa ajili ya kazi hiyo vimekwishaagizwa. Tume itavipokea
Agosti mwaka huu ili kuanza uboreshaji huo huku vifaa vichache kwa ajili ya
mafunzo kwa watendaji vitapokewa mwezi Julai na kuanza mfunzo hayo.
Uandikisha kwenye vitongoji Alisema kwa
sasa uandikishaji utafanyika katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa,
tofauti na awali ambapo vilikuwa katika ngazi ya mtaa. Sasa vituo vya
kujiandikishia, vimeongezeka kutoka 24,919 hadi 40,015 ili kuwa karibu na
wananchi na kuongeza mwamko wa kujiandikisha na kupiga kura. Mchakato wa
uandikishaji ukianza, huduma zitakuwepo kwa siku 14 kituoni.
Maandalizi Alisema maandalizi ya awali
yamekamilika, kinachofuata ni mafunzo na kuanza uboreshwaji wa daftari
utakaogharimu Sh bilioni 293 wanazopata kutoka serikalini na tayari sehemu ya
fedha, wameshapokea na kutumika kukagua vituo .
Naibu Katibu wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura na Tehama, Dk Sist Cariah, akizungumzia suala la vitambulisho vya
taifa na hivi vya wapigakura, alisema vitambulisho hivyo ni tofauti kwani wao
wanatoa kwa ajili ya kukamilika kwa muda maalumu lakini vile vya taifa ni
endelevu.
Alisema kwa sasa, vitambulisho vya
taifa hawajakamilisha kutoa hata Dar es Salaam pekee hivyo ni vigumu kutumika
kwa uchaguzi ujao na kura ya maoni kwa Katiba mpya lakini wakikamilisha
vitambulisho vya taifa , vitatumika katika uchaguzi.
Alisema katika mfumo huo mpya,
watawasiliana na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuweza kuwaondoa
wote waliofariki kwa kutumia takwimu za hospitalini na vyeti vya vifo
vitakavyotolewa.
Credit: Habari Leo
Credit: Habari Leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ VITAMBULISHO VYA KUPIGIA KURA KUTOLEWA UPYA, SASA WENYE MIAKA 17 RUKSA KUJIANDIKISHA.”
Post a Comment